NI wiki tatu au zaidi kuna sakata ambalo linaendelea kuhusu Feisal Salum 'Fei Toto' dhidi ya klabu yake ya Yanga.
Ni mgogoro wa kimkataba baina ya pande hizo mbili. Kiungo huyo amevunja mkataba lakini klabu hiyo haitaki kukubaliana na uamuzi wa mchezaji huyo kutoka Zanzibar.
Fei Toto anataka kuondoka, lakini klabu yake inamwambia kama anataka kuondoka basi afuate taratibu zinazotakiwa.
Kuna mengi yameelezwa na kutokea, ikiwamo Yanga kufungua shauri katika Kamati ya Sheria na Hadhi ya Wachezaji ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), na huko wakaamua kuwa Fei Toto ni mchezaji halali wa mabingwa hao watetezi wa Ligi Kuu Bara.
Nimeona mawakili wa mchezaji huyo wakiwa hawajaridhika na uamuzi huo, na kwa sasa wanajiandaa kwenda katika Mahakama ya Usuluhishi wa Masuala ya Michezo (CAS). Nadhani wao wanaamini haki haijatendeka kwa mteja wao.
Kwa sababu haya ni masuala ya mikataba na kisheria, basi tunawaachia wanasheria ambao waliotoa uamuzi na hao wanaotaka kwenye CAS.
Ila nilichoshangaa katika suala hili la Fei Toto ni ukimya wa Chama cha Wachezaji Soka Tanzania (SPUTANZA).
Chama hiki kiko kwa ajili ya wanasoka Tanzania nzima, lakini kwenye shauri hili naona wako kimya kiasi mchezaji anaonekana kama yupo peke yake sana.
Sisemi kama SPUTANZA wao wangeamua chochote, lakini hata wao kuna kitu wangesema kuonyesha wameguswa na hilo kama wengine walivyokuwa wakilisemea.
Tumeona huko nyuma chama hicho kikitoa matamko, kusimama na wachezaji, angalizo na hata kuwaonya wachezaji kuhusu masuala mbalimbali yanayofanana na haya, lakini hili imekuwa kinyume chake.
Mwaka 2015, SPUTANZA ilivalia njuga suala la Juma Kaseja na Yanga, ambapo iliiandikia barua TFF imtangaze mlinda mlango huyo ni mchezaji huru.
Hiyo ni baada ya Yanga kumfungulia mashtaka mchezaji huyo katika Mahakama ya Kazi ikimtaka Kaseja kuwalipa fedha wakimtuhumu kuvunja mkataba na timu hiyo.
Na kweli baadaye sakata liliisha na Kaseja akawa mchezaji huru.
Mwaka huo huo kulikuwa na kesi ya Ramadhani Singano 'Messi' wakati huo akiitwa dhidi ya Simba. Nayo ilikuwa ni ya kimkataba.
SPUTANZA iliwasilisha TFF nyaraka muhimu kuhusu mkataba wa winga huyo na Simba ili kumaliza mvutano uliojitokeza.
Kulikuwa na mvutano kati ya Messi na uongozi wa Simba baada ya winga huyo kudai kutoutambua mkataba wa miaka mitatu kati yake na klabu hiyo ya Msimbazi uliopo TFF.
Iliwasilisha nyaraka za mikataba miwili ya Messi na Simba baada ya kubaini kuna utata katika mkataba ambao mchezaji huyo akadai kutoutambua, huku yeye akiutambua ule ya miaka miwili.
Mwaka 2016, SPUTANZA iliingilia kesi ya klabu ya Simba kumfungia mchezaji wake Hassan Kessy kwa mechi tano baada ya kumchezea rafu mbaya mchezaji wa Toto African wakati huo, Edward Christopher.
Hata hivyo meneja wake, Athumani Tippo, alipinga hilo na kupeleka malalamiko huko.
Hiyo ni mifano michache tu inayoonyesha chama hicho kimefanya kazi kubwa sana kusaidia wachezaji Tanzania na soka kwa ujumla. Kwa hili mbona iko kimya? Imepatwa na nini? Au Fei Toto si mwanachama wao? Au hajaenda kupeleka malalamiko yake huko? Hapa inabidi chama hicho kitoe ufafanuzi hakiwezi kusema lolote, au kufanya chochote mpaka wapelekewe malalamiko rasmi?
Mashabiki wengi wamekuwa wakijiuliza imekuwaje? Mbona hakisikiki kwenye hili? Hata kisiegemee upande wowote ule, lakini kitoe japo msimamo wake na ushauri pia.