Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Saka apitishwa kwenye kilinge cha Messi, CR7

Bukayo Saka Too Bukayo Saka

Sun, 17 Dec 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Bukayo Saka kwa sasa ameshafikisha mechi 200 alizocheza akiwa na uzi wa Arsenal kwenye mwili wake na mambo yake si haba kwenye kikosi hicho cha Emirates.

Namba hazidanganyi kwa kile ambacho amekifanya ndani ya uwanja. Kwenye soka la kizazi hiki cha sasa, kipimo cha ubora wa takwimu za ndani ya uwanja ni watu wawili tu, asipokuwa Lionel Messi basi ni supastaa Cristiano Ronaldo.

Kwa kuzingatia hilo, baada ya Saka kutimiza mechi 200 akiwa na kikosi cha Arsenal takwimu zake zimelinganishwa na kile ambacho Messi na Ronaldo walifanya wakati walipocheza mechi zao 200 za kwanza.

Messi na Ronaldo wamechora mstari kwenye viwango bora vya mchezo wa soka kwa miaka ya karibuni baada ya kucheza kwa ubora mkubwa na kutawala mchezo huo kwa miongo miwili. Wakati Saka akiwa ndiyo kwanza anaanza kuonyesha ubora wake, rekodi zake huko Arsenal kwenye mechi hizo 200 alizocheza, hakika zinavutia.

Kocha, Unai Emery, anayeinoa Aston Villa kwa sasa, ndiye aliyempa nafasi Saka ya kutumikia kikosi cha wakubwa wakati alipokuwa akiifundisha Arsenal mwaka 2018.

Tangu wakati huo, Saka amekuwa akiboresha kiwango chake siku hadi siku na sasa panga pangua amekuwa tumaini kubwa kwenye kikosi hicho kinachonolewa na Mhispaniola mwingine, Mikel Arteta.

Saka, ambaye ni staa wa kimataifa wa England, mwanzoni mwa maisha yake ya soka kwenye kikosi cha Arsenal alitumika kama beki wa kushoto, kabla ya kuonyesha makali ya kutosha akiwa winga wa kulia chini ya Kocha Arteta.

Saka, 22, alitoa mchango muhimu wakati Arsenal ilipokuwa ikichuana kuwania ubingwa wa Ligi Kuu England msimu uliopita na ameendeleza moto wake msimu huu.

“Kwa kipindi hiki hana kikwazo, anataka zaidi na zaidi na watu wanahitaji zaidi pia kutoka kwake,” alisema Arteta alipomzungumzia staa wake huyo.

“Wachezaji wenzake wanafahamu ni kitu gani anahitaji ili acheze vizuri. Ana makocha na wafanyakazi wengine ambao watamfanya kuwa bora. Nadhani ni mahali pazuri kwake yeye kuzidi kukuza kiwango chake cha soka.”

Saka, mechi yake ya 200 kwenye kikosi cha Arsenal ni ile ya katikati ya wiki iliyopita, alipocheza dhidi ya Luton Town na winga huyo machachari alionyesha makali makubwa katika mchezo huo.

Katika mechi nane zilizopita alizochezea Arsenal, Saka amechangia mabao tisa na hakika amekuwa kwenye kiwango bora sana kwa siku za karibuni.

Alipoulizwa kuhusu Saka kufikisha mechi 200 na kile alichofanya, Arteta alisema: “Takwimu si mbaya kwa umri wake! Ameonyesha mwendelezo mzuri wa kiwango chake na zote tumeona uwezo wake na kila anachoweza kukifanya.

“Atakua na kupevuka, lakini kwa wakati huo huo ana nafasi ya kuwa bora zaidi. Makocha wake wote waliomfundisha kwenye akademia wamemmwagia sifa. Ni mchezaji spesho.”

Mwanaspoti linajaribu kuangazia rekodi za Saka kwa kile alichofanya katika mechi 200 alizochezea Arsenal na kulinganisha wakali wawili, Messi na Ronaldo walipocheza mechi zao 200 za mwanzo. Takwimu hizi ni kwa mechi za klabu tu.

Chanzo: Mwanaspoti