Shabiki kindakindaki wa Simba Sc, maarufu kama GB 64 amesema kuwa baada ya kifo cha aliyekuwa Mwenyekiti Bodi ya Wakurugenzi wa Klabu hiyo, Zacharia Hans Poppe klabu ilianza kuyumba kuanzia viongozi wake.
GB 64 amesema kuwa, kifo cha kiongozi huyo ambaye alikuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili ya Simba kilisababisha hata mwekezaji wa Timu hiyo, Mohammed Dewji pamoja na aliyekuwa CEO wa Klabu, Barbara Gonzalez kujiondoa kutokana na majungu.
“Ninapata mashaka iwapo kweli Mo Dewji alitoka au aliondolewa Simba. Inawezekana figisu figisu zile, Barbara (CEO wa zamani wa Simba) alitoka kwa sababu gani? Alivyokufa Hans Poppe tu, Barbara naye akaamua akae pembeni.
“Maana yake Hans Poppe alikuwa anawaongoza wote hawa na walikuwa wanamuogopa. Hans Poppe kafa na Simba yake, kaondoka na timu yake.
“Sajili kuanzia hapo zikaanza kuwa mbovu, Barbara alivyoondoka sajili ndio zikaanza kuharibika, tunaletewa kina Pa Omary Jobe, sijui kina Fred Michael na nani, hamna kitu,” amesema shabiki huyo.
Simba kwa sasa inapitia wakati mgumu ikiwa ni miaka mitatu tangu kifo cha Hans Poppe huku hivi karibuni ikiondoshwa kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika na kuondoshwa pia kwenye michuano ya Kombe la Shirikisho Tanzania.