Wakati kikosi cha Mbeya City kikiondoka leo kuelekea Singida kwaajili ya mchezo wa robo fainali Kombe la Azam Sport Federation (ASFC) utakaopigwa wikiendi hii benchi la ufundi limepata pigo.
Kocha Msaidizi wa Mbeya City, Anthony Mwamlima alisema mshambuliaji wao tegemeo, Sixtus Sabilo anasumbuliwa na majeraha na anaweza kuukosa mchezo huo.
Alisema Sabilo kwa wiki chache hali yake ya kiafya haijakaa sawa na hata mchezo wa Jumapili dhidi ya Singida Big Stars utakaopigwa Uwanja wa Liti hawana uhakika kama atacheza.
“Tutasafiri naye hadi Singida lakini suala la kucheza au kutokucheza linategemeana na ripoti ya mwisho ya daktari wa timu jinsi atakavyoshauri kama atafaa kucheza.
“Wachezaji wengine wapo salama na afya njema ambao tunauhakika watafanya vyema katika mchezo huo muhimu kwetu kusonga hatua ya mbele,” alisema Mwamlima.
Aliongeza hesabu za kumaliza ‘Top Four’ kwenye Ligi Kuu hazipo na sasa wanapambana kuona watavuna alama tatu katika michezo mingine ya ligi iliyobaki.
Daktari wa timu hiyo, Stanley Kayombo alisema Sabilo alipata tatizo la mshtuko wa misuli na akapewa siku kadhaa za mapumziko na sasa anaendelea vizuri.
“Kabla ya mchezo tutafanya mazoezi ya mwisho na ninaamini atakaa sawa na kutumika vyema kwa kadiri benchi la ufundi litakavyoona sababu siku alizopewa kupumzika zimefika.
“Tunaamini atafanya vyema kwenye mchezo huo suala la kuumwa hilo tuwaondoe shaka wapenzi wa Mbeya City.”