Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Saa ya Rudiger ni kufuru

Saa Rudiger Saa ya Rudiger ni kufuru

Fri, 7 Jun 2024 Chanzo: Mwanaspoti

Beki wa Real Madrid, Antonio Rudiger ameshangilia taji la Ligi ya Mabingwa Ulaya kwa kujipongeza na saa ya Pauni 1.4 milioni sawa na zaidi ya Sh 4.6B.

Miamba hiyo ya Hispania iliweka rekodi ya kunyakua taji hilo la Ulaya kwa mara ya 15 baada ya kuwachapa Borussia Dortmund 2-0 katika mchezo wa fainali uliofanyika uwanjani Wembley, Juni Mosi.

Rudiger, 31, ambaye alishinda taji lake la kwanza la Ligi ya Mabingwa Ulaya akiwa na Chelsea mwaka 2021, alikuwa na mchango mkubwa kwenye beki ya Los Blancos katika msako wao wa taji hilo la 15 la Ulaya.

Alionekana kuwa mwenye furaha akiwa amebeba taji hilo. Lakini, watu na macho yao waliona saa aliyokuwa amevaa beki huyo. Kwa mujibu wa Insaneluxurylife, saa hiyo ni aina ya Patek Philippe Nautilus 5711/1A-018. Na kinachoelezwa, saa hizo zimetengenezwa 170 tu.

Kutokana na uchache wake sokoni, inaripotiwa kwamba saa aliyokuwa amevaa Rudiger, thamani yake ni Pauni 1.4 milioni.

Rudiger, ambaye ameitumikia Ujerumani mara 68 alijiunga na Real Madrid kwa uhamisho wa bure mwaka 2022 baada ya mkataba wake kufika ukomo huko Chelsea. Tayari ameshaichezea Los Blancos zaidi ya mara 100 akiwa chini ya kocha Carlo Ancelotti.

Ameshinda mataji kibao, ikiwamo La Liga, Copa del Rey, Spanish Super Cup na Klabu Bingwa Dunia na atakuwapo kwenye fainali za Euro 2024, zitakazoanza Juni 14 huko kwenye ardhi ya kwao Ujerumani.

Chanzo: Mwanaspoti