Moto wa Ligi Kuu Bara bado haujakolea vizuri kutokana na ratiba ilivyo na mwingiliano wa mashindano mbalimbali, lakini hilo halijaondoa taswira kwa makocha wa timu za ligi hiyo namna wanavyotengeneza vikosi vyao.
Katika kuhakikisha wanamaliza ligi vizuri, ni lazima wafanye usajili utakaowaweka katika ushindani na hilo linaweza kufanyika kwenye dirisha dogo litakalofunguliwa Desemba mwaka huu.
Makala haya yanakuletea mastaa ambao wanaweza kusajiliwa katika hilo na kuzisaidia baadhi ya timu ambazo baadhi ya maeneo hayako vizuri.
ANDREW SIMCHIMBA
Ni moja ya washambuliaji wazuri kwa nyakati tofauti na msimu uliopita akiwa na Ihefu alifunga mabao saba katika Kombe la Shirikisho la Azam (ASFC).
Utupiaji wake wa mabao uliwafanya mabosi wa KMC wamsajili msimu huu lakini amekumbana na changamoto kutokana na uwepo wa washambuliaji kama Wazir Junior ambaye ameifungia timu hiyo mabao mawili na Sadala Lipangile ambaye ni nahodha wa timu hiyo.
Kwa timu ambazo hazina washambuliaji wazuri zaidi zinaweza kumchukua mchezaji huyu hata kwa mkopo kwa sababu kwenye kikosi cha KMC hapati nafasi hata ya kukaa benchi hivyo ni rahisi kwake kushawishika kuondoka.
PAUL GODFREY ‘BOXER’
Beki huyu ametoka kwa mkopo kwenda Ihefu akitokea Singida Big Stars lakini bado hajaweza kufua dafu mbele ya Kenneth Kunambi.
Katika mechi tano zote za kwanza, Boxer hajapata nafasi na huenda inachangiwa na kuchelewa kwake kujiunga na wenzake wakati wa maandalizi ya msimu mpya (Pre Season).
Boxer ni beki mzuri wa kulia na zipo timu ambazo zinahaha kwa sasa zikikosa mtu sahihi eneo hilo.
Ni ngumu kwa Boxer kuona akikubali kuendelea kusugua benchi huku ikiwa ametolewa kwa mkopo na Singida Big Stars ili apate nafasi ya kucheza.
ANDREW VICENT ‘DANTE’
Ilishtua kuona anakosekana hata kukaa benchi katika mechi tano mfululizo za KMC.
Ujio wa Juma Shemvuni na Twalib Mohammed umetengeneza kombinesheni mpya katika safu ya ulinzi ya KMC na matokeo yao ya mechi yamefanya benchi la ufundi liendelee kuwaamini. Wakati wachezaji hao wanacheza, Dante ni ngumu kuona anaendelea kukosekana hata benchi hivyo ni rahisi kwake kutoka dirisha dogo.
Dante katika misimu mitatu mfululizo akiwa KMC alikuwa mchezaji panga pangua kikosi cha kwanza.
RAMADHAN CHOMBO ‘REDONDO’
Kiungo huyu mkongwe kwa sasa hana timu yupo zake tu mtaani baada ya kumaliza mkataba na Polisi Tanzania.
Aliwahi kukaririwa akisema anasubiri dirisha dogo ili kurejea na amekosekana kwa sasa sababu kubwa ni kutofikia makubaliano na timu moja iliyokuwa ikihitaji huduma yake.
Redondo anaweza kurejea katika Ligi Kuu dirisha dogo na anafanya vizuri kwa sababu bado ana uwezo wa kufanya hivyo.
Ni miongoni mwa viungo wenye uwezo mkubwa na hajakubali kirahisi soka limtupe mkono hivyo ni wazi kabisa timu zinaweza kumpata katika dirisha hilo.
JABIR AZIZ ‘STIMA’
Kama ilivyo kwa Redondo ndivyo ilivyo kwa Stima kwani kwa sasa ameamua kufanya mazoezi yake binafsi huku akiendelea na biashara zake.
Kiungo huyu aliamua kupumzika mwenyewe kucheza msimu huu hadi dirisha dogo na sasa ni wakati ambao anaweza kabisa kushawishika mapema na kurejea uwanjani.
Ni miongoni mwa viungo wenye uwezo mzuri wa umiliki mpira na kupiga pasi za mwisho eneo la ushambuliaji.
Hana gharama kwa sababu hajafungwa na mkataba wowote ule ambao utamfanya ashindwe kujiunga kwa wakati na timu itakayohitaji huduma yake.
NASSOR KAPAMA
Huyu ni kiraka ndani ya kikosi cha Simba lakini amekuwa na ingia toka na kukosa uhakika wa kucheza kikosi cha kwanza.
Ni miongoni mwa wachezaji wanaoweza kumudu eneo la kiungo mkabaji, mshambuliaji na hata beki wa kati.
Simba ni timu kubwa na yenye ushindani wa kutosha hivyo kwake inaweza kuwa changamoto kucheza lakini sio sehemu nyingine.
Huu ni msimu wake wa pili na wa mwisho, ipo wazi atahitaji kutoka ili akapate muda wa kucheza na kulinda soko lake.
CRISPIN NGUSHI NA DENIS NKANE
Mastaa hawa bado ni sehemu ya wachezaji wa Yanga lakini muda wao wa kucheza ni mdogo.
Ngushi katika dirisha la usajili lililopita alikuwa anahitajika na baadhi ya timu lakini aliamini bado ana nafasi ya kucheza ndani ya Yanga ila mambo bado ni magumu upande wake.
Upande wa Nkane na eneo lake ndani ya uwanja ni wazi ni ligumu, ni muda sahihi kwao katika dirisha dogo kuomba kutoka kwa mkopo ili wapate muda wa kucheza.
Mastaa wengi wakitoka katika timu hizi kubwa ni rahisi kupata zingine zinazohitaji huduma zao.