Chelsea inajiandaa kufanya usajili mwingine mkubwa mwishoni mwa msimu huu.
Na kutokana na hilo, kuna mastaa saba wana miezi miwili ya kuamua hatima, kama watabaki au wataondoka.
Tajiri mmiliki wa timu, bilionea Todd Boehly ameshatumia pesa nyingi kwenye usajili, zaidi ya Pauni 1 bilioni tangu aliponunua timu hiyo mwaka 2022. Hata hivyo, mambo hayaendi vizuri ndani ya uwanja kwa timu hiyo. Mauricio Pochettino ni kocha wa tano kuinoa Chelsea katika kipindi kifupi tu chini ya tajiri Boehly baada ya Thomas Tuchel, Graham Potter, Bruno Saltor na Frank Lampard.
Kutokana na hilo, bila shaka, tajiri Boehly atalazimika kuingia sokoni dirisha lijalo kuziba maeneo muhimu. Anahitaji straika ambapo anayetajwa ni mkali wa Brentford, Ivan Toney.
Chelsea inahitaji pia beki wa kati na beki wa kushoto, wambamba na winga mwenye ujuzi mwingine, anasakwa pia atue haraka huko Stamford Bridge.
Lakini, Chelsea tayari ipo kwenye mstari wa kubanwa na kanuni ya Financial Fair Play, ambayo itawalazimisha kama wanataka kusajili nyota wapya, basi ni lazima wauze mastaa.
Tajiri Boehly anaamini kipa Kepa Arrizabalaga na straika Romelu Lukaku wote wataondoka kwenye dirisha lijalo.
Kinachoelezwa wachezaji saba ambao wamebakiza miezi miwili ya kuamua hatima kubaki au la, ni Raheem Sterling, , Conor Gallagher, Robert Sanchez, Marc Cucurella, Trevoh Chalobah, Armando Broja na Thiago Silva.