Nyota mpya wa JS Soura, Adam Salamba amejiapiza huko Algeria kwa kuwa ahidi mabao mashabiki wa timu hiyo ikiwa ni siku chache tangu atambulishwe kuwa mchezaji rasmi wa vigogo hao kitokea Namungo.
JS Saoura imetumia mitandao yao ya kijamii kumtambulisha mshambuliaji huyo kwa kusema atawatumikia kwa misimu miwili ijayo huku akikabidhiwa jezi namba tisa (9) na tayari amejumuika na wachezaji wenzake kwa ajili ya maandalizi ya msimu ujao.
Salamba amesema, ”Nashukuru kwa imani ambayo benchi la ufundi na klabu kwa ujumla wameonyesha kwangu, nimeanza maisha mapya huku Algeria na ahadi yangu kwao ni kuhakikisha nafanya kila ambalo litakuwa ndani ya uwezo wangu ili kuisaidia timu kufikia malengo.
“Hii ni mara yangu ya kwanza kucheza soka Algeria lakini naamini kuwa nitakuwa na msimu mzuri kwa kushirikiana na wachezaji wenzangu,” alisema mshambuliaji huyo wa zamani wa wekundu wa msimbazi, Simba SC.
Salamba ambaye aliwahi kucheza soka la kulipwa Kuwait, atakuwa Mtanzania wa pili kuichezea JS Saoura nyuma ya Ulimwengu ambaye ndani ya michezo 13 aliyoichezea timu hiyo 2019 akitokea Al-Hilal Club ya Sudan alipachika bao moja.
Wadau na mashabiki mbalimbali wa timu hiyo baada ya kutambulishwa kwa Salamba wametoa maoni tofauti kwenye mitandao yao ya kijamii kutokana na usajili wa mchezaji huyo, Hammani EL Amine alisema: ”Kwa muonekano wa kawaida anaonekana kuwa ni mshambuliaji mzuri, karibu sana Algeria. Tunataka mabao.”
Nouar Dehina amesema, ”Huu unaweza kuwa usajili bora, nimejaribu kumfuatilia anaonekana kuwa ni mshambuliaji mzuri mwenye uwezo wa kutumia nguvu na akili.”
Kwa upande wake, Khalifa Hassan amesema, “Siwezi kusema chochote kwa sasa kwa sababu ni mshambuliaji mgeni kabisa machoni mwangu labda anaweza kuwa mzuri.”