Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Sababu tatu za kumtimua Amrouche Stars hizi hapa

Mwana Fa Amroucheee Sababu tatu za kumtimua Amrouche Stars hizi hapa

Mon, 22 Jan 2024 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Taifa Stars imeshuka uwanjani jana Jumapili kuvaana na Zambia kwenye mechi ya pili ya Kundi F ya Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (Afcon) 2023 na kutoa sare ya bao 1-1 baada ya awali kufungwa 3-0 na Morocco kwenye mchezo wa kwanza, huku siku za kocha mkuu wa timu hiyo, Adel Amrouche zikihesabika.

Imeelezwa kuwa, kocha huyo raia wa Algeria hana muda mrefu kwani upo mpango wa kutimuliwa  baada ya Afcon inayoendelea Ivory Coast ambapo Stars inashiriki kwa mara ya tatu baada ya 1980 na 2019.

Chanzo cha ndani kutoka Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kimelithibitishia gazeti hili kuwa Amrouche atatimuliwa kwa sababu tatu.

Sababu ya kwanza ni uhusiano usiyoridhisha baina yake na baadhi ya viongozi wa TFF, wachezaji na maofisa wa benchi la ufundi jambo ambalo limesababisha kufanyika kwa uamuzi ambao mwingine hauna manufaa kwa timu.

“Ni kocha ambaye amekuwa hashauriki na hana lugha nzuri kwa watu hasa wachezaji, jambo ambalo limewafanya wengi kutokuwa na morali ya kufanya kazi chini yake,” kilisema chanzo.

“Mfano kuna baadhi ya wachezaji wazuri hakuwajumuishwa katika kikosi kinachoshiriki Afcon pasipo sababu ya kueleweka na kuna wengine wapo ndani ya timu amekuwa akiwasema vibaya.”

Vilevile mwenendo usioridhisha wa Stars chini ya Amrouche ni sababu inayoweka shakani kibarua cha kocha huyo mwenye uraia pia wa Ubelgiji hasa katika mechi za hivi karibuni ambazo imecheza katika mashindano.

Mbinu ya kucheza soka la kujilinda ambayo amekuwa akipendelea kuitumia tangu alipoanza kuinoa timu hiyo inaonekana kutowafurahisha wengi na inatajwa kama chanzo cha Stars kupoteza makali ya kutengeneza nafasi na kufunga mabao na pia imekuwa ikiruhusu nyavu zake kutikiswa mara kadhaa.

Tangu Amrouche aanze kuinoa Stars, timu hiyo imefunga mabao manne katika mechi nane ilizocheza za mashindano na kirafiki, huku ikiruhusu manane sawa na wastani wa bao moja katika kila mechi.

Kudhihirisha udhaifu wa Stars katika utengenezaji wa nafasi, kumiliki mpira na kushambulia tangu ilipoanza kunolewa na Amrouche, imekuwa haina takwimu za kuvutia kwenye mechi saba za mashindano.

Takwimu zinaonyesha chini yake timu ya taifa imekuwa na umiliki wa mpira wa wastani wa asilimia 45.3 kwa mchezo, hali inayomaanisha kuwa wapinzani wamekuwa wakimiliki mechi dhidi yake kwa wastani wa asilimia 54.7.

Chini ya kocha huyo pia, Stars imepiga mashuti 12 yaliyolenga lango katika mechi saba ambazo imecheza za mashindano, ikiwa ni wastani wa shuti 1.7 kwa mchezo.

Sababu ya tatu inayochochea kumuweka kikaangoni ni tuhuma ambazo alizitoa kwa Shirikisho la Soka la Morocco kuwa linajihusisha na vitendo vya hujuma kwa timu pinzani kwa kuchagua marefa na fitina za nje ya uwanja.

Amrouche aliyasema hayo alipokuwa akifanya mahojiano na kituo mojawapo cha habari cha kwao Algeria.

“Morocco inaamua kila kitu katika soka la Afrika. Pia wanachagua waamuzi wao.  Tunabaki kuwa watazamaji kwa sababu wanaamua kila kitu. Sitashangaa yakijirudia haya katika mchezo ujao wa Afcon dhidi yao,” alinukuliwa Amrouche aliyeajiriwa Machi, mwaka jana kuchukua nafasi ya Kim Poulsen.

Hata hivyo, siku moja baadaye, Rais wa TFF, Wallace Karia alijitokeza hadharani na kutangaza msimamo wa shirikisho kuwa hausapoti kauli ya kocha huyo na kauli aliyotoa ni yake binafsi.

“Sisi kama TFF hatukubaliani na hiyo kauli.  Shirikisho la Morocco na Tanzania ni marafiki tuko mbali na kauli zake na hatukubali. Tutajua tutafanya nini, tuko kwenye mashindano,” alisema Karia.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live