Ilianza kama utani vile, CEO wa Simba, Babra Gonzalez alirusha Clip akilalamika kukataliwa kuingia Uwanjani katika jukwaa la VVIP mechi dhidi ya Yanga.
Mamlaka na Shirikisho wakaja na ufafanuzi wa sababu za msingi zilizosababisha kukataliwa kuingia kwa Mtendaji huyo kwa kuwa alitaka kuingia na watoto watatu ambao kwa taratibu hawaruhusiwi eneo hilo.
Wakamruhusu aingie yeye peke yake lakini akagoma na kwa mujibu wa taarifa ya TFF wanadai alitoa lugha chafu na kuondoka.
Viongozi wa Simba nao walishutumiwa kwa kufanya vurugu wakilazimisha mmoja wa viongozi wao kuingia pasipo kuwa na kadi ya mwaliko.
Baada ya tukio hilo wanasimba wengi walilalamikia kitendo hicho na hawakutaka kusikia lolote kutoka TFF wala Bodi ya Ligi, wanaamini Kiongozi wao hajatendewa haki.
Pengine labda ni matukio kadhaa ya nyuma dhidi ya mdhamini mwenza GSM ambao Simba waligomea kuvaa nembo ya mdhamini huyo.
Kwa hiyo lilipokuja suala hilo, wengi waliona kama Mtendaji wao anafanyiwa makusudi kwa kauli zake juu ya sakata la nembo ya mdhamini mwenza.
Alisistiza hawatovaa na kweli kwenye mechi dhidi ya Yanga hawakuvaa na kubwa zaidi mpaka mabango ya uwanjani yaliondolewa.
Sasa kutokana na hilo la kuzuiwa uwanjani vigogo wengi wa Simba walitoa kauli ambazo ni dhahiri zinaonekana zina mlengo mmoja.
Viongozi hao wametaka kuwa na Uwanja wao, ambapo wazo hilo linaonekana kuungwa mkono na wanasimba karibu wote.
Sio jambo baya kama watafanikiwa azma yao hiyo lakini kuzungumza na kupanga ni jambo moja ila kutekeleza ni jambo jingine.
Tayari mwekezaji ndani ya Simba anatajwa kutoa kiasi cha Tsh. Bilioni mbili kwa kuanzia huku akitaka nguvu na sapoti kutoka kwa wengine.
Kila la heri klabu ya Simba katika utekelezaji wa mipango hiyo bora na yenye afya kwa soka la Tanzania, kwa kuwa ikipata Simba basi Tanzania imepata.