Kiungo mshambuliaji wa Simba, Saidi Ntibazonkiza 'Saido' ametumia siku 150 kumpindua aliyekuwa nyota wa kikosi hicho, Jean Baleke katika ufungaji wa mabao ndani ya timu hiyo baada ya kufunga mawili katika ushindi wa 4-1, dhidi ya Geita Gold.
Katika mchezo huo wa Ligi Kuu Bara uliopigwa kwenye Uwanja wa Azam Complex Chamazi jana, Saido alifunga mawili dakika ya 45 kwa mkwaju wa penalti na 71 huku mabao mengine ya kikosi hicho yakifungwa na Ladaki Chasambi aliyefunga pia mawili.
Mabao hayo mawili ya Saido yamemfanya nyota huyo kwa sasa kufikisha tisa msimu huu katika Ligi Kuu Bara akiwa ni kinara ndani ya timu hiyo baada ya kuivuka rekodi iliyokuwa inashikiliwa na Jean Baleke aliyeondoka dirisha dogo Januari mwaka huu.
Baleke aliyejiunga na klabu ya Al-Ittihad ya Libya, hadi anaondoka alikuwa amefunga mabao manane ya Ligi Kuu Bara ambayo yalichukua muda mrefu kufikiwa na mastaa mbalimbali wa kikosi hicho hadi Saido alipoibuka jana na kuipiku rekodi hiyo.
Mara ya mwisho kwa Baleke kufunga ilikuwa sare ya timu hiyo ya kufungana mabao 2-2, dhidi ya KMC Desemba 23, mwaka jana kwenye Uwanja wa Azam Complex Chamazi na baada ya hapo imechukua siku 150 kwa Saido kumpiku raia huyo kutoka DR Congo.
Baleke kwa mara ya kwanza alijiunga na Simba katika dirisha dogo la Januari mwaka jana akitokea Nejmeh SC ya Lebanon aliyokuwa anaichezea kwa mkopo akitokea TP Mazembe ya kwao Congo ambapo hadi msimu unaisha alifunga pia mabao manane.
Msimu huu umekuwa mgumu zaidi kwa Saido ndani ya timu hiyo tofauti na ilivyokuwa msimu uliopita ambapo alikuwa mfungaji bora wa Ligi Kuu Bara akiwa na mabao 17 akifungamana na aliyekuwa nyota wa Yanga, Fiston Mayele aliyejiunga na Pyramids FC ya Misri.
Baada ya Saido kufunga mabao hayo mawili katika mchezo huo dhidi ya Geita Gold alionyesha ishara ya kuwaaga mashabiki wa timu hiyo kwa sababu mkataba wake na kikosi hicho alichojiunga nacho Januari, mwaka jana unafikia tamati msimu huu.
Hata hivyo, Katika mahojiano aliyofanya baada ya mchezo huo, Saido hakutaka kabisa kuzungumzia suala la kuondoka kwake kikosini humo.
Kwa mara ya kwanza Saido kutua nchini alijiunga na Yanga aliyoitumikia miaka miwili kuanzia 2020 hadi 2022 akitokea timu ya Vital'O FC ya kwao Burundi na baada ya hapo alijiunga na Geita Gold kisha kujiunga na Simba anapomaliza mkataba wake.