Staa wa Al Ittihad, Karim Benzema amekanusha vikali taarifa zinazosambaa kwamba yeye ni miongoni mwa watu wanaounga mkono magaidi.
Waziri wa mambo ya ndani wa Ufaransa alidai Benzema ana uhusiano na kundi la kigaidi la Muslim Brotherhood. Kauli za kwamba Benzema anashirikiana na kundi hilo la kigaidi iliibuka baada ya staa huyo kuweka wazi hisia zake kupitia mitandao ya kijamii juu ya mgogoro unaoendelea baina ya Palestina na Israel.
Kupitia ukurasa wake wa Twitter, Benzema aliandika: “Maombi yetu yote kwa watu wa Gaza na waathirika wote wa mabomu yanayorushwa katika eneo hilo ambayo hayawasamehi wanawake ama watoto.” Baada ya kauli yake hii Waziri wa Mambo ya Ndani wa Ufaransa, Gerald Darmanin alipofanya mahojiano na CNews channel alisema:
“Benzema ana uhusiano na Kundi la Muslim Brotherhood.” Mbali ya kusema hayo taarifa zinadai baadhi ya viongozi wanataka staa huyo apokonywe uraia wa Ufaransa huku kukiwa na ripoti pia anaweza kupokonywa hadi Tuzo ya FIFA Ballod D’or ambayo alishinda mwaka jana ikiwa atakutwa kweli na hatia ya kushirikiana na kundi hilo.
Kundi hili linatambulika kuwa ni kundi la kigaidi ndani ya Saudi Arabia na nchi nyingine jumla sita. Kwa mujibu wa Le Parisien, Mwanasheria wa Benzema amesema kwamba wapo kwenye mchakato wa kuchukua hatua za kisheria dhidi ya mwanasiasa huyo kwa sababu kauli zake zimemharibia jina lake na heshima. “Tumepanga kufungua mashtaka dhidi ya waziri, kwa kuzingatia sheria ya kutoataarifa za uongo juu ya mtu au kutoa lugha zisizofaa juu ya mtu kwa sababu Benzema hana uhusiano wowote na kundi hili.”
Hii sio mara ya kwanza kwa Benzema kuhusishwa kushirikiana na Wahuni, iliwahi kutokea hivyo mwaka 2021, ambapo alikutwa na hatia ya kushirikiana na kikundi cha wahuni kumtapeli mchezaji mwenzake Mathieu Valbuena.
Valbuena alitishiwa kwamba atoe pesa ama kikundi hicho cha wahuni kisambaze video zake za faragha alizochukuliwa na Benzema ndio alikuwa amesimama mstari wa mbele kumtaka Valbuena akilipe kikundi hicho ili mambo yaishe jambo lililozua hisia tofauti kwa staa huyo na baada ya uchunguzi kufanyika Benzema akakutwa na hatia ambapo alitakiwa alipe faini ya dola 84,000!