Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Sababu 5 Simba kichapo kwa Mkapa dhidi ya Raja

Simba Robo Fainali Caf Sababu 5 Simba kichapo kwa Mkapa dhidi ya Raja

Mon, 20 Feb 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Kwa mara ya kwanza Simba imepoteza mechi yake ya kwanza dhidi ya timu za Afrika Kaskazini, maarufu kama 'timu za Waarabu' nchini, ilipofungwa mabao 3-0 dhidi ya Raja Casablanca ya Morocco.

Juzi kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Simba ilichapwa mabao 3-0 dhidi ya timu hiyo, ikiwa ni mechi ya Ligi ya Mabingwa Afrika na kutibua rekodi yao hiyo.

Yalikuwa ni mabao ya Hamza Khabba dakika ya 30, Soufiane Benjdida aliyefunga dakika ya 82 na Ismael Mokadem aliyepachika kwa mkwaju wa penalti dakika ya 86.

Raja Casablanca inakuwa timu ya kwanza ya 'Waarabu,' kuifunga Simba kwenye ardhi ya nyumbani, ikicheza nayo pia kwa mara ya kwanza kwenye historia za timu hizo.

Pia inakuwa timu ya nne kuifunga Simba kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, ambapo Aprili 3, 2011 ilifungwa mabao 3-2 dhidi ya TP Mazembe, Februari 17, 2013 ilifungwa na Recreativo de Libolo ya Angola bao 1-0 na Oktoba 24, 2021 ilichapwa mabao 3-1 dhidi ya Jwaneng Galaxy, huku mechi zote hizo zikiwa ni za Ligi ya Mabingwa Afrika. Dhidi ya Libolo, TP Mazembe na Jwaneng Galaxy zilikuwa ni za mechi za Raundi ya Kwanza, huku ya juzi ilikuwa ni hatua ya makundi.

Hata hivyo, bado Simba ndiyo timu iliyoshinda mara nyingi zaidi kwenye uwanja huo kwenye mechi za kimataifa kuliko timu yoyote ile nchini.

Kwa nini Simba ilipoteza mechi yake ya pili kwenye Ligi ya Mabingwa? Mwandishi wa makala haya anaainisha jinsi mechi hiyo ilivyokuwa...

Haikuisoma vema Raja Casablanca Ukiiangalia mechi hiyo, sidhani kama benchi la ufundi la Simba liliwaoma vema wapinzani wao. Badala yake ilicheza inavyocheza siku zote. Hawakuangalia ni wachezaji gani hatari ambao wanaweza kusambaza mipira kwao na kuwa hatari.

Nadhani ilifikiria kuwa timu za Waarabu huwa na tabia ya kuzuia sana wanapocheza ugenini. Lakini haikuwa hivyo kwa asilimia zote.

Raja Casablanca iliikuwa inaisubiri wenzao washambulie, halafu kwa sababu walikuwa na uwezo wa kuzuia na kukaa na mpira wapandisha mashambulizi kwa haraka kwenda mbele na mpangilio maalum, ambayo yalikuwa ya hatari sana.

Kuna wakati baada ya kuona wamewakamata Simba, waliamua kutawanyika na kusakata kandanda bila kukaa nyuma, wakionyesha ufundi waliojaliwa nao miguuni.

Simba sasa imezoeleka Wakati Simba inaonekana haikuisoma Raja Casablanca, uwezo wao kitimu, kimbinu na mchezaji mmoja mmoja, kinyume chake ni kwanza wapinzani wao walionekana kufahamu wanakwenda kucheza na timu ya aina gani.

Ukiwaangalia viungo na mabeki wa timu hiyo, walionekana kudili zaidi na mipira ya kupenyezwa kati. Ubora wa Simba siku zote haupo kwenye kupiga krosi na kufunga. Huwa wanapitia kati kufunga mabao yao. Mabeki wa viungo wa timu hiyo walionekana kucheza kwa maelekezo na kuzuia pasi zote mpenyezo.

Kama vile haitoshi, inaonekana waliwafahamu Clatous Chama na Saido Ntibazonkiza kuwa ndiyo wapishi wa timu hiyo, ndiyo maana hawakuwapa kabisa nafasi hata ya kukaa na mpira, au kuwaacha wafikiri.

Wanapogusa mpira tayari kuna mtu ambaye alikuwa anafanya kazi ya kumghasi ili asilete madhara. Ndiyo maana kwenye mechi ya juzi Chama na Saido ukiangalia kwa haraka haraka ni kama hawakuwa kwenye viwango vyao, la hasha.

Hawakuachiwa hata sekunde chake za kukokota mpira kwenye eneo la hatari na kufikiri cha kufanya. Hiyo peke yake iliinyima Simba kupata nafasi nyingi ambazo huwa inazitengeneza kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa.

Ukweli kwamba Simba ina wachezaji wengi ambao wamecheza misimu mitano Ligi ya Mabingwa, hivyo kusomeka ni rahisi sana na imeshazoeleka na kutengenezewa mpango mkakati wa kudhibitiwa.

Kutochezesha mastraika wawili Kwa sababu Simba ilihitaji zaidi ushindi, makocha walipaswa kuweka mastraika wawili ili kuweza kufanya mashambulizi mengi langoni mwa wapinzani wao.

Kuwapo kwa Bocco tu mbele, huku akiwa amebanwa na mabeki wawili warefu, hakukuwa na tija yoyote kwa wenyeji, badala yake walikuwa wakifanya mashambulizi kwa kubahatisha zaidi, tofauti na wapinzani wao ambao walishambulia kwa mpangilio na ya hatari.

Kuna wakati Shomari Kapombe alipokuwa anakwenda kupiga krosi, mbele kulikuwa na Bocco tu, halafu nyuma yake hakukuwa na mtu yeyote.

Katikati ya kipindi cha pili ambapo Jean Baleke na Mosses Phiri walipokuwa ndani ya uwanja, ulikuwa unaona sasa Simba yenye uhai na ndicho kipindi yalipigwa mashuti yenye kulenga lango, yote yakipigwa na Mzambia Phiri.

Nadhani huenda hali ingekuwa tofauti kama wangeanza, au Bocco angekuwa na msaidizi tangu mwanzo.

Raja Casablaca ilicheza kikubwa Kuna funzo ambalo inabidi timu za Tanzania ilipata kwenye mechi hiyo, kwani pamoja na kwamba ilionekana wachezaji wa Raja Casablanca wana uwezo mkubwa wa kuchezea mpira, lakini hawakuwa na mbwembwe nyingi.

Badala yake walikuwa wanacheza soka la moja kwa moja ili kupata ushindi tu na si vinginevyo. Soka la maelekezo na si la kufurahisha jukwaa.

Hawakufanya mashambulizi mengi sana langoni mwa Simba, lakini kila shambulizi lao lilikuwa la hatari mno. Mawinga wao hawakupiga krosi wanapofika kwenye mstari, walikuwa wanaangalia nani yupo eneo sahihi.

Zilikuwa ni krosi pasi. Wachezaji wao walikuwa wanagawanyika wanapoingia kwenye eneo la hatari. Wengine wanakuwa langoni na baadhi nyuma, mbali kidogo ya lango. Wale wanaokuwa nje kidogo ya lango ndiyo huwa hatari zaidi.

Viwango vya timu vimeamua mechi Hata kama mechi ya juzi ingechezwa mpaka asubuhi ya jana, sidhani kama Simba ingeweza kurudisha mabao hayo. Labda kuongezwa. Ilionekana kabisa utofauti wa viwango vya wachezaji wa timu hizi mbili.

Wachezaji mmoja mmoja wa Raja Casablanca walikuwa na viwango vikubwa zaidi tofauti na Simba. Kwa bahati nzuri kwao, hata kiufundi na maelekezo kutoka kwa kocha wao walikuwa bora zaidi.

Mechi iliamuliwa zaidi na viwango vya wachezaji na ukubwa wa timu. Ukiiangalia Raja Casablanca ni timu yenye kiwango cha kuweza kufika hata fainali ya Ligi ya Mabingwa msimu huu.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live