Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Said Mbatty: Nahodha Tabora United aliyeisotea Ligi Kuu Bara

Said Mbatty . Said Mbatty.

Mon, 16 Oct 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Said Mbatty sio jina geni katika soka hapa nchini kutokana na kucheza misimu 10 tofauti, tisa ikiwa ni katika madaraja ya chini huku mmoja Ligi Kuu na sasa ni nahodha wa Tabora United ambayo inashiriki Ligi Kuu.

Hivi karibuni, Mbati alifanya mahojiano na Spoti Mikiki akafichua mengi kuhusu maisha ya soka na nyakati alizokutana na changamoto iliyomfanya ajihusishe na usafirishaji abiria kwa pikipiki maarufu kama bodaboda ili ajipatie riziki.

“Nimepambana hadi nafika hapa nilishawahi kukata tamaa kisa kushindwa kupata nafasi ya kucheza Ligi Kuu kutokana na kupandisha timu na kuachwa,” anasema.

UDEREVA HADI UNAHODHA

Kila binadamu ana ndoto zake katika maisha kwani kuna wanaopenda kuwa walimu, madaktari na majukumu mengine lakini kwa upande wa Mbatty anakiri kuwa alikuwa ana ndoto ya kuwa dereva.

“Nimelelewa katika familia ya soka na mjomba ndiye alikuwa ananinunulia vifaa vya michezo akinitaka niwe mchezaji jambo ambalo nililifurahia,” anasema Mbatty.

“Nakumbuka kipindi hicho nilikuwa naishi Kariakoo kwa mjomba ambaye ni maarufu kwa jina la Mzee Nyumba alikuwa ni kiongozi wa Pan Africa ndiye alinifanya niwe mchezaji.”

SOKA HADI BODABODA

Kazi yoyote ina changamoto na sio wachezaji wote wanaweza kukamilisha ndoto kutokana na changamoto wanazokutana nazo wengine wamekuwa wakizifikia huku wengine wakiishia njiani.

“Nimecheza soka kwa muda mrefu, lakini nilikuwa naishia madaraja ya chini. Kuna kipindi napambana kupandisha timu daraja lakini naachwa,” anasema mchezaji huyo.

“Nilipandisha Mwadui FC, nilicheza msimu mmoja wa pili tulipanda nikaachwa. Nikacheza Polisi Tabora ilishushwa daraja na Geita Gold, nikatimkia Stand United ya Ligi Kuu kwa mara ya kwanza nikacheza nakumbuka ulikuwa msimu wa 2017 sikuwa na bahati kwani nikaumia mbavu sikufanikiwa kucheza mechi hata moja.”

Anasema baada ya kushindwa kucheza msimu mzima aliachwa akaamua kutimkia Mlale JKT na pia alishindwa kuipandisha baada ya kuzidiwa pointi moja ilipofungwa na na KMC.

Matty anasema baada ya kuona amekuwa na bahati mbaya ya kushindwa kukipiga Ligi Kuu aliamua kuachana na soka msimu wa 2018 na kununua bodaboda na bajaji kuwekeza huko.

“Soka sikuona kama ni bahati kwangu. Nikaamua kuachana nalo na kuamua kuingia kwenye kazi ya bodaboda na bajaji,” anasema Mbatty.

MATUNDA FC YAMRUDISHA UWANJANI

Maisha yana changamoto zake unaweza ukatoka sehemu ukashindwa kufikia malengo na kujaribu mambo mengine haya ni majibu ya Mbatty katika kujaribu.

“Baada ya kuamua kufanya mambo ya bodaboda na bajaji nikiwa kitaani nilikuwa na marafiki zangu ambao wanapenda soka wakawa wananichukua na kunipeleka mazoezini.

“Mtaani tuna timu inaitwa Matunda FC hii ndio naweza kusema iliyonipa nguvu za kurudi uwanjani. Kuna siku kulikuwa na mechi ya kirafiki pamoja na mazoezi yangu ya beach (ufukweni) nilionekana kuwa fiti,” anasema.

“Kutokana na ubora niliouonyesha kwenye mchezo huo nikapata nafasi ya kucheza tena Ashanti United na baadaye nikajiunga Ndanda FC ikiwa Ligi Kuu.

“Nikiwa Ndanda FC baada ya kushuka ndio nilionwa na Kitayosce ikiwa daraja la chini. Nimedumu nayo kwa misimu minne, msimu mmoja Division One (Daraja la Pili)na miwili Championship (Daraja la Kwanza) na ulioisha nimepandisha ligi timu baada ya miaka 10.”

KISA MFUNGO ATUMIA DAKIKA 15

Mara nyingi wachezaji Waislamu wamekuwa wakipita wakati wa mfungo wa Ramadhani wakiwa kwenye ligi na hawajawahi kuachana na imani bali hufuata sheria kama kawaida na hii imethibitishwa na Mbatty.

“Nakumbuka kipindi cha mfungo tukiwa Championship tulicheza mechi na Biashara United ilikuwa ni siku ya mfungo tatu na hatukuwahi kufanya mazoezi jioni siku hiyo nilifunga sambamba na beki mwenzangu ambaye tunaishi chumba kimoja.

“Nilikuwa naishi na Komanje Sandale basi mechi ilitushinda kabisa tulicheza dakika 15 na kutolewa nje kwa pamoja. Sitasahau niliumia sana kwa sababu ni wachezaji ambao tulikuwa tunategemewa,” anasema.

Mbatty anasema wote wawili msimu huo kabla ya mchezo walikuwa tayari wamecheza mechi 25 za msimu mzima huku akikiri kuwa hadi anamaliza msimu hakupata kadi hata moja ya njano wala nyekundu.

GUU LA KUSHOT LABADILI NAMBA

Sio kila mchezaji anayejua mpira anaweza kucheza nafasi zote uwanjani, kuna wanaocheza nafasi moja na wengine zaidi ya nne huku wengine kila nafasi wakiweza kucheza, lakini upande wa Mbatty anakiri kuwa alianza kucheza nafasi ya kiungo na sasa beki.

“Zamani kila mtu ambaye alikuwa na ndoto ya kucheza soka alikuwa anaanza na nafasi ya kiungo namba sita au nane na mimi nimetoka huko,” anasema nyota huyo.

“Nikiwa chini ya kocha Antonia Metod ambaye alikuwa anainoa JKT Tanzania na kushindwa kuipandisha kabla ya Malale Hamsini ndio nilibadili nafasi ya kucheza.”

Mbatty anasema mbali na kubadilika chini ya kocha huyo kutokana na kutumia mguu wa kushoto, ila alipojiunga na kituo cha Kinondoni Spoti Academy (Kisa) alijifunza kucheza nafasi nyingi zaidi.

Anasema kwa sasa licha ya kuwa na uwezo wa kucheza nafasi nyingi, lakini anafurahi zaidi kucheza nafasi aliyopewa na amekuwa akifanya vizuri.

UNAHODHA NI WITO

Kuongoza wachezaji 11 uwanjani kutokana na kitambaa anachovaa mchezaji mmoja mkononi uwanjani kukiwa na wachezaji wengi zaidi sio kazi ndogo. “Nimekuwa nahodha wa Tabora United kwa sasa kwa misimu minne. Kuna muda naweza kupishana kauli na wenzangu lakini ukiwa kiongozi busara huwa mbele.”

Chanzo: www.tanzaniaweb.live