Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Safari ya Chama ilianzia katika 5-1

Chama Ss Safari ya Chama ilianzia katika 5-1

Wed, 3 Jul 2024 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Baada ya muda mrefu wa kuhusishwa kwa muda mrefu kusajiliwa na Yanga, hatimaye mapema Jumatatu, wiki hii Clatous Chama alitambulishwa rasmi na klabu hiyo kama mchezaji wao mpya.

Chama amejiunga na Yanga akiwa mchezaji huru baada ya mkataba wake wa miaka miwili na Simba kufikia tamati, Juni 30 mwaka huu na klabu hiyo kuamua kutomuongezea mkataba kiungo huyo mshambuliaji wa Zambia.

Kwa kipindi cha zaidi ya mwezi mmoja tetesi za Chama kuhusishwa kujiunga na Yanga zilikuwa zikisambaa kwa kasi katika vyombo vya habari na mitandao ya kijamii huku ikitajwa kwamba Simba haikuwa na mpango wa kumpa mkataba mpya.

Unamzungumzia Chama, mchezaji aliyejenga jina na heshima kubwa ndani ya Simba huku akiwa kipenzi cha mashabiki na wanachama wa klabu hiyo tangu alipojiunga nayo mwaka 2017 akitokea Zesco United ya Zambia.

Ni mchezaji aliyefanya makubwa ndani ya Simba na hilo linathibitishwa na takwimu ambazo ameacha katika mechi alizoichezea kwenye mechi za ndani na mashindano ya kimataifa.

Kwa mujibu wa takwimu, Chama katika michezo 179 ya Ligi Kuu na mashindano ya klabu Afrika, amehusika na idadi ya mabao 102 akifunga mabao 42 na kupiga pasi za mwisho 60.

Uamuzi wa pande hizo kunadhihirisha rasmi minong'ono ya muda mrefu ambayo ilikuwa ikiendelea ndani ya Simba ya kutokuwa na imani na kiungo huyo mshambuliaji kutoka Zambia akidaiwa amekuwa na mahusiano yaliyopitiliza na upande wa pili na kupelekea kuathiri kiwango chake ndani ya uwanja.

Ni kwa misimu mitatu mfululizo, viongozi na mashabiki wengi walikuwa wanamtazama Chama kama mtu ambaye amepoteza mapenzi ndani ya timu yao na anaitumikia kwa sababu ya fedha tu hivyo uzi baina yao ulikuwa unazidi kuwa mwembamba na kamba ilikuwa inaelekea kukatika.

Sio jambo la kificho kwamba kwa muda mrefu, viongozi wa Simba walikuwa wanatamani kuachana na Mwamba wa Lusaka hasa wakichagizwa na ripoti kutoka katika mabenchi yao ya ufundi ambayo mara kwa mara yalishauri timu hiyo iachane na Mzambia huyo kama inataka kupiga hatua zaidi.

Hata hivyo uamuzi wa kumuacha Chama ulikuwa mgumu kwa viongozi kwa vile walikuwa wanaogopa presha na lawama kutoka kwa mashabiki na wanachama wa timu hiyo kutokana na mahaba makubwa ambayo walikuwa nayo kwa nyota huyo kutoka Zambia.

Kulikosekana nyakati au tukio fulani ambalo lingewapa ujasiri viongozi wa kusimama mbele ya wanachama wao baada ya kuamua kuachana na Chama hadi pale ilipofika Novemba 5, 2023 pale ilipopoteza kwa mabao 5-1 dhidi ya Yanga katika mchezo wa mzunguko wa kwanza wa Ligi Kuu Tanzania Bara.

Ni matokeo ambayo kwa kiasi kikubwa yalibadilisha kwa kiasi kikubwa maisha ndani ya Simba na hilo linajidhihirisha katika namna tofauti.

Mahaba ya mashabiki wengi wa Simba kwa baadhi ya nyota ndani ya timu hiyo akiwemo Chama yalipungua wakiamini hawakucheza kwa kujituma katika mchezo huo huku wakienda mbali zaidi na kuwa tayari kuona wakitupiwa virago.

Kana kwamba haitoshi kulikuwa na tuhuma za baadhi ya wachezaji kuihujumu timu katika mchezo huo hadi kupelekea kupoteza kwa idadi kubwa ya mabao mbele ya watani wao wa jadi.

Lakini kingine mashabiki walianza kuamini kuwa inawezekana kupoteza mchezo tena hata kwa idadi kubwa ya mabao ukiwa na mastaa wako kikosini hivyo walianza kushinikiza kupewa nafasi kwa wachezaji ambao awali hawakuwa wakiaminiwa na benchi la ufundi mbele ya mastaa hao.

Hiyo ilitengeneza urahisi kwa uongozi wa Simba kuchukua maamuzi magumu katika dirisha hili kubwa la usajili kwa vile unafahamu kuwa kundi kubwa la wanachama na mashabiki kwa sasa linaimba nao lugha moja tofauti na awali ambapo ingekuwa gumu kufanya uamuzi ambao ungekuwa hauungwi mkono na mashabiki walio wengi.

Wimbo wa kuitengeneza Simba mpya na kuwapa mkono wa kwaheri mastaa ambao wamedumu kwa muda mrefu ulianza kusambaa na kueleweka kwa kasi vichwani mwa Wansimba na wengi wakawa wanatamani kuona fagio la haja linapita ili waanze upya.

Kitendo cha kupewa 'Thank You' kwa watu kama John Bocco, Luis Miquissone na Saido Ntibazonkiza ambao walikuwa wachezaji waandamizi kikosini, kilikuwa ni kama kinawaandaa kisaikolojia mashabiki na wanachama kuwa wawe tayari hata kuondoka kwa kipenzi chao Chama.

Tangu Simba ilipofungwa mabao 5-1 na Yanga hadi dirisha la usajili lilipofika mashabiki, wanachama na viongozi wake walikuwa kama wamechomwa ganzi na wasingeweza kusikia maumivu yoyote kwa mchezaji yeyote kuondoka.

Ndio maana haikushangaza kuona licha ya kufahamu mkataba wa Chama unaelekea ukingoni, hawakujihangaisha kumuongezea mkataba mpya na badala yake wakawa wanampambania Kibu Denis abaki.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live
Related Articles: