Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Sabilo: Bado nipo nipo sana City

Sabilo Pic Sixtus Sabilo

Fri, 16 Dec 2022 Chanzo: Mwanaspoti

Wakati dirisha dogo la usajili likifunguliwa leo Alhamis hadi Januari 15 mwakani, Mshambuliaji wa Mbeya City, Sixtus Sabilo amesema hakuna timu iliyotuma ofa kwake na bado yupo yupo sana Mbeya City.

Sabilo amebakisha miezi sita kumaliza mkataba wa mwaka mmoja aliosaini na Mbeya City Julai 2022 akitokea Namungo wa mkoani Lindi.

Sabilo amekuwa na kiwango bora katika mzunguko wa kwanza wa Ligi Kuu Bara, kwa upande wa wazawa ndiye kinara wa mabao akiwa amefunga mabao saba huku Fiston Mayele wa Yanga na Moses Phiri wa Simba wakiwa na mabao 10 kila mmoja.

Pia, staa huyo ana assist sita sawa na Saido Ntibanzokiza wa Geita Gold na Ayoub Lyanga wa Azam huku Clautos Chama wa Simba akiongoza kwa assisti saba ambapo mwezi Oktoba alichaguliwa kuwa mchezaji bora wa mwezi huo.

Sabilo anatajwa kutakiwa na Singida Big Stars, Yanga na Dodoma Jiji kwa ajili ya mzunguko wa pili wa Ligi Kuu Bara.

Akizungumza Sabilo alisema hakuna timu yoyote iliyomfuata na yupo kambini na Mbeya City kujiandaa na mzunguko wa pili wa Ligi Kuu.

“Sina ofa yoyote mengine ni maneno tu nataka zaidi kuisaidia timu yangu na kuboresha zaidi kiwango changu,” alisema mshambuliaji huyo aliyeanzia maisha ya mpira Stand United ya mkoani Shinyanga.

Alipoulizwa kama atakuwa tayari kuondoka Mbeya City endapo atapata timu nyingine, Sabilo alisema; “Maisha yangu ni mpira ila bado nina mkataba na Mbeya City.”

Mshambuliaji wa zamani wa Kagera Sugar, Seleman Msagasumu alimshauri mchezaji huyo kumaliza msimu na Mbeya City na msimu ujao ndio atafute timu nyingine.

“Fedha zipo ila ukiwa unacheza Mbeya City, huko Kariakoo unaweza ukapata hela lakini ukawa na muda mchache wa kucheza,” alisema mshambuliaji huyo wa zamani wa Reli na CDA.

Chanzo: Mwanaspoti