Katika Kariakoo Dabi ya Ligi Kuu Bara kati watani wa jadi, Simba na Yanga iliyochezwa Jumamosi iliyopita kwenye Uwanja wa Benjamini Mkapa ilishuhudia Yanga ikiibuka na ushindi wa mabao 2-1.
Kama unavyofahamu mchezo huu unachezwa kwa mbinu nyingi za uwanjani na nje ya uwanja, kelele za mashabiki mitandaoni na uwanjani vinasababisha kuwepo kwa hamasa kubwa mchezoni.
Jicho la kitabibu lilitua kwa wachezaji wawili ambao walipata majeraha ya mapema na kutolewa. Katika soka mchezaji kupata majeraha na kutolewa nje ni kiashiria kuwa yalikuwa majeraha makali.
Katika mchezo huo, Yanga ndio walikuwa wa kwanza kupata pigo katika dakika ya 8 pale beki wake Joyce Lomalisa ambaye alipata majeraha alipotolewa na nafasi yake kuchukuliwa na Nickson Kibabage.
Dakika 3 baadaye Simba nayo ilipata pigo baada ya beki wake wa kati Henock Inonga kuumia na nafasi ya kuchukuliwa na Hussein kazi.
Majeraha haya yalikuwa ya mapema sana kwa wachezaji hawa ambao walianza kucheza kikosi cha kwanza. Huwa ni kawaida kwa mechi kama hizi wachezaji kuwa na hamasa ya juu hatimaye kukamia mchezo.
Mchezo wa soka kama huu wenye upinzani mkali wachezaji wanatumia nguvu nyingi na kasi kubwa. Hata katika kukabana huwa nako ni mapambano na hatimaye kukwatuliwa na kupata majeraha.
Kupata majeraha ya mapema kunaweza kuwa ni ishara ya wachezaji hawa kutumika sana mara kwa mara kutokana na umuhimu wao katika kuisaidia timu kupata mafanikio.
Mchezo wa soka huwa una mambo mengi uwanjani ikiwamo kutumia nguvu sana kucheza hivyo ni kawaida wachezaji kama hawa kupata mrundikano wa vijijeraha vya ndani kwa ndani.
Kitendo cha kutumika sana na nafasi wanazocheza ni kawaida kukumbana na majeraha ya aina ile kwani mabeki nao huweza kupanda na kushambulia.
Kitendo cha kuumia na kushindwa kuendelea na mchezo ni ishara kuwa sio jeraha dogo, huenda likawa jeraha la kati mpaka la kiwango cha juu.
Majeraha ya aina hiyo huenda yakahitaji muda zaidi kuweza kupona kwa wachezaji hawa, haitashangaza kwa majeraha yale kuwa nje kwa muda wa wiki na zaidi. Soka ni mchezo ambao unahusisha kukabana kimwili, pamoja na mbinu mbalimbali zinatumika kupunguza majeraha lakini ni kawaida kutokea majeraha.
SABABU ZA MAJERAHA MAPEMA Mchezaji anaweza kupata majeraha yatokanayo na mchezo katika eneo la miguu yanaweza kutokea kutokana na kukimbia kasi, kugongwa, kujipinda vibaya hasa maeneo ya maungio kama goti na kifundo na kutua vibaya wakati wa kuruka.
Vile vile majeraha yanaweza kutokea wakati maungio na misuli vinapofanya kazi ya ikiwamo kukakamaa, kupata mkazo, kuchanika au kuvutika kupita kiasi.
Katika mchezo kama ule ambao unakuwa na hamasa kubwa kwa wachezaji ni kawaida pia kwa mchezaji pinzani kutumia nguvu kubwa kumkaba mwingine hatimaye kumjeruhi.
Mchezaji kucheza akiwa bado hajapona vizuri, hii inaweza kuwa moja ya sababu kwani kama jeraha halijapona vizuri ni rahisi kupata majeraha tena kwani eneo hili linakuwa sio timamu.
Kutokufanya mazoezi ya kupasha mwili moto na yale ya kunyoosha viungo kabla ya mchezo kuanza. Wataalam wa viungo wanaweza kumpa mchezaji mazoezi hayo lakini asifanye kwa ukamilifu.
Viungo vya mwili visipofanyiwa mazoezi ya kupasha mwili moto huwa ni rahisi kupata majeraha hasa kwa misuli ya mwili.
Wakati wa kucheza mchezaji mwenyewe anaweza kutumia nguvu sana wakati wa kucheza au kukaba, hii inaweza kuchangia kujijeruhi mwenyewe pasipo kuchezewa faulo ikiwamo kujipinda uelekeo hasi.
Kutokana na mchezo wenyewe ulikuwa ni wa upinzani mkali, ni kawaida kufanyiwa faulo mbaya na kupata majeraha.
Mwanasoka anapokuwa anategemewa katika timu anaweza kuamua kudanganya kuwa hana maumivu ya mwili na kucheza au akalazimishwa kucheza akiwa ametumia dawa za maumivu.
Mchezaji anaweza kushawishika au kudanganya ili tu apangwe kucheza kikosi cha kwanza jambo ambalo humpatia bonasi ikiwamo ile anayopewa endapo atafunga, ataanza kikosi cha kwanza au kuibuka na ushindi.
Wanamichezo ambao wako nje ya uwanja kwa kuwa majeruhi hudhani kuwa maumivu yanapopungua tu wamepona na wako fiti kuanza kucheza. Pasipo kufahamu kuwa jeraha bado halijapona vizuri.
Mara yingine misuli ya mwili ya mwanamichezo inapotumika sana huambatana na vimichubuko vya ndani kwa ndani ambavyo uwapo wa maumivu ni kama ombi la mwili kuhitaji kupumzika ili kupona kabisa.
Ingawa ni kawaida pia majeraha ya mapema kutokea bila sababu ya msingi kutokana na mwili wenyewe kushindwa kustahimili shinikizo lililopata.
MAMBO HATARISHI Kutofanya mazoezi kwa ratiba na kutozingatia ushauri wa wataalam wa benchi la ufundi. Mazoezi pia yana kiwango chake, yakifanywa bila kuzingatia sayansi ya mwili huweza kujeruhi mwili.
Kanuni za lishe za wanamichezo zinapokiukwa ikiwamo mchezaji kutozingatia vyakula kama protini na unywaji maji kwa wingi kabla ya mchezo vinaweza kumweka katika hatari ya kupata majeraha kirahisi.
Mchezaji mwenye upungufu wa maji mwilini yuko katika hatari ya kupata tatizo la kubanwa msuli. Upungufu wa protini unachangia misuli kutofanya kazi ya kukunjuka vizuri.
Mchezaji asiyepata muda wa kutosha wa kupumzika na kulala kwa muda wa saa 8 kwa usiku mmoja. Mchezaji asipofanya haya anaharibu utimamu wa mwili kwani mwili unakosa muda kusahihisha na kujijenga.