Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Saido afikia rekodi ya miaka 15 iliyopita

SAIDOOO Saido Ntibazonkiza

Fri, 9 Jun 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Kiungo mshambuliaji wa Simba, Saido Ntibazonkiza amevunja rekodi iliyodumu kwa miaka 15 ya kufunga mabao matano katika mechi ya Ligi Kuu Bara dhidi ya Polisi Tanzania iliyokuwa inashikiliwa na straika, Nsa Job, aliyekuwa Azam FC.

Ntibazonkiza pia ana rekodi ya kufunga  'hat-trick' mbili msimu huu kama alivyowahi kufanya Job.

Mrundi huyo ambaye alisajiliwa na Simba kipindi cha dirisha dogo, aliiwezesha timu yake kushinda mabao 6-1, mechi ya raundi ya 29 iliyochezwa kwenye Uwanja wa Azam Complex, Dar es Salaam na kufikisha mabao 15, akibakisha moja tu kumfikia, Fiston Mayele wa Yanga.

"Nashukuru timu yangu kwa kupata matokeo mazuri na mimi kufunga mabao matano, kikubwa siangalii sana ufungaji bora, ninachoangalia ni timu kwanza kupata matokeo bora halafu vitu vingine tunaangalia baadaye, Fiston (Mayele) ni mchezaji mzuri na mfungaji mzuri, kama ikitokea nikifanikiwa kuwa mfungaji bora nitafurahi na kumshukuru Mungu," alisema kiungo huyo.

Ntibazonkiza alipachika mabao hayo dakika ya 15, 20, 27, 79 na 89, ikiwa ni 'hat-trick' yake ya pili msimu huu ambao unamalizika kesho, ya kwanza akiifunga Desemba 30, mwaka jana kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam, Mnyama akiwachapa Tanzania Prisons mabao 7-1.

Mabao hayo alifunga dakika ya 61, 63 na 70, katika mechi ambayo pia nahodha wa Simba, John Bocco, pia alipiga 'hat-trick'.

Inakuwa ni 'hat-trick' ya sita katika Ligi Kuu msimu huu, nyingine zikiwekwa na Bocco (mbili), moja kwenye mechi dhidi ya Ruvu Shooting mechi ikichezwa Novemba 19, mwaka jana Simba ikishinda mabao 4-1.

Mayele alipiga hat trick yake kwenye mechi ya iliyochezwa Novemba 17, mwaka jana, Uwanja wa Benjamin Mkapa, Yanga ikiifunga Singida Big Stars mabao 4-1, na Ibrahim Mkoko wa Namungo aliyefunga katika mechi dhidi ya KMC, timu yake ikishinda magoli 3-1.

Mara ya mwisho mchezaji kufunga mabao matano kwenye Ligi Kuu Tanzania Bara ilikuwa ni Machi 24, mwaka 2009, msimu wa 2008/09, iliyowekwa na Job, akifunga dakika ya 21, 24, 51, 79 na 87, Azam ikiishindilia Villa Squad magoli 6-2.

Msimu wa Ligi Kuu Bara 2022/2023 unatarajiwa kumalizika kesho kwa timu zote kushuka dimbani wakati tayari Ruvu Shooting na Polisi Tanzania zimeshashuka daraja.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live