Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Sababu za mastaa wa Ulaya kutaka kuhama Saudi Arabia

Benzema Ahusishwa Na Ugaidi Karim Benzema

Thu, 18 Jan 2024 Chanzo: Mwanaspoti

Ndoto ya kulipwa mishahara mikubwa na kwenda kuanza maisha kwenye ligi mpya ya Saudi Pro League imegeuka kuwa majanga kwa baadhi ya wanasoka duniani na sasa wanatafuta njia ya kurudi Ulaya.

Kundi kubwa la mastaa wa maana kwenye mchezo wa soka lilihamia huko Mashariki ya Kati katika dirisha la majira ya kiangazi la mwaka jana baada ya kuvutiwa na pesa kwamba wangekwenda kulipwa mishahara mikubwa kwa kujiunga na timu za Saudi Arabia.

Walishawishika na walifanya hivyo, ambapo mtangulizi wao alikuwa mshindi mara tano wa Ballon d’Or, Cristiano Ronaldo alipojiunga na Al Nassr akitokea Manchester United, Januari mwaka jana.

Lilipofika dirisha la majira ya kiangazi la mwaka jana, mastaa wengine wa nguvu kwenye soka akiwamo Karim Benzema, Neymar, Roberto Firmino, N’Golo Kante, Jordan Henderson, Riyad Mahrez, Jota, Aleksandar Mitrovic na wengineo kibao walikwenda kuungana na Ronaldo kwenye ligi hiyo ya Saudia.

Akaunti zao zimenona kwelikweli kutokana na mishahara wanayolipwa, ambapo Ronaldo inadaiwa anapokea Pauni 172 milioni kwa mwaka. Si pesa ndogo.

Sehemu kubwa ya wanasoka hao waliotimkia Saudi Arabia ni wale waliokwenda kujiunga na klabu zinazomilikiwa na nchi hiyo, Al-Ittihad, Al-Nassr, Al-Ahli na Al-Hilal - wakati kiungo wa zamani wa Liverpool, nahodha Henderson alikwenda kujiunga na Al Ettifaq inayonolewa na Steven Gerrard.

Lakini, miezi tu imepita tangu mastaa hao walipolipa kisogo soka la Ulaya, wengi wao wameshaanza kuhusishwa na mpango wa kuachana na maisha ya Saudia - ambapo Firmino anahusishwa na Fulham, Henderson anajiandaa kujiunga na Ajax, Jota anafikiria kutua Tottenham, na Benzema yupo kwenye rada za Chelsea.

Kwanini wachezaji hao wanataka kuhama Saudi Arabia mapema hivyo? Hizi hapa sababu chache zinazotajwa kuwa kichocheo cha wanasoka hao waliovutwa na pesa huko Saudi Arabia na sasa wanasaka njia ya kurejea Ulaya ikiwa imepita miezi michache sana.

Joto kali sana

Hali ya hewa ya Saudi Arabia inaripotiwa kuwafanya mastaa waliotoka Ulaya kushindwa kukabiliana na joto kali. Mazoezi yanafanywa jioni kutokana na hali ya hewa, ambapo kwa nyakati hizo nyuzi joto linafika hadi 40 katika baadhi ya maeneo ya nchi hiyo.

Imekuwa ikielezwa hiyo ni moja ya sababu za Henderson, 33, akitafuta namna ya kurudi Ulaya kwa sababu ameshindwa kuhimili joto kali wakati wa mechi. Na hilo haliwezi kushangaza.

Ronaldo, aliyekuwa staa mkubwa wa kwanza kuhamia huko Saudi Arabia akitokea Ulaya kwenda kucheza Saudi Pro League, alifichua namna alivyopata shida kuzoea mazingira mapya kutokana na hali ya hewa kuwa changamoto kubwa kwenye kuishi katika nchi hiyo kwa watu wasiokuwa wenyeji.

Hata nyakati za kufanya mazoezi huko Saudi Arabia zimekuwa tofauti, wanafanya nyakati ambazo joto limekuwa angalau kidogo limepoa.

Mashabiki wachache

Mastaa wa soka waliopata kucheza kwenye Ligi Kuu za Ulaya ambako zimekuwa zikivutia mashabiki wengi viwanjani wanakwenda kukutana na utamaduni tofauti kabisa kwenye mechi za Saudi Arabia. Mashabiki ni wachache sana wanaojitokeza viwanjani kutazama mechi.

Gwiji wa Liverpool, Henderson alizoea kucheza mbele ya mashabiki 50,000 uwanjani Anfield. Lakini, Novemba mwaka jana, wakati anaitumikia Al-Ettifaq mashabiki waliohudhuria uwanjani ni 610 tu.

Mwezi uliopita, kulishuhudiwa mechi yenye mashabiki wachache zaidi kwenye Saudi Pro League. Timu ya Al-Riyadh, inayoshika nafasi ya 15 katika ligi ya timu 18, ilicheza mechi mbili zilizohudhuriwa na mashabiki wasiofika 150 msimu huu.

Hata ile mechi ya kupambana kukwepa kushuka daraja kati ya Abha na Al-Hazm ilihudhuriwa na asilimia 1.2 tu ya uwezo wa uwanja, ambapo mashabiki 257 walihudhuria mechi wakati uwezo wa uwanja ni 20,000.

Staili tofauti ya maisha

Mambo mbalimbali ya staili za kimaisha imeripotiwa kuchangia kwa wachezaji wa kigeni kutaka kuachana na maisha ya Saudi Arabia.

Wanasoka hao wamekuwa na wakati mgumu juu ya wapenzi wao, ambapo wamekuwa na marufuku ya kutembea mitaani wenyewe. Vizuizi vya aina hiyo vimekuwa vikiwanyima wanasoka uhuru wa kufurahia maisha na familia zao wakiwa Saudia tofauti na walivyokuwa Ulaya. Huko Saudi Arabia, unywaji wa pombe si kitu unachoweza kukifanya kwenye hadhara, jambo ambalo limekuwa kikwazo kikubwa kwa maisha ya wanasoka wa kutoka Ulaya ambao wamekuwa na utamaduni na staili ya maisha ya aina tofauti kabisa.

Soka la kimataifa

Ishu nyingine inayowakwaza wachezaji wengi wa kutoka Ulaya ni hofu ya kupoteza nafasi kwenye kuzitumikia timu zao za taifa kwenye soka la kimataifa.

Soka la Saudia linaonekana kama halina upinzani mkali, hivyo makocha wa timu za taifa za Ulaya watafikiria zaidi kuchagua wachezaji wanaotoka kwenye ligi zenye ushindani mkali uwanjani ili kuunda timu zao wenye ubora mkubwa.

England inajiandaa na michuano ya Euro 2024, hivyo Henderson ambaye alikuwa nahodha wa Liverpool anataka kurudi Ulaya ndani ya dirisha hili la Januari ili acheze kwa ubora mkubwa kuanzia sasa hadi mwishoni mwa msimu ili kujitengenezea nafasi kwenye kikosi cha Three Lions.

Chanzo: Mwanaspoti