STAA wa Yanga, Mrundi Said Ntibazonkiza 'Saido' ameibua tafrani mitandaoni baada ya kufuta picha zake zote za Yanga kwenye ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa Instagram.
Hali hiyo imekuja siku moja baada ya nyota huyo kuifungia bao la tatu Yanga dakikia za mwisho kwenye mchezo timu hiyo ilioshinda 3-1 dhidi ya Gwambina na kuonesha ishara ya mabadiliko huku akinyosha kidole chake kwenye kichwa.
Ishara ile ilitafsiriwa kwa namna tofauti na wadau wa soka kwani baada ya kufanya vile alitoka nje ya uwanja na hata kaimu kocha mkuu wa timu hiyo Juma Mwambusi alivyomtaka arudi uwanjani aligoma na kuvua fulana yake na kuiweka begani kisha kuondoka uwanjani hapo akiwapigia makofi mashabiki.
Katika mchezo huo Saido alianzia nje na aliingia dakika ya 66 kuchukua nafasi ya Tuisila Kisinda aliyeumia bega sekunde chache nyuma.
Ufutaji wa picha hizo zenye maadhari, muonekana, jezi na vitu vingine vinavyoihusu Yanga ikiwemo zile alizopiga na wachezaji wa timu hiyo kumeleta sintofahamu kwa baadhi ya mashabiki wa Yanga huku wengi wakidhania kuwa anaweza kuwa anaachana na chama hilo kwa siku za hivi karibuni.
Mashabiki wengine wameenda mbali na kuanza kutoa lugha za matusi juu yake huku wengine wakisikilizia nini kinachofuta baada ya matukio hayo mfululizo.