Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Saido kaacha heshima, bado Yanga ilimuhitaji

Saidi Ntiba Aiyekuwa mchezaji wa Yanga, Saidi Ntibazonkiza (Kushoto)

Sat, 4 Jun 2022 Chanzo: www.mwanaspoti.co.tz

Saidi Ntibanzokiza ‘Saido’ ameondoka Yanga baada ya mkataba wake kumalizika mwishoni mwa mwezi uliopita.

Kidogo ilishtua. Hata hivyo, ilibidi iwe hivyo kutokana na pande mbili, yaani wajiri wake, Yanga na yeye mwenyewe kufikia makubaliano baada ya kushindwana kwenye masuala ya mkataba mpya.

Raia huyu wa Burundi ameshaondoka, lakini nyuma yake ameacha mambo makubwa na pengine Wanayanga hawatakaa wayasahau.

Mbali na heshima kubwa aliyoiacha Yanga kwa kuisaidia kuwa bora msimu huu, pia Saido ameacha rekodi tamu na ni wazi mashabiki wa klabu hiyo wasingetamani aondoke kutokana na kiwango bora alichokionyesha msimu huu.

Baadi ya wadau wa soka wanaona Saido angestahili kuendelea kuwapo Yanga kwani angewasaidia kwenye michuano ya kimataifa ya Ligi ya Mabingwa Afrika na ni wazi msimu ujao itashiriki kama mabingwa kutokana na mwenendo wao kwenye Ligi Kuu msimu huu.

Mwanaspoti linakuchambulia baadhi ya mambo yaliyomfanya awe lulu Yanga tangu ajiunge na miamba hiyo ya soka nchini msimu wa 2020/21 hadi alipoachana nao tangu akiwa kambini jijini Mwanza kujiandaa na mchezo wao dhidi ya Simba wa nusu fainali ya Kombe la Azam Sport Federation Cup na kuichapa Wekundu wa Msimbazi bao 1-0 na kuwanyang’anya ubingwa.

MABAO 11, asisti 9 Ligi Kuu

Msimu wa 2020/21 alianza kufunga dhidi ya Singida United kwenye mechi ya kirafiki ikiwa ndio mchezo wake wa kwanza tangu asajiliwe Yanga wakishinda mabao 3-0.

Baada ya hapo aliendeleza moto na kumaliza msimu wa Ligi Kuu Bara akiwa na mabao manne na asisti nne.

Msimu huu ndio ulikuwa moto zaidi na kutengeneza rekodi tamu na kumfanya kuwa kipenzi cha mashabiki.

Amefunga mabao saba na asisti tano na alikuwa msaada mkubwa kwa swahiba wake, Fiston Mayele anayeongoza kwa ufungaji wa mabao Ligi Kuu akiwa nayo 14.

MATAJI MAWILI

Tangu atue Ynaga Saido amebeba mataji mawili ikiwa ni lile la Kombe la Mapinduzi walilolibeba baada ya kuifunga watani zao wa jadi Simba kwenye mchezo wa Fainali, pamoja na Ngao ya Jamii ikifanya hivyo pia baada ya kuifunga Simba kwa bao la Fiston Mayele.

TUZO MBILI

Mbali na tuzo za mataji mawili aliyobeba kwa maana ya medali ya Kombe la Mapinduzi na Ngao ya Jamii, Saido pia ana tuzo binafsi mbili.

Katika kuonyesha amekuja Tanzania na ubora wake, Saido alinyakua tuzo yake ya kwanza ya mchezaji bora wa Mwezi Desemba msimu uliopita wa 2020/21 huku msimu huu 2021/22 pia akifanya hivyo mwezi Februari.

UZOEFU WAMBEBA

Saido kabla ya kutua Yanga amepita kwenye timu za NEC ya Uholanzi, Cracovia ya Poland, Akhisar Belediyespor ya Uturuki, Caen na Caen B ya Ufaransa, Kaysar Kyzylorda ya Kazakhstan na Vital’O ya nchini kwao Burundi.

Ni kutokana na kupita kote huko Saido amekuwa moto na kuibeba Yanga hadi kufikia ilipo sasa ikiwa kileleni mwa msimamo wa Ligi Kuu na itacheza hatua ya fainali ya Kombe la FA dhidi ya Coastal Union ya Tanga ingawa mwenyewe hatakuwepo kwenye michezo ijayo ya ligi pamoja na wa fainali.

KIPENZI CHA MASHABIKI

Ni mmoja wa wachezaji walioteka hisia za mashabiki wao na walijaa uwanjani kumshuhudia akikiwasha.

Achana na Mayele anayeongoza kwa kupendwa, Saido amekuwa kipenzi cha mashabiki na kama asingeondoka msimu ujao angezidi kuteka hisia kutokana na ubora wake.

BADO ANA DENI YANGA

Jicho la ukocha la Kennedy Mwaisabula ‘Mzazi’ liliona bado Saido alihitajika Yanga, kutokana na majukumu ya Ligi ya Mabingwa Afrika iliyopo mbele yao.

“Yanga inakwenda kucheza michuano ya CAF, Saido ana uzoefu hivyo angeisaidia timu sana, lakini naamini viongozi ni watu makini watakuwa wamejua namna ya kuziba nafasi yake,” anasema Mwaisabula aliyewahi kuzinoa Yanga, Bandari Mtwara, SC Villa na nyinginezo.

Naye beki wa zamani wa Yanga na Simba, Bakar Malima ‘Jembe Ulaya’ anakiri Saido kuacha alama itakayowafunza wengine kujitoa kwa ajili ya timu.

“Mchango wake unaheshimika ndani ya Yanga ndio maana wachezaji wenzake waliandika mengi juu yake, ila soka ndivyo lilivyo, kesho upo hapa kesho kule,” anasema.

Chanzo: www.mwanaspoti.co.tz