Kocha Mkuu Simba SC Robero Oliviera ‘Robertinho’ ametoa sababu za kushindwa kuwatumia Washambuliaji Jean Baleke, Pape Osman Sakho, John Bocco na Peter Banda, kwenye mchezo wa Mzunguko wa tatu wa Kundi C, Ligi ya Mabingwa Barani Afrika.
Wachezaji hao walikuwa kwenye orodha ya wachezaji wa akiba, lakini hawakupata nafasi ya kucheza mchezo huo wa ugenini, uliopigwa katika Uwanja wa St Mary’s-Kitende mjini Entebe, Uganda.
Robertinho amesema yalikuwa maamuzi ya Benchi la ufundi kwa wachezaji hao kuanzia Benchi na kuangalia uwezekano kama wangeweza kuingia, lakini haikuwa hivyo kutokana na mfumo alioutimia.
Kocha huyo kutoka nchini Brazil amesema, ni wazi kila shabiki wa Simba SC alitamani kuwaona wachezaji hao wanne wakicheza, lakini amewataka kufahamu kuwa haiwezekani kwa mchezo wa soka kuwatumia wachezaji wote kwa wakati mmoja.
Amesema hata waliocheza dhidi ya Vipers SC ni wachezaji halali wa Simba SC na wameipa matokeo timu yake, hivyo amesisitiza kuwa, kama kuna wachezaji hawakutumika dhidi ya Vipers SC ugenini, huwenda wakatumika kwenye michezo mingine itakayowakabili siku za usoni.
“Hawa nitaanza nao kwenye mchezo wa Kombe la Shirikisho ‘ASFC’ dhidi ya African Sports, kisha watamalizia na Vipers SC na Mtibwa Sugar, kumbuka michezo hii yote ipo karibu karibu sana, ni lazima tujiweka vyema kwani kote tuna malengo ya kufanya vizuri.
“Hatuwezi kuichezesha timu nzima katika mchezo mmoja, kwanza tunahitaji kushukuru kumaliza mchezo salama, hao ambao hawakupata nafasi sio kwamba ni wabaya, lakini tuna michezo mingi na muhimu zaidi mbele yetu na ratiba ni ngumu, kwa hiyo tulihitaji kuhifadhi nguvu ya ziada kwa ajili ya michezo hiyo. Kila mchezo una mpango wake, huwenda mkawaona kwenye michezo ijayo,” amesema Robertinho.