Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Safari ya Tarimba, GSM Lubumbashi kuna jambo

Gsm 0 Vigogo wa Klabu ya Yanga

Sun, 2 Apr 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Leo kabla ya Mashetani Wekundu, Man United haijashuka Uwanja wa St James Park kuvaana na Newcastle United, mashabiki wa Yanga tayari watakuwa na matokeo ya pambano la timu hiyo dhidi ya TP Mazembe, lakini kuna jambo limeshtua wadau na kujikuta wakisema 'Yanga hii kweli imepania'.

Juzi wakati ikiondoka jijini Dar es Salaam, msafara wa Yanga ulishtua kwa kuwa na vigogo kadhaa, lakini sura mbili zilishtua zaidi za Tarimba Abbas na bilionea wa klabu hiyo, Ghalib Said Mohamed 'GSM' kutokana kilichokuwa kikielezwa mtaani baada ya kutua kwa udhamini wa Haier klabuni hapo.

Tarimba ndiye kigogo wa Wadhamini Wakuu wa Yanga, SportPesa, hivyo ilidhaniwa kwa GSM kuruhusu kampuni ya Haier kuingia Yanga kuidhamini kwenye michuano ya CAF kungeibua 'bifu' kubwa na pengine wawili hao kwa sasa wasingekuwa wakiiva chungu kimoja, lakini mambo sivyo.

Wawili hao kwa pamoja walikuwa sambamba na Rais wa Yanga, Injinia Hersi Said na makamu wake, Arafat Haji mbali na Geofrey Mwambe ambaye ni Mjumbe wa Baraza la Wadhamini wa Yanga na Mbunge kama ilivyo kwa Tarimba, mbali na Lameck Nyambaya Mwenyekiti wa Chama cha Soka Mkoa wa Dar es Salaam (DRFA) akiwa ndiye mkuu wa msafara wa timu hiyo jijini Lubumbashi.

Uwepo wa watu hao wazito kwenye msafara imeelezwa ni moja ya mkakati wa Yanga wa kuhakikisha kesho wanaimaliza Mazembe kama ilivyofanya katika mechi ya kwanza iliyopigwa Kwa Mkapa na Wakongo hao kulala mbao 3-1.

Kilichowapa raha zaidi mashabiki wa klabu hiyo ni hashtag iliyoambatana na video ya GSM ikieleza; 'Tunasafiri kwenda Congo na Boss #GSM je tutarudi na nani?', ambapo washangiaji walijibu swali hilo kuonyesha furaha yao na kumkubali bilionea huyo, aliyeisajilia timu mastaa walioibeba hadi sasa. Taarifa kutoka kwenye msafara na katika kambi ya timu hiyo iliyopo Lubumbashi, zinasema kuwa, imeongeza mzuka kwa mastaa ambao inadaiwa pia wameahidiwa donge nono wakishinda kesho.

Licha ya hamasa hiyo, ikijumuishwa na mashabiki waliosafiri kwa mabasi kwenda kuamsha shangwe DR Congo, lakini uwepo wa baadhi ya wachezaji kutoka nchini humo wenye uzoefu dhidi ya Mazembe kama kina Fiston Mayele, Yannick Bangala, Jesus Moloko, Joyce Lomalisa, Tuisila Kisinda na Djuma Shaban waliowahi kukipiga AS Vita inaelezwa ni faida nyingine ya kuibeba Yanga.

Chanzo: Mwanaspoti