Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Sababu za MO kujitoa Simba

65798 Mo+pic

Sun, 7 Jul 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Mwekezaji wa Simba, Mohammed Dewji 'MO' amewaambia baadhi ya wajumbe wa bodi ya klabu hiyo sababu tano zinazomfanya afikirie kujitoa Msimbazi.

Licha ya hilo, amewaambia kuwa akiondoka atasamehe takribani Sh5 bilioni alizotumia kwa ajili ya mambo mbalimbali ya klabu hiyo ikiwa ni pamoja na ujenzi wa uwanja, usajili wa wachezaji, kulipa mishahara na mambo mengine.

Ndani ya Simba kuna mvutano mkubwa, huku mwenyekiti wa bodi ya Simba, Mo Dewji akiwa hayupo tayari kufanya kazi na mwenyekiti wa klabu, Sued Mkwabi kwa madai anamuhujumu.

Mmoja wa wajumbe wa bodi wenye nguvu Simba, amefichua kuwa Mo Dewji kawaambia kuwa hana imani na mwenyekiti wa klabu hiyo Mkwabi kwa sababu tano na kwamba akiondoka hatadai Sh5 bilioni ambazo ameshatumia kwa mambo mbalimbali.

“Ametuambia hana imani na mwenyekiti kwa sababu amekuwa akitoa habari za vikao nje, hafanyi majukumu anayopewa, hapendi mabadiliko, yupo karibu na watu wanaopinga mabadiliko na yupo karibu sana na baadhi ya watu wa Yanga,” amesema mjumbe huyo jana akiomba jina lake lisitajwe.

“Tupo vitani, unashangaa vikao vimekwisha tu baada ya dakika chache habari zipo kwa wapinzani wetu. Habari zinafikaje kwa wanaopinga mabadiliko tunayopitia, lakini wakati mwingine mpaka Yanga wanajua mipango yetu,” amesema mjumbe mwingine wa bodi ya Simba.

Habari kutoka katika klabu hiyo zinadai kuwa Mkwabi amekuwa akiwashutumu baadhi ya wajumbe walioteuliwa na Mo Dewji, jambo ambalo mwekezaji huyo anaona ni hujuma kwake.

Habari hizo zinasema Mo amekuwa akilalamika kuwa Mkwabi amekuwa akichelewesha baadhi ya majukumu anayopewa, ikidaiwa kuwa hata hati ya kiwanja inayoshikiliwa na Mzee Hamis Kilomoni anahusika.

“Wakati mwingine anaambiwa kwa sababu upo Cairo, nenda makao makuu ya CAF kafuatilie fedha zetu za kushiriki Ligi ya Mabingwa Afrika, lakini hafanyi lolote,” amedai mjumbe huyo.

Mvutano huo ulishika kasi Mei 30 mwaka huu wakati wa hafla ya Mo Simba Awards, baada ya Mkwabi kutopewa nafasi ya kuzungumza kwa nafasi yake ya mwenyekiti badala yake nafasi hiyo akapewa mwenyekiti wa zamani wa klabu hiyo, Salim Abdallah maarufu kwa jina la ‘Try Again’.

Inadaiwa kuwa Mkwabi amekuwa akiona kama madaraka yake Simba yanaporwa na kwamba hana nguvu tofauti na alivyotarajia.

Inadaiwa kuwa kutokana na hilo Mkwabi amekuwa akihoji mara kwa mara kuhusu uwezekaji wa Sh20 bilioni, na licha ya kuwa majibu anayo, amekuwa akirudia mara kwa mara kuhoji jambo hilo.

Kupata ufafanuzi juhudi za kumtafuta Mo Dewji simu yake ilikuwa ikiita tu bila kupokewa, lakini akaunti yake ya Twitter ilitoa ujumbe: “Kwenye uongozi, na kwenye maisha, huwa nakaribisha kukosolewa. Lakini siwezi na sikubali kufanya kazi na mtu anayehujumu malengo, mipango na maslahi mapana ya taasisi - mtu anayetoboa mtumbwi tunaosafiri nao.”

Kabla ya ujumbe huo, Mo alitangulia kuandika: "Watu wenye nia mbaya: Kazi yao sio kujenga, ni kuvunja tu. Kaa nao mbali. Narudia kaa nao mbali sana!"

Chanzo: mwananchi.co.tz