Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Sajili zilizotikisa na wametemwa

Moloko X Konkoni Moloko na Konkoni

Wed, 17 Jan 2024 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Simba na Yanga kuna sajili zilizotikisa wakati wanatua, lakini ulipofika wakati wa kuondoka walipoa na wakaonekana wa kawaida sana.

Mastaa hao baada ya kujiunga na klabu hizo walionyesha uwezo wao kwa nyakati tofauti, pia walipitia nyakati za viwango vyao kushuka, jambo lililowafanya wakatwe ndani ya klabu zao bila maswali mengi.

Yanga chini ya kocha Miguel Gamondi kuna wachezaji hawana nafasi ndani ya kikosi chake, mmoja wapo ni Jesus Moloko ambaye wakati wa Nasreddine  Nabi nyota yake ilingara.

Vivyo hivyo kwa Simba,  Abdelhak Benchikha kuna nyota chini yake wanaonekana wa kawaida mfano Jean Baleke, tofauti na kipindi alichoingia cha kocha Roberto Oliveira 'Robertinho', alichokuwa hatari kwa kucheka na nyavu.

Mwanachi linakuchambulia mastaa ambao tayari wamekatwa ndani ya klabu hizo, sababu ikitajwa ni viwango vyao kuwa chini, hivyo makocha kushindwa kuendelea nao, lakini wanatua walikuja kwa mkwara mzito.

MOSES PHIRI-SIMBA

Msimu uliopita straika, Moses Phiri alimaliza na mabao 10 na mwishoni akapata majeraha yaliyopunguza kasi yake, usajili wake wa kutua ndani ya klabu hiyo akitokea Zanaco, ulitikisa kwani Yanga ilihusishwa kuhitaji huduma yake.

Msimu huu kacheza mechi tisa na dakika 287 za Ligi Kuu dhidi ya Mtibwa Sugar (dakika 23), Dodoma Jiji (38),Prisons (7), Singida Fountain Gate (dakika 44), Ihefu (dakika 44), Yanga (22), Namungo (45) Kagera Sugar (64), amefunga mabao matatu, kiwango chake kushuka inatajwa ndio sababu ya kuachwa, anahusishwa kwenda  Power Dynamos ya nchini kwao Zambia.

JESUS MOLOKO-YANGA

Msimu huu hadi anaachana na Yanga hakuwa na bao isipokuwa asisti mbili, kacheza dakika 334 na mechi sita za Ligi Kuu, usajili wake ulikuwa mkubwa, ingawa msimu wake wa kwanza hakuanza vizuri, isipokuwa ulioisha alikuwa kwenye kiwango cha juu.

Kacheza dhidi ya KMC (dakika 79), Namungo (23), Ihefu (68), Coastal Union (21), Mtibwa (79),Tabora United (64),alitoa asisti mbili dhidi ya KMC moja na Coastal Union moja na kuondoa kwake amempisha Augustine Okrah.

JEAN BALEKE-SIMBA

Straika Jean Baleke, wakati anajiunga na Simba kupitia dirisha dogo, akitokea Nejmeh SC ya Lebanon, mechi yake ya kwanza ilikuwa dhidi ya Dodoma Jiji, Januari 22,2023 ndiye aliyefunga bao moja iliyoipa timu hiyo pointi tatu.

Japokuwa Simba haijatoa taarifa rasmi za kukatwa kwake, imeelezwa alipaswa kurudishwa kwa mkopo TP Mazembe ila yeye hataki na msimu huu, kafunga mabao saba, ila kuondoka kwake kumestua watu wengi, kwani ndiye kinara wa mabao ndani ya Simba.

HAFIZ KONKONI -YANGA

Je ungekuwa Gamondi ungefanyaje? kwenye maamuzi ya straika Hafiz Konkoni ambaye alimpa nafasi ya kucheza, ila kafunga bao moja, staa ambaye wakati anasajiliwa alitegemewa azibe pengo la Fiston Mayele aliyetoka nchini akiwa mfungaji bora wa ligi, ila mambo yakaenda sivyo ndivyo.

Konkoni amecheza jumla ya dakika 189 dhidi ya KMC (dakika 26), JKT Tanzania (59), Geita Gold (31), Azam (dakika moja) na Singida Fountain Gate (dakika 72), amefunga bao moja na asisti moja dhidi ya KMC.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live