Kocha mkuu wa Yanga, Miguel Gamondi hatanii kabisa kwani juzi Jumatatu jioni aliwapigisha tizi kali mastaa katika Ugukwe wa Coco kwa saa 1, ili kuhakikisha miili inakuwa fiti kabla ya mchezo wa Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya El Mereikh ya Sudan.
Hii ni mara ya kwanza mastaa wa Yanga kufanya mazoezi ya wazi huku wakishuhudiwa na mashabiki tangu msimu huu wa Ligi Kuu Bara uliopoanza.
Gamondi aliwaongoza mastaa wa kikosi hicho ambao hawajaitwa katika timu za taifa na alionyesha hatanii kuhakikisha wanafuata programu zitakazokuwa zinatolewa bila kufanya mzaha wowote.
WATUA NA NDINGA
Mastaa walianza kuwasili Coco saa 9:30 alasiri wakiwa na magari yao na wa kwanza alikuwa Jesus Moloko akiwa na gari lake aina ya Toyoto Mark X.
Mchezaji wa pili alikuwa Kennedy Musonda aliyeongozana na beki Gift Fred wakiwa na gari aina ya Hyundai Veloster likiwa na namba za usajili za Zambia.
Mastaa wengine waliendelea kuwasili Zawadi Mauya akiwa na gari aina ya Mark X nyeupe, Kibwana Shomari BMW, Abutwalib Mshery Crown nyeupe na Farid Mussa akiwa na Harrier nyeusi.
Mastaa hao walikuwa hawana mambo mengi kwani walibadili nguo za nyumbani haraka kisha wakavaa jezi na kusubiri programu za kocha.
Kocha Gamondi ambaye alifika na gari aina ya Toyota Vanguard alizungumza na wachezaji mawili matatu kisha ilipofika saa 10:37 aliwataka wote kushuka ufukweni na kuanza rasmi mazoezi.
WAKIMBIZWA DK 15
Gamondi alizungumza nao kidogo eneo la Uwanja wa Beach Soccer kisha aliwashusha chini na kuanza mazoezi.
Kocha huyo aliwataka wachezaji hao kukimbia pembezoni mwa ufukwe na alitumia dakika 15 kuamsha misuli ya mastaa wake huku akiwa anafuatilia kwa karibu.
Wakati wachezaji wake wanakimbia, bosi huyo wa benchi la ufundi alikuwa anawafuata kwa nyuma huku akitembea akiangalia kusiwe na yoyote ambaye anatembea.
Mastaa hao walikimbia umbali mrefu wakiwa huku mashabiki mbalimbali wakiwaangalia sambamba na wale ambao walitaka kufanya mazoezi ya kukimbia wakijiunga nao kwa pembeni.
WAPIGISHWA KONI
Wachezaji wengi unapofika wakati wa zoezi la koni hushika viuno, ndivyo ilivyokuwa kwa Yanga kwani baada ya kutoka kukimbia walikuta uwanja wa soka la ufukweni ukiwa umepangwa koni za kutosha.
Katika mazoezi hayo kocha wa viungo, Taibi Lagrouni ndiye aliyekuwa anasimamia kuhakikisha kila mchezaji aliyekuwepo kufanya mazoezi yote aliyoyatoa.
Zoezi la koni, kocha Lagrouni alianza kwa kuwataka wakimbie tena na pia alikuwa anachanganya na wachezaji hao kuchezea mpira kwa kupiga danadana na kuruka vichwa.
Tizi hilo lilidumu kwa dakika 26 ambapo kila mchezaji pia ilikuwa lazima acheze mpira wa kichwa pale wanaporushiana kwa juu na benchi lote la ufundi lilisimamia.
WEPESI, STAMINA
Baada ya kufanya zoezi la koni, Gamondi na Lagrouni waligeukia zoezi lingine la kuwapa stamina wachezaji na spidi, na kuwataka wakimbie tena kwenye uwanja huo na lilitumia dakika nne za nguvu bila kusimama.
Wachezaji hawakupumzika kwani wakikimbia upande mmoja, basi walitakiwa warudi tena upande wa pili ambao walitokea kiasi cha kuwafanya waonekane kuchoka.
Katika mikimbio hiyo Skudu Makudubela, Salum Abubakari (Sure Boy) na Maxi Nzengeli walikuwa mstari wa mbele kuwaongoza wenzao.
MASTAA HOI
Gamondi alimaliza mazoezi saa 11:34 jioni, lakini mastaa wengi walionekana kuwa hoi huku wengine wakikaa chini.
Kipa Abuutwalib Mshery na Pacome Zouazoua walionekana kuwa hoi sambamba na wachezaji wa chini ya miaka 20 ambao walichukuliwa kufanya mazoezi katika timu ya wakubwa kutokana na mastaa wengine kuwa kwenye mashindano ya timu za taifa.
Wachezaji waliokuwa katika mazoezi hayo ni Mshery, Yao Attohoula, Farid, Sure Boy, Skudu, Hafidh Konkon, Chrispin Ngushi na Kibwana.
Wengine ni Musonda, Denis Nkane, Gift, Moloko, Pacome na Mauya.
HUYU HAPA GAMONDI
Baada ya mazoezi kumalizika, kocha Gamondi alisema sababu kubwa ya mazoezi hayo ilikuwa kuwatengenezea wepesi wachezaji pamoja na utimamu wa miili.
“Tumecheza mechi nyingi mfululizo sambamba na kukaa sehemu moja, na ndio maana tumekuja hapa kwa lengo la kuwabadilishia wachezaji mazoezi na pia kuwapa wepesi na utimamu wa miili,” alisema kocha huyo aliyetua Jangwani msimu huu.
“Mara zote ushindi huwa unaanzia hapa mazoezini. Nina furaha kuona tukifanya mazoezi huku watu wakiwa wapo pembeni wanatuangalia.”