Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Sakho: Naanzia nilipoishia

Sakhooooooooooooooo Pape Sakho

Mon, 5 Sep 2022 Chanzo: Mwanaspoti

Straika wa Simba, Pape Sakho amesema kiwango alichomaliza nacho msimu uliopita kwenye mashindano ya ndani na kimataifa amepanga kukiendeleza msimu huu.

Sakho alisema Simba msimu huu ina wachezaji wengi bora zaidi ya uliopita ambao hakufanikiwa kufanya vizuri mwanzoni kutokana na majeraha ambayo yalikuwa yakimsumbua.

Alisema baada ya kurejea mashindano ndani watakuwa na ratiba ngumu mechi za ligi na zile za CAF, kila baada ya siku tatu lakini kutokana na mazingira yalivyo wanakwenda kupambana kupata matokeo mazuri.

Nyota huuyo anataka kila mechi acheze kwa kiwango bora ili kutimiza jukumu lake ya kufunga mabao, kutengeneza nafasi kwa wenzake, kuanzisha mashambulizi hatari na kufanya kila kilichokuwa bora uwanjani.

“Nataka kuonyesha ubora katika mashindano ya ndani ili timu iweze kuchukua ubingwa wa ligi pamoja na Kombe la Shirikisho (ASFC), bila kusahau kutetea ubingwa wa Kombe la Mapinduzi,” alisema Sakho.

“Tumepoteza taji la kwanza Ngao ya Jamii sidhani kama litakuwa jambo rahisi kwetu kukubali kupoteza mataji mengine ya ndani ushindani ni mkubwa ila tunakwenda kupambana ili kuhakikisha malengo tunayafikia.

“Ili niweze kuonyesha ubora huo sio mashindano ya ndani, bali nimepanga kufanya hivyo katika Ligi ya Mabingwa Afrika kwani huko nitaipa timu mafanikio na kufika kwenye hatua ya mbali zaidi ya msimu uliopita.

“Nikifanikiwa kuonyesha ubora katika Ligi ya mabingwa Afrika maana yake mbali ya yale mafanikio ya timu binafsi nitafika mbali zaidi katika maisha yangu ya soka ikiwemo kuchukua tuzo kama msimu uliopita.

“Naendelea kujiandaa ili kufikia malengo kama haitoshi nipo tayari kutetea tuzo ya bao bora niliyochukua msimu uliopita na ule ubora niliomaliza nao mashindano hayo nitakwenda kuonyesha zaidi msimu huu.”

Katika hatua nyingine Sakho aliongeza kuwa akionyesha makali na timu kufikia mafanikio itakuwa na faida hata upande wake kuzivutia timu nyingine kubwa zaidi ya zile zilizokuwa zinamhitaji msimu uliopita ikiwemo RS Berkane kutokea Morocco.

Kocha wa Simba, Zoran Maki alisema Sakho ni mmoja wa wachezaji wenye kasi na anawasumbua mabeki wa timu pinzani, mtulivu anapokuwa na mpira, anaweza kutengeneza nafasi za kufunga na muda mwingine hufunga kulingana na aina ya shambulizi lilivyo.

“Miongoni mwa wachezaji wenye kasi kila kocha anatamani kuwa nae, anapenda kutoa mchango kila nyakati anapokuwa uwanjani kutokana na uchezaji wake ila nimemueleza natamani kumuona anapunguza mambo mengi yasiyokuwa na ulazima pindi anapokuwa na mpira atakuwa mchezaji mkubwa zaidi ya sasa,” alisema Zoran.

Simba itakuwa na ratiba ngumu katika mechi za kimashindano kwani Septemba 7, itacheza na KMC ndani ya siku tatu inatakiwa kusafiri kwenda Malawi kucheza mchezo wa Ligi ya mabingwa Afrika mzunguko wa kwanza dhidi ya Nyasa Big Bullets Septemba 10.

Baada ya mchezo huo itakuwa na siku nyingine nne kurudi nchini na kusafiri hadi Mbeya kucheza dhidi ya Tanzania Prisons Septemba 14, Simba itakuwa na siku nyingine tatu kusafiri kurudi Dar es Salaam, kufanya maandalizi kwa ajili ya kucheza na Nyasa Big Bullets mchezo wa marudiano Septemba 17.

Simba baada ya kumalizana na Nyasa Big Bullets kisha kufahamu hatma yake itasafiri hadi Mbeya kucheza mechi ya ligi dhidi ya Mbeya City kisha baada ya mchezo huo itasafiri tena hadi Singida kucheza dhidi ya Singida Big Stars katika Uwanja wa Liti mjini Singida.

Chanzo: Mwanaspoti