Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Sajili hizi hapa Ligi Kuu Wanawake zimetiki

Wanawake Sajili Sajili hizi hapa Ligi Kuu Wanawake zimetiki

Wed, 17 Jan 2024 Chanzo: Mwanaspoti

Huku kwenye Ligi ya Wanawake WPL) kuna timu zimeokota dodo kwa usajili kuwaendea vizuri. Baadhi ya timu zimesajili wachezaji na kuingia moja kwa moja kwenye vikosi vyao ikionesha matunda ya pesa zilizotoka kwenye dirisha hili dogo.

Ukiachana na Simba, Yanga na JKT kuna timu nyingine kama Alliance nazo zimefanya usajili wa wachezaji bora ambao mpaka sasa wameonesha viwango vyao.

Mwanaspoti limekuchambulia timu zinazoshiriki WPL ambazo mpaka sasa usajili waliofanya umewalipa.

JKT QUEENS

Mabingwa watetezi wa Ligi Kuu Bara, JKT ndio timu inayoongoza kuwa na makocha wote wazawa pamoja na wachezaji wake.

Ukiachana na ubora waliounyesha kwenye ligi msimu uliopita umewafanya waongeze baadhi ya wachezaji kwenye madirisha mawili makubwa na hili dogo.

Mpaka sasa imesajili wachezaji sita watatu kutoka Fountain akiwemo, Winifrida Gerald, Joyce Lema na Christer Bahera huku Amina Ally akitokea Yanga Princess.

Usajili wao umeonekana kuwalipa kwani wachezaji hao wamekuwa na mchango kwenye kikosi hicho na kuleta ushindani wa hali ya juu.

Mfano winga, Winifrida tangu amecheza mechi tatu za ligi amefunga mabao sita na Amina aliyefunga matatu kwenye mechi mbili. Mastaa hao wameongeza ushindani kwa Stumai Abdallah na Donisia Minja ambao msimu uliopita walikuwa wakiwania kiatu cha ufungaji bora.

Usajili wa beki Christer na kiungo Joyce umeenda kuongeza kitu kwenye safu ya ulinzi kwani mpaka raundi ya tatu timu hiyo haijaruhusu bao.

SIMBA QUEENS

Simba imesajili wachezaji watano wa kigeni na mpaka sasa ni wawili ambao wameonyesha kiwango bora na wameisaidia timu hiyo.

Msimu uliopita Simba iliwapa mkono wa kwaheri wachezaji wawili, Jentrix Shikangwa aliyetimkia China na Topister Situma na dirisha hili wameongeza watano.

Winga Elizabeth Wambui na Riticia Nabbosa ndio ambao mpaka sasa wameonesha ushindani kwenye nafasi zao na ni usajili ambao Simba imelamba jike.

Wengine kama Isabelle Diakisse ambaye anamudu kucheza nafasi ya ushambuliaji bado hajaonyesha kiwango chake kutokana na Asha Djafa na Mnuka ambao wanacheza nafasi hiyo kumudu vyema wakimpa wakati mgumu wa kupata namba na tayari amecheza dakika 15 dhidi ya Yanga.

Usajili wa wachezaji hao wawili umeonekana kutiki kutokana na kiwango bora walichoonesha tangu wametua Msimbazi.

YANGA PRINCESS

Imekuwa kawaida kwa Yanga karibu kila msimu kuwatema wachezaji wengi na kuwaongeza baadhi ambao nao wamekuwa wakifanya vibaya.

Msimu uliopita iliwapa mkono wa kwaheri wachezaji 12 na imeongeza 11 wanne wazawa na sita kutoka mataifa mengine.

Wachezaji hao ni Adejoke Ejalonibu (Raja Casablanca), Madina Traore (Etincelle Burkina Faso), Faiza Seidu (Ghana), Airin Madalina na Janet Moraa (Kenya), Rechenelle Kiteko (TP Mazembe) na Kaeda Wilson (7 Elite-Marekani) huku wazawa ni Lucy Pajero, Neema Paul, Lidya Maximillan na Rehema Yahya.

Ukiangalia kwenye kundi la wachezaji hao walioletwa wazawa wawili ni Lucy na Neema ambaye anamudu kucheza nafasi ya winga ndiye ameonesha angalau kucheza akifunga mabao mawili kwenye mechi tatu.

Wageni Janet mwenye mabao mawili kwenye mechi tatu na Airin mwenye bao moja kwa msimu huu ndio unaweza kusema wachezaji ambao Yanga imesajili lakini wengine tuendelee kuwapa muda wanaweza kubadilika baadaye kutokana na ugeni wa ligi.

Ili Yanga ifikie malengo ya kuchukua ubingwa kama Simba na JKT inatakiwa kuwekeza zaidi kwa upande huo ili kuleta matunda kama wanayopata wenzao.

FOUNTAIN GATE PRINCESS

Miongoni mwa timu ambazo zimekuwa zikizalisha vipaji vingi vinavyozinufaisha timu za Simba, Yanga na JKT.

Msimu huu timu hiyo imeachana na wachezaji wengi muhimu akiwemo Winifrida anayefanya vizuri JKT mapa sasa na Riticia ambaye ni kiungo bora kwenye Ligi ya WPL.

Mpaka sasa timu hiyo imesajili mchezaji mmoja kwa mkopo akitokea Simba Queens, Jackline Albert ambaye bado hajacheza mechi yoyote lakini kama atapata nafasi ni kiungo mshambuliaji mzuri.

Hata hivyo, Fountain wachezaji wake walewale wa zamani bado wanaipambania timu hiyo akiwemo nahodha, Aquila Gasper na Hasnath Ubamba wamekuwa na mwendelezo wa viwango vyao.

Kuondoka kwa wachezaji muhimu katika kikosi hicho kumekuwa na mapengo kwani hata kwenye ligi Fountain imeshindwa kufurukuta mbele ya Yanga nyumbani kwake ikikubali kichapo cha bao 1-0.

AMANI QUEENS

Kwa sasa inaweza kuitwa Mashujaa Queens baada ya mwenye timu hiyo kuiuza kwa Jeshi la kujenga Taifa (JWTZ).

Kwa misimu miwili mfululizo Amani imekumbwa na tatizo la ukata wa fedha uliowasababishia kutofanya vizuri kwenye ligi msimu uliopita ikimaliza nafasi ya nane kati ya kumi.

Msimu huu mpaka sasa imecheza mechi tatu ikiruhusu mabao 17, 6-1 dhidi ya Yanga, 10-0 dhidi ya JKT na kufunga manne ikichukua pointi tatu mbele ya Alliance Girls kwa kuifunga mabao 4-1.

Baada ya kuuzwa ikaanza vyema kwenye mechi ya kwanza ikiifunga Alliance ambayo iko nafasi ya tano kwenye msimamo wa ligi.

Achana na matokeo yao lakini nayo haijapoa kwani imesajili wachezaji 10 kutoka JKT ambao wana uzoefu mkubwa wa kuwasaidia kwenye ligi.

Katika usajili wa wachezaji hao 10, wawili ndio wameonekana wakicheza vizuri akiwewemo Zainabu Mohamed ambaye amekuwa akiisaidia timu ya taifa (U-18) na Asha Mrisho ambaye ana uzoefu na Ligi.

CEASIAA QUEENS

Kwa aina ya usajili ambao wanafanya baadhi ya timu za Ligi Kuu inaonyesha ni namna gani WPL inazidi kukua.

Ceasiaa ni miongoni mwa timu ambazo mbali na kusajili wazawa lakini imewaleta wageni tatatu kutoka Uganda.

Timu hiyo imesajili mshambuliaji kutoka Kampala Queens, Grace Aluka na winga Magret Kunihira ambao walibeba ubingwa wa ligi nchini humo na kiungo Naume Nagadya kutoka She Cooperate ambao walikuwa bora.

Usajili wa wachezaji hao utawanufaisha kwanza kuinusuru timu hiyo kupata matokeo mabaya kwa kuwa tayari wana uzoefu na ligi.

BUNDA QUEENS

Ukiachana na mwenendo mbaya walioanza kwenye ligi ni miongoni mwa timu zenye wachezaji wengi wadogo ambao bado hawana uzoefu mkubwa.

Hilo linaweza kusababishwa na ugeni wao kwenye ligi kwani ndio mara yao ya kwanza kucheza na ili kubakia Ligi Kuu itatakiwa kufanya kazi kubwa kutokana na ushindani uliopo.

TIMU HIYO IMESAJILI WACHEZAJI WATATU

Saumu Baya, Uweza Queens na Elizabeth Khisa kutoka Gaspo Women ya Kenya.

Elizabeth ndiye usajili ulioanza kuonesha matunda kwani kacheza mechi moja dhidi ya Ceasiaa na kufunga bao moja.

ALLIANCE GIRLS

Tofauti na misimu miwili nyuma Alliance ilikuwa tishio WPL lakini msimu huu imepungua makali.

Alliance na Fountain ni miongoni mwa timu zinazoongoza kwa kuzalisha vipaji vingi lakini msimu huu tayari imedondosha pointi tatu dhidi ya Amani Queens.

Timu hiyo inahusishwa kupata saini ya kiungo Salome Sati kutoka Kangemi Ladies inayoshiriki Ligi Kuu nchini Kenya na kama watafanikiwa ataenda kuisaidia timu hiyo.

Kama atapata nafasi na kuonesha kiwango chake unaweza kuwa usajili bora kwa timu hiyo na anaweza kuingia fedha kwa kuuzwa na timu kubwa.

Chanzo: Mwanaspoti