Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Sabilo fundi aliyerejea na moto mpya Ligi Kuu Bara, alivyonusurika...

Sabiloo Sixtus Winga wa Mbeya City, Sixtus Sabilo

Wed, 31 Aug 2022 Chanzo: Mwanaspoti

Safari ya soka na maisha ya Sixtus Sabilo ambaye amejulikana zaidi kupitia Timu ya Namungo FC imejaa huzuni, furaha, simanzi na mafunzo makubwa lakini hakuwahi kukata tamaa kupigania kutimiza ndoto zake.

Winga huyo msimu huu anaitumikia Mbeya City na ameanza vizuri kwani tayari ameishafunga mabao mawili.

Ameishaifungia klabu yake hiyo katika michezo ya Ligi Kuu ya Tanzania Bara dhidi ya Dodoma Jiji ambao walishinda 3-1 na Singida Big Stars walipoteza kwa mabao 2-1.

Katika mahojiano na Mwanaspoti, kuna wakati simanzi ilitawala hasa alipokumbuka maisha aliyopitia mpaka kuwa mchezaji wa soka.

Sabilo ambaye amewahi pia kuzichezea Stand United, na Polisi Tanzania anafunguka mambo ya kushangaza ikiwemo la kunusurika kufa katika Ziwa Victoria.

ALIVYONUSURIKA

Sabilo anasema amezaliwa na kukulia katika Kijiji cha Kasahunga, wilayani Bunda mkoani Mara na shughuli kubwa ya wakazi wa eneo hilo ni uvuvi katika Ziwa Victoria.

Anasema alikuwa mvuvi ambapo katika udogo wake alinusurika kufa mara baada ya mtumbwi aliokuwa akivua kuzama.

“Unajua lile ziwa ni kubwa sana huoni nchi kavu lakini kwa sababu tulikuwa na dira hiyo ndio tuliyokuwa tukiitumia.

“Nakumbuka nilikuwa katika hali tete tulikaa kwenye maji kwa saa tano nikisubiri nije niokolewe.

“Mtumbwi ulizama kuanzia saa tatu asubuhi nilikaa mpaka saa nane ndio nikapata msaada wa wenzetu walikuja kutuchukua. Hapo nilikuwa ni kijana mdogo tu, ndio nimemaliza darasa la saba,” anakumbuka Sabilo.

Anasema baada ya kuokolewa hakutaka kurudi tena kuvua ziwani ndio mwanzo wa kurudi shule na kuanza kidato cha kwanza katika Shule ya sekondari ya Nyeruma ambako ndiko kipaji chake cha kucheza soka kilipoanza kuonekana.

KILICHOMSHTUA

Sabilo anasema katika shule hiyo ndiko kulikomfanya ajue ana kipaji cha kucheza soka kupitia mashindano ya Umiseta.

Mwaka 2011 alishiriki Mashindano ya Umiseta Kibaha mkoani Pwani akiutumikia Mkoa wa Mara.

“Nilicheza katika mashindano yale na kuonesha uwezo mkubwa lakini hakuna mtu aliyenifuata, hivyo nilirudi nyumbani nikiwa mpole ila nilijiona nimecheza vizuri.

“Mwaka 2013 nikawaona wale waliokuwa wakichezea mikoa yao wakicheza Ligi Kuu, nilishtuka nikajua kama wale wanacheza na mimi nina kipaji.

Anawataja baadhi ya wachezaji waliocheza kwenye Umiseta na baadaye wakaanza kucheza Ligi Kuu kuwa ni Erick Mlilo, Danny Lyanga na Shiza Kichuya.

“Nikasema na mimi naweza, hivyo nikawa natafakari nitafanyaje ili na mimi kipaji changu kiweze kuonekanekana.

“Sikuwa natamani kurudi nyumbani kwa sababu kuna maisha ya ufukara nilikuwa natamani kupitia kipaji changu nikiokoe kizazi changu kutoka katika lindi la umaskini,” anasema Sabilo.

NDONDO YAMLETA MJINI

“Kuna Mzee anaitwa Kadoto Mboje alinitoa nyumbani kijijini na kunileta mjini kulikuwa kuna mashindano yaliyoandaliwa na Ester Bulaya (aliyewahi kuwa Mbunge wa Bunda).

“Katika mashindano yale nilionesha uwezo mkubwa yule mzee akasema nisirudi kijijini nibaki mjini akiamini nitapa timu.

“Nilimshukuru kwa sababu kijijini maisha yalikuwa magumu na nilikuwa nimeishamaliza masomo nikiwa sijui hatma yangu ni ipi,” anasema Sabilo ambaye amewahi kuitwa Timu ya Taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’

MASSAWE AMVUTA LIGI KUU

“Katika ndondo hiyo nilikutana na mchezaji wa Namungo kwa sasa Jacob Massawe wakati huo akichezea Stand United.

“Alinifuata na kuniuliza nacheza timu gani nikamwambia sina timu, aliniambia najua mpira niende kwenye majaribio Stand United ile ya mwaka 2016 ya Kocha Mfaransa, Patrick Liewig.

“Niliwaza nikasema nitaweza kweli lakini nilivyoenda kocha alinielewa na huo ukawa mwanzo wa mimi kucheza Ligi Kuu.

Anasema Stand kipindi hicho ilikuwa ya moto kwani ilikuwa na wachezaji wenye uwezo mkubwa kama Adamu Kingwande, Amri Kiemba na Pastory Athanas.

“Nilijitahidi na nilipata nafasi ya kucheza na uwezo wangu ulionekana,” anasema Sabilo baba wa watoto wanne.

ALIVYOTAPELIWA

Winga huyo anasema wakati anajiunga na Stand United alisajiliwa kwa Shilingi 4 milioni wakati.

“Wakati naingia Stand United maisha yalikuwa sio mazuri kabisa nilivyoitwa na viongozi wa timu hiyo wakaniambia saini hapa tutakupa milioni nne.

“Nilikubali kwa sababu ndoto yangu ilikuwa ni kucheza, lakini sikupewa kitu baadaye nilikuja kupewa milioni moja tu tena baada ya kuonesha uwezo mkubwa,” anakumbuka winga huyo.

SOKA LIMEMPA KITU

“Sasa hivi sidaiwi kodi ninaishi kwangu, mahitaji madogo madogo hayanisumbui, familia yangu ipo vizuri pamoja na ndugu zangu.

“Nashukuru kwani bila soka ningekuwa mvuvi na wala nisingekuja mjini kwani niliokuwa nao karibia wote wapo kijijini,” anasema winga huyo.

MAISHA YA MBEYA CITY

“Yapo vizuri ni sehemu ambayo nimepokewa vizuri. Unajua ukicheza sehemu yenye amani unaonesha uwezo wako na mimi hapa naona nina amani na nitafanya mambo mazuri zaidi,”anasema.

NAMUNGO

Mchezaji huyo ambaye msimu uliopita aliichezea Namungo anasema: “Ruangwa kule ni sehemu nzuri tulipitia mambo magumu na mazuri pamoja nimejifunza vitu vingi sana kwangu ilikuwa ni hatua kubwa.

“Niseme nashukuru kwa hilo binafsi nawatakia kila heri na wataendelea kuwa watu wazuri kwangu.”

RAJA SIO WAAFRIKA

Winga huyo anasema amecheza michezo mingi lakini ambao anaukumbuka na hatausahau ni dhidi ya Raja Casablanca ya Morocco katika Mashindano ya Kombe la Shirikisho Afrika.

“Sisi tuliwaona kama vile wale sio Waafrika wenzetu. Kutokana na mafikio tuliyofikia ya kuingia hatua ya makundi Afrika, tulikutana na wapinzani ambao hawakuwa level yetu.

“Bahati nzuri tuiingia kwa kuwaheshimu. Mchezo ulikuwa mgumu kwetu lakini japo tulipoteza kwa bao 1-0 na unawajua Waarabu tena walitufunga kwa penalti baada ya mechi kumalizika hatujaamini,”anasema Sabilo.

Katika Ligi ya Bongo mchezo ambao anasema hatausahau ni wakati akiichezea Stand United msimu wa mwaka 2017-2018 walicheza dhidi ya Simba katika Uwwanja wa Taifa (sasa Benjamin Mkapa).

“Naukumbuka mchezo ule kwa sababu ulimalizika kwa kufungana mabao 3-3 kila mmoja alishangaa hii timu imewezaje kutoka sare na Simba ya moto ya wakati huo,” anasema Sabilo aliyekiri anavutiwa na uchezaji wa Jacob Massawe wa Namungo, lakini akikunwa pia na Erasto Nyoni wa Simba na Idd Seleman ‘Nado’ wa Azam FC.

“Nado ni vile tu msimu ulipita aliumia lakini napenda sana uchezaji wake ametoka Mbeya City na ameenda kudhihirisha kwa vitendo kwamba machezo wa soka anaujua pale Azam FC,” anasema Sabilo.

Tunamtakia kila la heri Sabilo. Aweze kufanya mambo mazuri zaidi anapoitumikia timu yake ya Mbeya City.

Chanzo: Mwanaspoti