Zimebaki siku 22 kufungwa kwa dirisha kubwa la usajili huku kila klabu ikiendelea kupambana kivyake kusajili kikosi ambacho inaamini kitakuja kulinda heshima msimu ujao ambao tunasubiri ratiba tu ya ligi hiyo.
Kwenye dirisha hili kumekuwa na taarifa nyingi za wachezaji na hata makocha kuhusishwa na klabu nyingine lakini wapo wale ambao taarifa zao zimesemwa sana kwamba wanakwenda kule kisha baadaye mambo yakageuka
MAKABI LILEPO
Mara baada ya ligi kumalizika taraifa za usajili kwa winga wa Al Hilal ya Sudan, Makabi Lilepo zilianza kuvuma zikianzia pale Yanga na alipohusishwa kuja kwa mabingwa hao kuchukua nafasi ya Fiston Mayele ambaye mapema ilionekana hakuna uwezekano wa kubaki ndani ya klabu hiyo.
Mbali na Yanga pia Azam nayo ilionekana kuipigia hesabu huduma ya Lilepo lakini mpaka mwisho licha ya Mayele kuondoka Yanga ilishindwa kumleta na mrithi wa Mayele amekuja mchezaji mwingine huku Azam ikimchukua mshambuliaji mwingine na Lilepo akabaki Al Hilal.
BRUNO GOMES
Kiungo wa Singida Fountain Gate raia wa Brazil ambaye baada ya ligi kumalizika tu maneno yakaanza kwamba anahitajika kwa klabu za Yanga na hata Simba.
Uvumi ulienea zaidi mara baada ya kuwa mmoja wa viungo bora katika kikosi cha msimu lakini mpaka Simba na Yanga zinafunga usajili wao, Singida ilifanikiwa kumbakisha ingawa bado hajarejea nchini kutoka mapumzikoni.
YAHAYA MBEGU
Badaa ya kufanya kazi bora msimu uliopita aliyekuwa beki wa kushoto wa Ihefu, Yahya Mbegu naye alizichanganya klabu mbalimbali, akianzia Simba ambako ilimpigia hesabu.
Taarifa za Simba zikagongana na kuhitajika pia Singida FG na na baadaye zikarejea tena kwamba ameshamalizana na Simba lakini mwisho wa siku Singida ndio iliyofanikiwa kumnasa na tayari ameshatambulisha.
LAMINE DJAJOU
Winga Msenegal, Lamine Djajou naye alikuwa mmoja kati ya wachezaji walioshtua mapema tu mara baada ya ligi ya msimu uliopita kumalizika lakini hata hivyo hakuweza kusajiliwa mpaka Azam ilipokuwa ikifunga usajili kwa wachezaji wa kigeni.
MAHOP
Jina lingine lilitajwa sana kuja kuchukua nafasi ya Mayele ni mshambuliaji Mcameroon, Emmanuel Mahop, ilifika wakati ilionekana wazi atachukua nafasi ya Mkongomani huyo lakini haikuwa hivyo. Licha ya kuja mpaka chini lakini bado dili hilo likakwama na Yanga kuamua kumchukua mshambuliaji raia wa Ghana, Afiz Konkoni ambaye ndiye aliyekuja kuchukua nafasi ya Mayele.
MOHAMED ZOUNGGRANA
Kiungo wa zamani wa Asec Mimosas ambaye alitajwa sana katika dirisha hili la usajili, mashabiki wa Yanga walitarajia angetua klabuni kwao lakini Simba nayo ilikuwa inajua anatua Msimbazi lakini haikuwa hivyo. Baada ya vuta nikuvute kubwa baadaye Zoungrana alitua Algeria na kusaini mkataba wa miaka mitatu na MC Alger iliyomaliza dili hilo fasta na kuziaacha Simba na Yanga zikiishia kwenye tetesi.
CLATOUS CHAMA
Ndani ya dirisha hili liliibuka kasheshe la hatma ya kiungo wa Simba, Clatous Chama, kiungo huyo aliibua sintofahamu kufuatia kukacha safari ya kwenda kwenye maandalizi ya msimu mpya na kikosi cha Simba wakati kikielekea Uturuki.
Lilipoibuka kasheshe hilo ghafla taarifa zikaanza Yanga inavizia saini yake hatua ambayo iliwashtua mashabiki wa Simba wakiwa hawajui kipi kinaendelea hata hivyo, Simba ilifanikiwa kushinda tena vita kwa kumbakiza na kumsafirisha kwenda kambini kuungana na wenzake.
BERNARD MORRISON
Baada ya kutemwa na Yanga kwa klabu hiyo kugoma kumuongezea mkataba ziliibuka taarifa kwamba anatimkia Singida FG na hatua ya kurejea kwake nchini akitokea kwao Ghana zilikoleza uvumi huo. Haikuishia hapo ikatajwa pia Azam inaweza kumchukua Morrison lakini hakutua klabu zote hizo na hata Singida FG juzi haikumtambulisha mtukutu huyo na sasa anatajwa kuelekea Morocco kujiunga na moja ya klabu za huko.
SOSPETER BAJANA
Alitajwa kutua Simba kiasi kwamba kila kitu kilikuwa tayari. Aliaminika ndiye angeenda kurithi nafasi na jezi ya Jonas Mkude lakini mambo yalibadilika ghafla na kuamua kubaki Azam FC. Hadi leo hakijulikani nini kilitokea.