Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Salamba: Shoo? Hapana! Ni boli, maokoto

Salambaaa Adam Salamba

Mon, 26 Feb 2024 Chanzo: Mwanaspoti

Ni mwendo wa maokoto tu. Mshambuliaji wa Kitanzania, Adam Salamba anayesimamiwa na The One ni kati ya wachezaji wenye bahati, kwani licha ya kuchukuliwa poa amekuwa akipata madili ya maana kutoka klabu moja kwenda nyingine nje ya mipaka ya Tanzania.

Salamba ambaye alijipatia umaarufu nchini akiwa na Lipuli ya Iringa wakati huo ikiwa Ligi Kuu Bara kabla ya kutua Simba alikocheza kwa kipindi kifupi, kwa sasa ni mchezaji wa Ly Stade Club ya Libya.

Miezi michache nyuma, Salamba alikuwa mchezaji wa Ghazl El Mahalla ya Misri lakini alishindwa kuonyesha makali yake.

Usajili wa Salamba, Ghazl El Mahalla iliaminika mshambuliaji huyo anaweza kuleta mapinduzi kwenye safu yao ya ushambuliaji, wakati Mtanzania mwenzake, Himid Mao ‘Ninja’ akikiwasha zaidi ya michezo 20, Salamba alikuwa akisugua benchi mbele ya Abdo Yehia na Ahmed Ghoneim.

Mshambuliaji huyo kiwango chake kilishindwa kumshawishi Mohamed Ouda ambaye naye hata hivyo kibarua chake kiliota nyasi.

Kabla ya kujiunga na Ghazl El Mahalla, Salamba alikuwa mchezaji wa pili wa Kitanzania kusajiliwa na kuichezea JS Soura ya Algeria alikofuata nyayo za Thomas Ulimwengu.

Takwimu zinaonyesha Salamba wakati akiwa na miamba hiyo ya soka la Algeria, alicheza mchezo mmoja tu wa ligi ambayo ni maarufu kama Algerian Ligue Professionnelle, hakufunga wala kutoa asisti.

Timu ya kwanza kabisa kwa Salamba kuichezea nje ya Tanzania, ilikuwa Al-Jahra SC ya Uarabuni ambako alikaa kwa kipindi kifupi kutokana na janga la virusi vya corona hivyo alilipwa chake kulingana na mkataba wake ulivyokuwa.

Yusuph Kajuni ambaye ni Mtanzania anayeishi Algeria amewamwagia sifa maajenti wa mchezaji huyo huku akiamini kama wangeamua kuwashika mkono na wachezaji wengine basi ni wazi ulaji kwa wachezaji wa Kitanzania ungekuwa nje nje kama ilivyo kwa mchezaji huyo.

“Nimemwona Salamba akiwa hapa (Algeria), ni mchezaji mzuri lakini nadhani JS Soura ilikuwa kubwa kwake ndio maana alishindwa kuonyesha ubora wake, nadhani Ulimwengu angalau alionyesha kwa kiasi fulani,” anasema mdau huyo wa Nje ya Bongo.

Kwa upande wake, Mohamed Badru ambaye ni kocha wa vijana wa Azam FC, anasema, “Kucheza nje kuna mambo mengi, kwanza unatakiwa kuwa na watu wenye nguvu ya ushawishi na wenye kuaminika, kingine ambacho ni muhimu sana unaweza kucheza kwa wenyewe kukuona na sio kupelekwa tu kwao.”

Salamba ndiye mchezaji pekee kutoka Tanzania anayesimamiwa na The One huku kwa Kenya akiwa ni Nicholas Kipkirui anayeichezea Gor Mahia, pia yupo kiungo wa TP Mazembe ya DR Congo, Merceil Ngimbi Vundi.

Ly Stade Club inamatumaini makubwa na Salamba aliyezaliwa Novemba 25, 1999 huku mashabiki wake wakiamini uzoefu wake unaweza kuwa chachu ya kuifanya timu hiyo kupanda daraja.

MSIKIE MWENYEWE

Salamba anasema maisha yake kiuchumi yamebadilika akiyatofautisha na kabla ya kuanza kucheza nje na akili yake inapanuka kutokana na mazingira ya aina tofauti anayokutana nayo.

“Soka limenifanya nipige hatua kubwa sana kimaisha, japokuwa siwezi kusema nimepata hiki na kile, hiyo ndio sababu inayonifanya nisiridhike, pia unapokutana na wachezaji mbalimbali unajifunza vitu vingi, jambo lingine linalonipa nguvu nikiwaona wachezaji wa kigeni kwenye ligi yetu najiuliza mimi nitashindwa nini,” anasema.

Tayari amecheza nchi nne tofauti Algeria, Misri, Kuwait na sasa Libya.

“Nilipata shida sana Kuwait kuzizoea tamaduni zao, hilo halikuwa rahisi kwangu, ingawa ikanifunza nakunifanya niwe najaribu kuchangamkia fursa za nchi mbalimbali,” anasema. Salamba anasema kutokana na kuzunguka kwake ameanza kujifunza kuzungumza Kiarabu, ili kupata urahisi wa kuwasiliana na wachezaji wenzake.

“Nazungumza baadhi ya maneno, ila kwa asilimia kubwa nasikia kile kinachoongelewa.”

“Karibu Sana Libya, hapa ni sawa na Tanzania tu,” anasema Official King kwenye utambulisho wa mchezaji huyo siku chache zilizopita.

Chanzo: Mwanaspoti