Mwaka mwingine, msimu mwingine wa bila ya taji kwa straika Harry Kane. Ndiyo hivyo.
Ndicho unachoweza kusema baada ya Tottenham Hotspur kutokuwa na uhakika wa kushinda taji la Ligi Kuu England msimu huu, huku ikiwa imetupwa nje kwenye makombe mengine yote, ikiwamo la Ligi ya Mabingwa Ulaya waliloaga Jumatano iliyopita mbele ya AC Milan katika hatua ya 16 bora.
Spurs ilisukumwa nje kwa tofauti ya bao moja tu, walilofungwa 1-0 kwenye mechi ya kwanza San Siro, kabla ya kutoka sare ya bila ya kufungana katika mechi ya marudiano iliyofanyika London, usiku wa Jumatano iliyopita.
Spurs pia ilitupwa nje mapema kwenye Kombe la Ligi na Kombe la FA, jambo linalofichua kwamba hilo linaweza kumsukuma straika Kane akaamua kuachana na timu hiyo ili kwenda kujiunga kwingine ambako atapata fursa ya kubeba mataji kabla hajastaafu.
Kutokana na hilo, ni mahali gani Kane anaweza kushawishika kwenda kujiunga mwishoni mwa msimu huu - ambako atapata fursa ya kucheza kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu ujao na uwezekano wa kunyakua mataji ili asistafu kinyonge.
MAN UNITED
Ni jambo la wazi, Manchester United kwa muda mrefu imekuwa ikihusishwa na mpango wa kunasa saini ya straika Harry Kane huku imani ya mabosi wa Old Trafford, wakiamini jambo hilo linakwenda kutumia kwenye dirisha lijalo la majira ya kiangazi. Mwaka jana, Kane alisakwa sana na Manchester City - lakini safari hii Man United ndiyo wanaonekana kuwa na nafasi kubwa ya kunasa saini yake kwa timu za Ligi Kuu England. Bei yake inaweza kufikia Pauni 100 milioni.
BAYERN MUNICH
Timu ya pili inayopewa nafasi kubwa ya kunasa saini ya Kane ni mabingwa wa Ujerumani, Bayern Munich, ambao kwa muda mrefu wamekuwa wakisaka mtu anayefaa kwenye kuziba pengo la Robert Lewandowski, aliyetimkia zake Barcelona mwaka jana.
Straika Eric Maxim Choupo-Moting anajaribu kuisaidia timu hiyo kwa sasa sambamba na Sadio Mane, lakini Bayern wanahitaji Namba 9 wa asili na kwenye hilo mpango wao ni kwenda kunasa saini ya Kane. Ni suala la kusubiri kuona kama Kane atatua Allianz Arena.
REAL MADRID
Miamba mingine mikubwa katika soka la Ulaya inayopiga hesabu za kwenda kunasa saini ya straika Kane ni Real Madrid, ambao suala la kubeba mataji na kucheza kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya kwao halijawahi kuwa tatizo.
Real Madrid wanatambua wazi straika wao namba moja kwa sasa, Karim Benzema atakuwa na umri wa miaka 36 msimu ujao, hivyo watahitaji mchezaji mwenye umri mdogo, licha ya Kane mwenyewe anakaribia kufikisha umri wa miaka 30.
NEWCASTLE UNITED
Baada ya kuwa chini ya umiliki mpya na mtu mwenye pesa za kutosha, Newcastle United ndoto zao za sasa ni kuwa moja ya timu za kutisha huko Ulaya.
Katika kutimiza mpango huo, Newcastle imekuwa ikitafuta namna ya kusajili wachezaji wenye viwango bora kabisa na kwenye hilo straika Harry Kane anaweza kuhusika akanaswa St James' Park akakipige kuanzia msimu ujao. Lakini, Newcastle itafanikiwa tu kumnasa Kane kama itanyakua tiketi ya kucheza Ligi ya Mabingwa Ulaya mwaka huu.
CHELSEA
Kitu ambacho bilionea Todd Boehly anakitaka, basi atafanya kila analoweza kukipata. Tajiri huyo mmiliki wa klabu ya Chelsea tayari ameshatumia karibu Pauni 600 milioni kwenye usajili peke yake tangu alipochukua klabu hiyo mwaka jana.
Alizipiku timu kibao kwenye usajili wa Enzo Fernandez na Mykhaylo Mudryk kwenye dirisha la Januari mwaka huu, hivyo bila ya shaka, anaweza kuzipiku klabu nyingine kwenye mbio za kunasa saini ya straika Kane. Ni suala la kusubiri na kuona.