Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Sajili 10 za mastraika garasa Ligi Kuu Bara

Garasaaa Pic Data Sajili 10 za mastraika garasa Ligi Kuu Bara

Fri, 26 Mar 2021 Chanzo: www.mwanaspoti.co.tz

ACHANA na usajili mbovu wa wachezaji wa nafasi za nyuma kama kipa wa Yanga, Clouds Kindoki ambazo zilikuwa za hasara kutokana na viwango walivyoonyesha kwenye mechi mbalimbali za mashindano ikiwemo Ligi Kuu Bara.

Kwa miaka miwili timu kubwa nchini Simba, Yanga na Azam FC zimeingia katika orodha ya kusajili wachezaji wasiokuwa na viwango vya kuzichezea, licha ya viongozi kuwa na matumaini makubwa kwao.

Mwanaspoti linakuletea washambuliaji 10 waliosajiliwa na timu hizo ambao ni kama hasara kwa klabu kutokana na viwango vya chini walivyovionyesha.

JUNIOR LOKOSA - SIMBA

Simba ilimsajili Lokosa kwa mkataba wa miezi sita akiwa kama mchezaji huru baada ya mkataba wake na Esperance de Tunis kuvunjwa.

Usajili wa Lokosa ulifanyika wakati wa dirisha dogo la usajili ili kuongeza nguvu kikosini, hasa ikilenga michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika mara baada ya kuingia hatua ya makundi.

Tangu asajiliwe Lokosa hajacheza mechi hata moja licha ya timu hiyo kucheza michezo sita ya hatua ya makundi.

Sababu kubwa inayomfanya Lokosa kutocheza ni kutokuwa fiti kimwili pamoja na ubora ambao wanaonyesha mastraika wenzake.

Halitakuwa jambo la kushangaza mwisho wa msimu Lokosa kuingia kwenye orodha ya wachezaji watakaoonyeshwa mlango wa kutokea.

YIKPE GISLAIN - YANGA

Kabla ya kuanza msimu uliopita Yanga walimsajili Yikpe kwa mkataba wa miaka miwili akitokea Gor Mahia ya Kenya, lakini hakudumu na timu hiyo kutokana na kiwango chake kibovu.

Yikpe akiwa na Yanga ndani ya msimu mmoja alifunga mabao matatu na mawili kati ya hayo alifunga dhidi ya Singida United ambayo ilishuka daraja na aliifunga nyumbani na ugenini.

Licha ya Yanga kutengeneza nafasi nyingi za kufunga katika mechi ambazo Yikpe alikuwa uwanjani, lakini hakuonyesha makali ya kutupia mabao kama ambavyo alitakiwa.

Kutokana na kiwango hicho ambacho hakikuwaridhisha mabosi wake waliamua kuvunja mkataba kabla msimu huu.

MPIANA MONZINZI - AZAM FC

Msimu mmoja nyuma Simba na Yanga kuwa kwenye mbio za kuwania huduma ya straika huyo wa zamani wa FC Lupopo ya DR Congo kushindwa kumpata, Azam FC walifanikiwa kumnasa.

Azam walimpata Monzinzi katika dirisha dogo ili kuwa tiba ya ufungaji mabao, lakini mambo yamekuwa tofauti kwake mpaka sasa.

Monzinzi ameifungia Azam bao moja tangu kusajiliwa kwake - tena alifunga bao hilo kwenye Kombe la Mapinduzi katika mechi dhidi ya Mlandege FC. Tangu afunge bao hilo Januari 10, mwaka huu, hajafunga tena hadi sasa.

DITRAM NCHIMBI - YANGA

Yanga walimsajili Nchimbi katika dirisha dogo misimu miwili nyuma na Desemba 28, 2019 walimtangaza kama mchezaji wao akitokea Polisi Tanzania.

Nchimbi akiwa na Polisi Tanzania kabla ya kunaswa na Yanga katika mzunguko wa kwanza alicheza mechi 11 na kufunga mabao manne ikiwemo (hat-trick) aliyofunga dhidi ya Yanga ambao walimsajili.

Mbaya zaidi, Nchimbi ametimiza mwaka mmoja na siku kadhaa bila kufunga bao lolote katika mechi za Ligi Kuu Bara.

AKONO AKONO - AZAM FC

Mwanzo wa msimu uliopita Azam ilikamilisha usajili dakika za mwisho kwa kumsajili mshambuliaji wa kimataifa wa Cameroon, Alain Thierry Akono Akono akijiunga na timu hiyo kama mchezaji huru kufuatia kumaliza mkataba wake Fortuna Du Mfou.

Akono alisaini mkataba wa miaka miwili wa kuitumikia timu hiyo na alikuwa tegemeo katika timu ya Taifa ya Cameroon kwa wachezaji wa ndani (Chan). Alikuja Azam FC kuongeza nguvu eneo hilo.

Tangu kusajiliwa kwake Azam FC hakuwa anapata nafasi ya kucheza mara kwa mara. Hakuweza kufunga bao lolote katika mechi za mashindano na matajiri hao waliamua kumuuza klabu ya Negeri Sembilan ya Malaysia.

PATRICK SIBOMANA - YANGA

Mei 29, 2019, Yanga iliyokuwa ikinolewa na kocha Mwinyi Zahera, raia wa DR Congo ilitangaza kumsainisha winga msumbufu, Simbomana kutoka APR ya Rwanda kwa mkataba wa miaka miwili.

Sibomana licha ya kuwa alikuwa akipata nafasi ya kucheza mara kwa mara na kutengeneza nafasi za mabao muda mwingine alifunga mwenyewe. Baada ya msimu wa Ligi Kuu Bara 2019/20 aliachwa.

SADNEY URIKHOB -YANGA

Kabla ya msimu uliopita kuanza, Yanga ilitangaza kuboresha safu ya ushambuliaji kwa kumnasa straika raia wa Namibia, Urikhob.

Mchezaji huyo ambaye aliwahi kuja nchini kufanya majaribio katika timu ya Simba kabla ya Yanga kumnasa hakuwa na maisha mazuri katika kikosi hicho kwa kuonyesha kiwango bora.

Alicheza mechi chache akiwa Yanga na mara baada ya msimu kumalizika akiwa na mkataba wa miwili aliunganishwa katika orodha ya wachezaji 14 walioachwa na klabu hiyo.

ERICK KABAMBA - YANGA

Yanga walimsajili winga huyo kutoka Zambia, lakini hakuwa na maisha mazuri ndani ya kikosi cha Yanga kwa kuonyesha kiwango bora na badala yake alikuwa mchezaji wa kawaida.

Kabamba alisajiliwa kwa mkataba wa miaka miwili, ingawa hakufunga bao lolote na alicheza mechi za ligi ambazo hazikufika 10 msimu mzima.

Baada ya msimu wa 2019/20 kumalizika, Yanga waliamua kuachana na Kabamba akiwa bado na mkataba wa mwaka mmoja.

JUMA BALINYA -

YANGA

Mwanzoni mwa msimu uliopita Yanga walitangaza kukamilisha usajili wa mshambuliaji wa Uganda, Balinya Juma kutoka Polisi FC ya nchini humo.

Mchezaji huyo aliyeibuka mfungaji bora wa Ligi Kuu Uganda msimu 2018/19 akifunga mabao 17, alitambulishwa na wababe hao wa soka nchini kuwa amemwaga wino wa kuwatumikia kwa mkataba wa miaka miwili.

Balinya alicheza baadhi ya mechi za mzunguko wa kwanza na ilipofika dirisha dogo la usajili uongozi wa timu hiyo ulitangaza kusitisha mkataba wake alioutumikia kwa muda mfupi.

ISSA BIGIRIMANA -YANGA

Mei 29, 2019 Yanga ilitangaza kumsainisha mkataba wa miaka miwili winga Bigirimana kutoka APR ya Rwanda ili kuongeza nguvu katika kikosi hicho kwenye safu ya ushambuliaji.

Bigirimana hakuwa anapata nafasi ya kucheza mara kwa mara. Hata hivyo, kiwango chake hakikuwaridhisha viongozi ambao waliamua kuvunja mkataba wake uliokuwa umebakiza mwaka mmoja.

Chanzo: www.mwanaspoti.co.tz