Simba imeshauriwa uwepo wa makipa Ally Salim anayepewa nafasi kwa sasa na Hussein Abel ambaye hajaanza kucheza kutowasahaulisha na kuona wapo salama golini badala yake wafanye haya.
Kocha wa makipa wa Mtibwa Sugar, Patrick Mwangata alisema Salim ameanza kukomazwa ila haimaanishi wamtegemee kwenye michuano ya kimataifa, kwani yapo mambo ambayo hawezi kuyafanya kama anavyofanya Aishi Manula na kipa wa Yanga, Diarra Djigui.
“Kipa anatakiwa kuchunguzwa kwa umakini, mfano kama Diarra wa Yanga mabeki wake wanaweza wakampa bakipasi kwa amani kabisa, ila Simba unaona mabeki wanavyofanya kazi kubwa ya kuhakikisha wanamlinda (Salim),” alisema.
“Kama wanataka kuwakomaza Salim na Abel basi wawape muda wasije wakaanza kuwalaumu baadaye watakapokutana na timu zinazotumia nafasi moja ya makosa kufunga hasa michuano ya CAF, kwa jicho la kiufundi kwangu Salim bado hana sifa za kuaminiwa awe kipa namba moja.”
Aliyekuwa kocha wa makipa wa Yanga, Peter Manyika alisema klabu kongwe zinahitaji makipa wakomavu waliopitia mikimiki mingi iliyowakomaza, huku wengine wakiendelea kuwapa uzoefu kama Salim na Abel.
“Simba na Yanga zinahitaji aina ya makipa waliokomaa tayari kama Manula na Diarra hata timu ikielemewa wanaisaidia. Salim na Abel wanatakiwa kukomazwa zaidi, huko mbeleni watakuja kuwasaidia, ila kwa sasa kwa majukumu inalazimika yawe kwa Manula kama atapona haraka ama huyo mgeni ambaye bado hatujaona uwezo wake,” alisema.