Bado haijajulikana wazi kama kocha mkuu wa Senegal, Aliou Cisse atakiongoza kikosi hicho kwenye mechi ya hatua ya 16 bora ya Kombe la Dunia dhidi ya England leo baada ya taarifa kuwa anaumwa.
Cisse hakuwepo kwenye mkutano na waandishi wa habari kabla ya mechi ya mtoano, huku msaidizi wake, Regis Bogaert, akichukua majukumu ya kuzungumza na vyombo vya habari.
Bogaert alisema Cisse amekuwa mgonjwa kwa siku kadhaa, na hajawa sehemu ya mazoezi kuelekea mchezo wa leo.
“Amekuwa mgonjwa kwa siku kadhaa sasa,” alisema Bogaert. “Alituruhusu tuchukue jukumu la mazoezi jana, ni wazi na maagizo yake kwa wachezaji.” aliongeza Bogaert.
“Natumai kesho ataweza kuja na kuwa kwenye benchi na wachezaji lakini tuna uhakika saa 10 jioni atakuwa na timu ninaweza kuthibitisha kuwa ni mgonjwa na ana joto kidogo, ndiyo maana tunapaswa kuwa makini na hali yake.”alisema Bogaert.
Cisse ambaye alichezea klabu za Paris Saint-Germain, Portsmouth na Birmingham kama mchezaji, ameleta mafanikio makubwa sana tangu alipoteuliwa kuwa meneja wa Senegal mwaka 2015.