Mshambuliaji wa Yanga, Mrundi Said Ntibanzokiza ‘Saido’ ana mengi ya kuzungumzia ndani na nje ya soka.
Mwanaspoti lilisafiri hadi Avic Town, Kigamboni kwenye kambi ya kishua ya Yanga kumfuata Saido na kufanya naye mahojiano ambapo alifunguka mambo kibao.
Saido ni nyota wa zamani wa klabu za Vital’O ya Burundi, Cracovia ya Poland, Akhsar Belediyespor ya Uturuki, Caen ya Ufaransa na Kaysar Kyzylorda ya Kazakhstan.
AICHAMBUA YANGA
Saido ambaye ni nahodha wa timu ya taifa ya Burundi ameichambua timu hiyo kwa mapana akitumia uzoefu wake wa kuwepo ndani ya kikosi hicho tangu msimu uliopita.
Mshambuliaji huyo ambaye anasifika zaidi kwa kufunga mabao ya faulo na penalti na juzi aliipata timu yake ushindi katika mechi ya Ligi Kuu dhidi ya Biashara United akifunga bao la pili kwa penalti na mechi kumalizika kwa ushindi wa 2-1 katika Uwanja wa Benjamin Mkapa, anasema Yanga imekuwa bora sana msimu huu.
Anaeleza kuwa Yanga ya msimu huu ni bora zaidi kuliko msimu uliopita kutokana na wachezaji waliopo na namna inavyocheza.
“Kuna tofauti kubwa kati ya Yanga ya msimu uliopita na hii ya sasa. Msimu huu wamesajili wachezaji bora ambao kwa kushirikiana na waliokuwepo wanatengeneza muunganiko mzuri,” anasema.
“Timu iko na morali kubwa na ukiangalia namna inavyocheza unagundua kuna kitu inakitafuta kwani kila mchezaji anajituma kuhakikisha matokeo chanya yanapatikana.”
ISHU YAKE NA NABI
Hapo nyuma kidogo, Saido alikuwa haonekana kucheza mechi licha ya kwamba alikuwa akifanya mazoezi na timu na ishu kubwa ilielezwa kuwa ni kutokuwa na maelewano mazuri na kocha mkuu wa timu hiyo, Nasreddine Nabi, lakini staa huyo anaeleza kuwa hayo yaliisha na sasa wanaendelea vizuri.
“Hayo yamepita na sitaki kuyazungumzia kabisa. Kwa sasa namshukuru Mungu kwa kiwango ninachokionyesha, hivyo naomba tu kuwa na afya njema ili niendelee kuipambania timu na kuwafurahisha mashabiki wa Yanga,” anasema.
MKATABA MPYA
Mkataba wake na Yanga unatamatika mwishoni mwa msimu huu na hadi sasa ameonyesha kiwango boray lakini bado hajaongezewa, Mwanaspoti lilipomuuliza kuhusu hilo Saido alijibu hivi: “Bado nina mkataba na Yanga, siwezi kusema muda huu nitaongeza au nitaondoka, lakini kwa sasa bado nipo sana Yanga hadi mwisho wa msimu ndipo nitajua nini kinafuata.”
Saido alijiunga na Yanga katika dirisha dogo la msimu uliopita akitokea Vital’O ya kwao Burundi na tangu amejiunga na wana Jangwani hao amekuwa akicheza vizuri huku akitumika kama mchezaji kiongozi kwa kuwaelekeza wenzake kutokana na uzoefu alionao.
TIMU YA TAIFA BURUNDI
Taarifa kutoka Burundi zinaeleza kuwa Saido ni miongoni mwa mashujaa wanaokubalika hususan akiwa timu ya taifa ‘Intamba m’Urugamba’ na hapa anaichambua timu hiyo na kuweka wazi malengo yake. “Timu yetu ya taifa ipo vizuri, ina wachezaji wengi wenye uwezo mkubwa na wazalendo sana.
“Tuliteleza na kushindwa kufuzu Afcon lakini tunaendelea kujipanga kuhakikisha tunashiriki Chan mwakani,” anasema Sai-do.
USHIN-DANI WA NA-MBA
Ku-mbe haogopi! Saido anafunguka kuwa haogopi ushindani wa namba uliopo kikosi cha Yanga kutokana na wachezaji waliopo na wapya wanaosajiliwa kwani anajiamini.
Anaeleza kuwa timu ikiwa na wachezaji wengi bora ndio vizuri kwani ushindani unaongezeka na kujenga kikosi imara.
“Mimi sina tatizo kwani ni kawaida ya timu kubwa kuwa na wachezaji wengi bora, lakini naamini kwenye ubora wangu na kila nikipata nafasi najitahidi kufanya vizuri zaidi,” anasema Saido.
MIKOANI NOMA
Sadio amefunguka kuwa mechi za nje ya Dar es Salaam huwa ngumu kwake kutokana na viwanja kutokuwa rafiki.
Anasema licha ya kucheza timu nyingi hajapata changamoto kubwa kama anayokutana nayo kwenye viwanja vya mikoani.
“Aisee mikoani ni noma. Vile viwanja sio vizuri, kuna muda hadi pasi hazipigiki kwa ufasaha. Hiyo ni changamoto na mara nyingi timu pinzani hucheza rafu kutokana na kutokuwa na uhakika na mpira kutulia katika viwanja,” anasema mwamba huyo tajiri anayemiliki vitu mbalimbali kama magari ya kifahari na ya abiria na mitindo ya nguo zake zenye nembo ya ‘Lion 10’ ambayo ni a.k.a yake.
AFICHUA SIRI
Kwa miaka ya hivi karibuni wachezaji wengi kutoka Burundi wamekuwa wakija Tanzania kucheza soka na wengine kujizolea umaarufu mkubwa na kuondoka, lakini Saido anataja siri ya wao kuja Bongo. Laudit Mavugo, Didier Kavumbagu na Amissi Tambwe ambaye kwa sasa anakipiga DTB ya Championship ni miongoni mwa wachezaji wa Burundi ambao miaka michache iliyopita waliliteka soka la Bongo kutokana na viwango vyao kuonekana kuwa bora na kuwavutia watu wengi.
Haikuishia hapo, msimu huu pia katika timu tofauti za Ligi Kuu Bara kuna wachezaji wengi kutoka Burundi kama kina Stive Nzigamasabo (Mtibwa Sugar), Bigirimana Blaise, Jonathan Nahimana na Erick Kwizera (Namungo), Emmanuel Mvuyekure (KMC) na wengine kibao. Sio kwa wachezaji tu bali hata makocha kutoka Burundi wamekuwa wakija Tanzania na kujizolea umaarufu na Saido amefichua siri ya yote hayo kuwa ni kujitambua kwa wanamichezo wa Burundi.
“Sio kwamba Warundi ndoto zao ni kucheza au kufanya kazi Tanzania, hapana, lakini siri kubwa ni kwamba wana ndoto kubwa, hivyo huwa wanaitumia Tanzania kama daraja la kuonekana kile wanachokifanya na kusonga mbele zaidi, hiyo ndiyo siri kubwa,” anasema Saido ambaye ni mchezaji pekee anayecheza Tanzania aliyewahi kucheza Ligi Kuu ya Ufaransa 2015/2016 akiwa na Caen.