Kumekuwa na minong’ono juu ya uamuzi wa Kocha Mkuu wa Simba, Roberto Oliveira ‘Robertinho’ kuwachezesha kwa pamoja viungo washambuliaji, Clatous Chama na Saido Ntibazonkiza, baadhi ya watu wanadai hawapaswi kutumiwa hivyo na wengine kuona freshi tu.
Nyota hao ambao wamekuwa kama ndio injini ya timu hiyo kwenye mechi za Ligi Kuu na ile ya CAF wamekuwa wakianzishwa pamoja tangu, Saido aliposajiliwa kupitia dirisha dogo na moto wao mwanzoni chini ya Kocha Juma Mgunda aliyekuwa akiishikilia timu ulionekana wa kutisha zaidi.
Hata hivyo, baada ya Robertinho kutua na kuanza kuwatumia kwa pamoja wameshindwa kutisha licha ya awali kuonekana kama kombinesheni yao ingelipa katika mechi za awali kabla ya kupotea katika mechi tatu zilizopita za mashindano kwa kushindwa kufanya maajabu uwanjani.
Baadhi ya wadau wa soka wamewaangalia wachezaji hao na kusema Saido na Chama wana sifa zinazolingana hivyo kucheza pamoja huifanya timu ipungue nguvu katika kujilinda kwani wote ni wazuri zaidi kwa kushambulia, huku baadhi wakimtetea kocha kwa kile wanachosema jukumu lao mama ni kushambulia na sio kuzuia.
Wanaomtetea Mbrazili wanasema mbona walipokuwa chini ya Mgunda waliwasha moto na kutengeneza mabao ya kutosha dhidi ya Tanzania Prisons walioifumua 7-1 kabla ya ujio wa Robertinho na kuonyesha maelewano makubwa na kuchangia mabao mengi tofauti na ilivyo sasa.
Wawili hao chini ya Mgunda walihusika kwenye mabao saba katika mechi moja waliyocheza pamoja ambapo Chama hakufunga, lakini aliasisti mbili, huku Saido alifunga hat trick na kuasisti moja.
Kisha ndipo Robertinho akaanza kazi kwenye mechi ya Mbeya City na timu kuibuka na ushindi wa mabao 3-2, Saido alifunga mabao mawili na asisti moja, huku Chama pia akitoa asisti moja kabla ya kutolewa na kuzua mzozo mkubwa.
Mechi ya pili ya Robertinho ilikuwa ni dhidi ya Dodoma Jiji, lakini Chama hakuambatana na timu na Simba ikashinda 1-0, huku Saido alicheza akishirikiana na kina Jean Baleke aliyefunga bao pekee.
Timu ikacheza mechi ya Kombe la AZFC ikiwa chini ya Mgunda tena baada ya Robertinho kuondoka kwa dharura na Chama na Saido walicheza pamoja na timu kushinda 1-0, huku Chama akihusika kwenye bao baada ya kutoa pasi kwa Pape Ousmane Sakho aliyempa Saido Ntibazonkiza kisha Mbrazili akarudi na kuwaanzisha tena dhidi ya Singida Big Stars, Simba iliibuka na ushindi wa mabao 3-1 yalifungwa na Saidoo bao moja Chama asisti mbili dhidi ya Baleke na Sakho.
Robertinho amebadili maeneo ya uchezaji kwa nyota hao kwani kipindi cha Mgunda Saido alishambulia kutokea pembeni na Chama kucheza kama namba 10, lakini kwa sasa Chama anatokea pembeni na Saido ndiye anacheza katikati.
Kwenye mechi mbili za kimataifa Kombe la Ligi ya Mabingwa Afrika Simba ikicheza mechi mbili na kupoteza zote ni mechi moja wamecheza pamoja dhidi ya Raja Casablanca wamefungwa mabao 3-0.