Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Saido mtu sana, aingia anga za juu

SAIDOOO Saido mtu sana, aingia anga za juu

Fri, 9 Jun 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Juzi Jumanne nyota wa Simba Mrundi, Saidi Ntibanzokiza 'Saido' ameifungia timu yake mabao matano katika ushindi wa mabao 6-1 dhidi ya Polisi Tanzania kwenye mechi ya Ligi Kuu iliyopigwa uwanja wa Azam Complex na moja kwa moja kuingia anga za wakongwe Edibily Lunyamila na Nsa Job.

Kitendo hicho cha kufunga mabao matano kwenye mechi moja ya ligi, kimemfanya Saido kuweka rekodi ya kipekee na kuwa mchezaji wa tatu kufunga idadi hiyo ya mabao kwenye ligi baada ya watangulizi wake Lunyamila na Nsa waliofanya hivyo katika miaka ya nyuma.

Lunyamila ndiye mchezaji wa kwanza kufunga mabao matano kwenye mechi moja ya ligi akifanya hivyo mwaka 1998 wakati timu yake ya Yanga ikiichapa Kagera Stars (ssa Kagera Sugar) mabao 8-0, huku Nsa akifuatia mwaka 2009 akiiongoza Azam kuifunga Villa Squad mabao 6-2.

AMBIPU MAYELE

Mabao hayo ya Saido juzi yaliibua mjadala mpya wa nani ataibuka kinara wa mabao kwenye ligi msimu huu baada ya kufikisha mabao 15 akimfukuzia kwa karibu Mkongomani Fiston Mayele wa Yanga anayeongoza akiwa nayo 16 huku wote wakiwa wamebakiza mechi moja.

Kabla ya Saido kufunga mabao hayo, ni kama Mayele alikuwa amejihakikishia kubeba kiatu cha ufungaji bora kwa msimu huu kwani alikuwa anawaacha kwa mabao sita, Saido, Moses Phiri na Bruno Gomes waliokuwa nayo 10 yeye akiwa na 16.

Hivyo basi, mechi za mwisho zitakazopigwa kesho Ijumaa, ndizo zitaamua nani kuibuka mfungaji bora ambapo Simba ya Saido itakutana na Coastal Union katika uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam huku Yanga ya Mayele itakuwa Mbeya uwanja wa Sokoine ikimenyana na Tanzania Prisons.

Kama Saido atafunga mabao mawili kwenye mchezo huo atampiku Mayele kwani atafikisha 17 lakini pia kama Mayele atafunga bao moja au mawili atazidi kujitengenezea mazingira ya kutwaa kiatu lakini pia kama watalinganisha mabao basi watapewa wote kiatu. Kiufupi dakika 90 za mechi za mwisho ndizo zitaamua mbio hizo.

MSIMU MMOJA, TIMU MBILI

Wakati ikiwa ngumu kwa baadhi ya wachezaji kuhama timu na kufanya vizuri, Saido ameliweza hilo kwani kwa msimu huu amecheza timu mbili na kote ameuwasha moto. Nyota huyo aliyewahi kucheza Ligi Kuu ya Ufaransa, msimu huu aliuanza akiwa na Geita Gold na kufunga mabao manne na asisti sita, lakini katika dirisha dogo lililofungwa Januari 15 mwaka huu alijiunga na Simba na hadi sasa amewafungia Wekundu wa Msimbazi hao mabao 11 na asisti sita kwenye ligi, ikiwa na maana kwenye mabao 72 ya Simba kahusika na mabao 17.

NAMBA ZINAONGEA

Saido msimu huu ndiye mchezaji anayeongoza kwa kuhusika na mabao mengi kwenye ligi 27 akiwa amefunga 15 na kuasisti 12, akifuatiwa na Mayele aliyehusika kwenye 19 akifunga 13 na kuasisti tatu sambamba na Clatous Chama aliyehusika kwenye 18 baada ya kufunga manne na kuasisti mara 14.

Ukiachana na hilo, Saido anaungana na nahodha wake wa Simba, John Bocco kuwa wachezaji pekee waliofunga mabao matatu kwenye mechi moja 'Hat trick' mara mbili kwenye Ligi Kuu.

Saido alifanya hivyo dhidi ya Tanzania Prisons Desemba 30 mwaka jana katika ushindi wa 7-1, ambapo na Bocco alifunga Hattrick, ikiwa ni ya pili kwa Bocco baada ya ile ya Novemba 19 mwaka jana dhidi ya Ruvu Shooting. Hadi sasa kwenye ligi zimefungwa jumla ya Hat trick nane, kutoka kwa wachezaji sita.

Ukiachana na Saido na Bocco wenye mbili mbili, wengine wenye Hat trick kwenye ligi ni Jean Baleke wa Simba aliyefunga dhidi ya Mtibwa Sugar, Ibrahim Mkoko wa Namungo aliyeipata mbele ya KMC, Mayele dhidi ya Singida Big Stars na Stephane Aziz Kii wa Yanga aliyefunga dhidi ya kagera Sugar.

Saido mwenye umri wa miaka 36 msimu huu hadi sasa amecheza mechi 22 za ligi akiwa na Geita na Simba na kabla ya hapo aliwahi kuichezea Yanga alikoachwa baada ya mkataba wake kumalizika.

Timu nyingine Saido alizowahi kucheza ni Vital' O ya Burundi, Kaysar Kyzylorda ya Kazakhstan, Akhsar Belediyespor ya uturuki, Caen ya Ufaransa, Nec Nijmegen ya Uholanzi na Cracovia ya Krakow pia kwa nyakati tofauti amekuwa akiitwa timu ya taifa ya Burundi na kuwa nahodha.

Akizungumzia kasi yake ya upachikaji mabao, Saido alisema ni moja ya kazi yake kwani akiwa uwanjani anapambana kuhakikisha timu inapata matokeo inayoyataka.

"Nashukuru kwa kufunga mabao matano lakini kikubwa ninachozingatia ni timu kwanza kupata matokeo kisha mambo binafsi yanafuata. Nikifanikiwa kuwa mfungaji bora nitafurahi lakini cha kwanza ni kuhakikisha timu inashinda mechi," alisema Saido.

27 Idadi ya mabao aliyohusika nayo Saido katika Ligi Kuu msimu huu akifunga 15 na kuasisti 12.

14 Miaka iliyopita tangu Job alipofunga mabao matano katika mechi moja ya ligi kabla Saido kuifikia.

72 Jumla ya mabao iliyofungwa na Simba katika mechi 29 msimu huu, huku Saido akihusika na 17.

1998 Mwaka ambao Lunyamila aliweka rekodi kwa kufunga mabao matano katika mechi moja ya ligi.

Chanzo: Mwanaspoti