Sakata la beki wa Arsenal kujiondoa kwenye timu ya taifa ya England limeibuka tena, baada ya kupita muda mrefu tangu alipojiondoa kwenye kambi ya timu hiyo katika fainali za Kombe la Dunia kule nchini Qatar 2022.
Wiki iliyopita, kocha wa England, Gareth Southgate aliita kikosi kilichopo kambini kwa ajili ya mechi za kirafiki dhidi ya Brazil na Ubelgiji na jina la Ben White halikuwepo, alipoulizwa akasema amekataa mwenyewe asijumuishwe.
Lakini taarifa kutoka Telegraph zinadai sababu kubwa ya White kukataa kuitwa ni kocha msaidizi wa England, Steve Holland.
Telegraph imeripoti kwamba Holland na White walikwaruzana nchini Qatar, baada ya kocha huyo kuanza kumuuliza Kyle Walker maswali kuhusiana na Manchester City kabla ya kumgeukia White na kumuuliza pia.
White mwenye umri wa miaka 26, akamwambia Holland kwamba hana majibu juu ya maswali aliyomuuliza, hali hiyo ikasababisha kocha huyo kumwambia kuwa hana mapenzi na hajui chochote kuhusu mpira.
Mazungumzo hayo yanadaiwa kufanywa mbele ya timu nzima jambo ambalo lilimkera sana White na haikuchukua muda mrefu, baada ya mechi dhidi ya Wales ambayo ilimalizika kwa England kushinda mabao 3-0, ikatoka taarifa ya White kuondoka kambini.
Inaelezwa kwamba White alichukizwa na mazungumzo hayo na kuona kocha huyo ni kama alimdhalilisha.
Beki huyu aliwahi kusema mara kadhaa kwamba tangu akiwa mtoto hadi sasa amekuwa hafuatilii sana mpira wa miguu, muda mwingi huwa anautumia kwenye kufanya mazoezi na kucheza.
Kitu pekee anachokipenda ni kucheza na sio kufuatilia ndio maana hana taarifa nyingi kuhusu mchezo huu. “Huwa najiangalia mwenyewe kwa ajili ya uchambuzi, pia mechi za England kidogo, lakini siwezi kukaa kutazama mechi.’’