Mabosi wa klabu ya Azam imeanza mchakato wa kumalizana na viongozi wa timu ya US Goree baada ya kikosi hicho cha Chamazi kumsajili mshambuliaji, Alassane Diao ambaye inaelezwa bado ana mkataba nao.
Juzi kupitia mitandao ya kijamii ya Goree ilitoa barua ya kusikitishwa na maamuzi yaliyofanywa na Azam ya kumtangaza mchezaji wa timu hiyo huku akiwa bado ana mkataba wa kuendelea kuichezea.
"Kwa kukumbushana US Goree inapenda kudokeza mchezaji Alassane Diao bado ana mkataba na klabu yetu na hakuna mazungumzo yoyote yaliyoanzishwa na Azam FC kuhusu kumuachia," ilisomeka taarifa hiyo.
Aidha taarifa hiyo ilieleza Diao hawezi kufuzu wala kucheza katika klabu nyingine nchini Senegal au kimataifa kabla ya kumalizika kwa mkataba wake mahakamani ambao bado umesalia na timu hiyo.
"Kwa kuheshimu maandishi yanayosimamia soka, Goree inasisitiza dhamira yake ya kufuata sheria za uhamisho zilizowekwa na FIFA na kuhakikisha maslahi ya klabu na wachezaji chini ya mkataba."
Wakati taarifa hiyo ikibamba, Ofisa Mtendaji Mkuu wa Azam, Abdulkarim Amin 'Popat' alisema suala hilo litamalizika na hakuna kitakachoharibu dili la mchezaji huyo kuichezea Azam kwa msimu ujao.
Hata hivyo, inafahamika kuwa nyota huyo aliwaambia viongozi wa Azam hana mkataba alikotoka jambo lililowafanya mabosi hao kumpa mkataba wa miaka miwili huku wao wakiwa hawajui chochote.
Raia huyo wa Senegal ni mchezaji wa nne kusajiliwa kwa msimu ujao huku wengine wakiwa ni Feisal Salum 'Fei Toto' aliyetoka Yanga, Gibril Sillah (Raja Casablanca) na Cheikh Sidibe wa Teungueth.