Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Sakata la Lawi Simba, Coastal mtihani kwa TFF

Lawi Ally Salim Msz Sakata la Lawi Simba, Coastal mtihani kwa TFF

Thu, 18 Jul 2024 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Sakata la klabu ipi ina haki ya kummiliki beki Lameck Lawi, kati ya Simba na Coastal Union bado limebaki mikononi mwa Kamati ya Hadhi na Haki za Wachezaji iliyopo chini ya Shirikisho la Soka nchini (TFF), baada ya pande mbili jana kutoa maelezo mbele ya kamati hiyo, imeelezwa.

Lawi msimu uliomalizika aliichezea Coastal Union na ulipomalizika akauzwa Klabu ya Simba, lakini wamiliki wake hao wa zamani walirejesha hela kwa madai muda waliowekeana wa malipo ulimalizika, jambo ambalo limezua mvutano kwani upande wa pili pia unasema ulifuata taratibu zote.

Hata hivyo, juzi kila upande ulitoa ushahidi wake mbele ya kamati hiyo, Coastal Union, ikiwakilishwa na Katibu Mkuu wake, Omary Ayoub, huku Simba ikiwakilishwa na wanasheria wao.

Akizungumza nasi baada ya kutoa ushahidi mbele ya kamati hiyo Makao Makuu ya TFF, Karume, Ilala jijini Dar es Salaam jana, Katibu wa Coastal Union, Ayoub alisema shauri la beki wao, Lawi bado lipo chini ya Kamati ya Hadhi na Haki za Wachezaji sasa ndio watakaoamua endapo ni mchezaji wa Simba au atabaki Coastal Union.

Ayub alisema kuwa waliitwa kwenye kamati na kusikilizwa pande zote mbili na sasa wanasubiri shauri na maamuzi kutoka kwenye kamati hiyo. 

“Tunaimani na hivi vyombo vinavyosimamia, maamuzi yakiamua mchezaji aende Simba bure bila Coastal Union kupata chochote tutaridhia, pia tukiambiwa Lawi abaki basi hatuna pingamizi, tunaimani na kamati,” alisema Katibu huyo.

Kwa upande wa Simba, wanasheria wao baada ya kumalizika kutoa ushahidi wao waliondoka huku kamati ikiendelea kusikiliza mashauri mengine yaliyofika mezani kwao.

Wakati huo huo, winga mpya wa Simba, Joshua Mutale, amebainisha kuwa wachezaji wengi Afrika wanatamani kuichezea klabu hiyo kutokana na kuwa moja ya klabu kubwa barani humo, huku ikiwa ndani ya nafasi kumi kwa ubora.

Akizungumza nchini Ismailia ambako timu hiyo imeweka kambi ya maandalizi ya msimu mpya, Mutale ambaye amesajiliwa msimu huu akitokea Power Dynamos ya Zambia, amesema hata nchini kwao, hakuna mchezaji ambaye akitakiwa na klabu hiyo atakataa, kwani imejipambanua kwa kuwa na ubora chini ya Jangwa la Sahara, ukiondoa Mamelodi Sundowns na TP Mazembe.

"Nimekuja Simba ili irudie kutwaa mataji, kama ni ubora imeshakuwa bora barani Afrika na kila mchezaji barani humu anapenda kuichezea klabu hii, nami pia nimefurahi kupata bahati hiyo, lakini hiyo haitoshi, ni lazima mtu ufanye kazi ya ziada ili ukubalike na mashabiki ambao nguvu yao nimeiona hata kwenye mitandao ya kijamii, lakini kuipatia mafanikio klabu," alisema.

Alisema hasemi kwa sababu amejiunga na timu hiyo, ila viwango vya ubora kutoka Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF), ndivyo vinaongea, kuwa ni moja kati ya timu tatu ambazo zipo kwenye kumi bora ya viwango vya Afrika chini ya ukanda huo, huku saba zilizobaki zinatoka Afrika Kaskazini.

"Kwa ubora huu, sidhani kama kuna mchezaji yeyote anaweza kuikataa nafasi hii, ndiyo maana walivyokuja tu kuniambia wananihitaji, sikutaka tena kuongeza mkataba kwenye timu yangu," alisema.

Alisema kingine kilichomfanya akubali kutua Simba ni rekodi nzuri ya wachezaji wa Kizambia waliopita kwenye klabu hiyo.

"Wachezaji wengi wa Zambia waliopita hapa wamefanya vizuri kama Felix Sunzu, Clatous Chama na Moses Phiri, rekodi hii imenivutia sana, naamini hata mimi nitafuata nyayo zao na nafikiri ndiyo maana klabu hii imekuwa ikiwaamini wa kutoka kwetu," alisema.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live