Mshambuliaji kinara wa Yanga Sc, Fiston Mayele raia wa Congo amesema amepata ofa ya kwenda kucheza katika vilabu vikubwa barani Afrika na nje ya Afrika lakini kwa heshima aliyoipata akiwa Yanga ameamua kuwapa nafasi ya kwanza waajiri wake hao ili waone namna ya kumbakisha.
Mayele ambaye ni mshindi wa Tuzo ya Mchezaji Bora wa Ligi Kuu Bara, mshindi wa Tuzo ya Mchezaji Bora wa Ligi na mfungaji Bora wa Michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika amesema hayo ikiwa leo ndiyo siku ambayo uongozi wa Yanga na wawakilishi wake wanakaa mkutano wa mwisho kukubaliana mchezaji huyo kuendelea kusalia Yanga ama kuondoka.
"Ni kweli kuna klabu ya Tanzania ilituma ofa, ila kwa heshima niliyoipata Yanga, sijawahi kuwa na mafanikio kama niliyoyapata Yanga, kwa hiyo mimi hata nikija kuondoka Yanga siwezi kucheza Tanzania nje ya Yanga.
"Ofa nyingine nimepokea kutoka Ulaya na Uarabuni, Ubelgiji, Qatar na nchi nyingine.
"Mimi bado ni mchezaji wa Yanga mpaka 2024, Jumamosi usiku timu ikirejea, tutakaa na uongozi kikao cha mwisho, Jumatatu tutajua kama nitaondoka au nitabaki Yanga," amesema Mayele.