Hii ni taarifa njema kwa mashabiki wa Simba SC ambao walikuwa na hofu baada ya nyota wa timu wao, Pape Othman Sakho na Jean Baleke kupata majeraha kwenye mechi ya kirafiki dhidi ya Al Hilal ya Sudan iliyopigwa kwenye Uwanja wa Benjamini Mkapa, Februari 5, 2023.
Sakho alishindwa kuendelea na mchezo huo baada ya kupata maumivu wakati Baleke alitolewa uwanjani kwa msaada wa machela hali iliyozua taharuki miongoni mwa mashabiki.
Daktari wa timu, Edwin Kagabo amesema nyota hao hawakupata madhara makubwa hivyo wanaendelea vyema na kesho wataendelea na programu ya mazoezi kama kawaida.
"Sakho na Baleke walipata maumivu katika mchezo wa jana lakini hawakupata madhara makubwa hivyo wanaendelea vizuri na kesho wataendelea na programu ya mazoezi," alisema Dk Edwin.
Kuhusu Augustine Okrah ambaye naye alishindwa kuendelea na mchezo Dk Edwin amesema wanasubiri majibu ya vipimo vya CT Scan ili kujua ukubwa wa jeraha lake.
Wachezaji wa Simba SC walipewa mapumziko ya siku moja baada ya kumaliza mchezo wa jana na watarejea kesho kuanza maandalizi ya mechi ya kwanza ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Horoya itakayopigwa Februari 11 nchini Guinea.