Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

SPOTIDOKTA: Uungwana unapunguza majeraha mabaya

Inonga Jeraha Haji Uungwana unapunguza majeraha mabaya

Sun, 1 Oct 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Katika mchezo wa Ligi Kuu Bara uliochezwa kwenye Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam Alhamisi iliyopita ilishuhudiwa beki wa Simba, Henock Inonga akichezewa rafu mbaAya na mshambuliaji wa soka wa Coastal Union, Haji Ugando.

Ilikuwa sio mchezo wa kiungwana, kwani rafu hiyo ilisababisha Inonga kutolewa nje katika dakika ya 20 ya mchezo kwa machela na kuwahishwa katika huduma za afya kwa kutumia gari la wagonjwa.

Mwamuzi wa mchezo huu alimpa kadi nyekundu mshambuliaji huyo wa Coastal na hivyo kuilazimu klabu hiyo kutoka mkoani Tanga kucheza pungufu na hatimaye kuambulia kipigo cha mabao 3-0.

Ilikuwa ni rafu mbaya ambayo ilimshtua kila mmoja ambaye alikuwa anaitazama mechi ile wengi wakiwa na hofu kubwa pengine ni jeraha linalohusisha kuvunjika mguu.

Lakini habari nzuri zilizotolewa hapo baadaye na msemaji wa klabu ya Simba, Ahmed Ally ni kuwa beki hiyo kisiki hakuvunjika mguu bali alipata kidonda ambacho kilimfanya ashonwe nyuzi kadhaa katika Hospitali ya Temeke.

Ukiacha mbinu nyingine zinazotumika kupunguza majeraha ya soka lakini pia kuna uungwana wa kimchezo kwa lugha ya Kiingereza kama ilivyo maarufu ni fair play ni moja ya nyenzo muhimu kulinda utimamu wa mchezaji.

Mchezaji anapokuwa muungwana na akashikamana na aina hiyo ya uchezaji inasaidia kupunguza majeraha mabaya yatokanayo na hekaheka za soka uwanjani.

Kwani kuna tofauti ya mchezaji mwenye kucheza na uungwana na yule ambaye si muungwana. Kuna wakati katika soka inamlazimu mwanasoka kufanya faulu ili kuzuia mashambulizi au kufungwa.

Timu yenye wachezaji waungwana hata kama watatumia mbinu za kufanya faulo basi watafanya hivyo kwa umakini mkubwa ili kutowaumiza wachezaji wa timu pinzani.

Ni matukio ambaye huwezi kumhukumu mchezaji moja kwa moja kuwa amedhamiria kufanya hivyo kwani mchezo wa soka wowote ule unabeba hisia na huku kukiwa na kukamiana ili kushinda.

Ugando mwenyewe alionyesha kuwa muungwana mara baada ya kitendo hicho kwani alionekana kujutia hasa pale alipomwona Inonga akigaragara kwa maumivu makali hapo chini.

Hata hivyo, katika soka matukio ya rafu kama hizo zenye kuashiria ukosefu wa uungwana katika soka sio mara ya kwanza kwani hata Inonga mwenyewe aliwahi kufanya rafu ya namna hiyo.

Mtakumbuka mwaka jana mwezi wa nane katika mechi ya watani wa Jadi Simba na Yanga, Inonga alimfanyia rafu mbaya isiyo ya kiungwana kiungo wa Yanga Salum Abubakar.

Kwa kuwa si matukio ambayo yanatokea mara kwa mara katika Ligi Kuu ya soka hapa nchini hivyo inawezakana ni matukio yaliyotokea kwa bahati mbaya tu.

Elimu kuhusu FIFA fair play katika soka haiepukiki katika klabu za soka duniani kwani ndio nyenzo rahisi inayozuia majeraha mabaya kutokea katika soka.

Hivyo ni muhimu wachezaji wakapewa elimu ya mara kwa mara ya uungwana mchezoni ili kupunguza hatari ya wanasoka kupata majeraha mabaya ya soka.

Uungwana wa kimchezo ndio unapunguza wachezaji kucheza kwa jazba kwani hata pale mpinzani anapokasirika au kuudhiwa na rafu aliyochezewa uungwana ndio unarudisha imani kwa mtendewa rafu.

Endapo uungwana ungelikosekana uwanjani ina maana majeraha yangekuwa ni mengi maana mchezaji asiye muungwana angebeba hasira ambayo ingemfanya kucheza faulo ya kulipa kisasi.

TIBA YA KIAKILI

Pale unapomfanyia madhambi kwa bahati mbaya kwa mchezaji mpinzani kitendo cha kumwonyesha uungwana aidha kwa kumwomba msamaha, kumpa pole au kumsaidia kupata huduma ya kwanza kwa haraka pale eneo la tukio inaondoa hasira kutoka kwa mjeruhiwa.

Hii inasababisha mchezaji mjeruhiwa kuja na hisia chanya ikiwamo kufurahi hata kama kaumia. Uwepo wa hisia chanya mwilini huwa ni faida kubwa kwa afya ya mwili na akili.

Mchezaji ambaye ametendewa ndivyo sivyo pasipo uungwana, huweza kumfanya kubeba hofu, wasiwasi, chuki au jazba. Mambo haya huleta hisia hasi kwa mwili hivyo kuteteresha afya ya akili.

Hii ikitokea inaweza kuwa chanzo cha mchezaji kutopona kwa wakati, kukosa umakini katika uchezaji wake au ufanyaji kazi zake kila siku.

UUNGWANA HUOKOA MAISHA

Mtakumbuka katika fainali za Euro 2020 timu ya soka ya Taifa ya Denmark na madaktari wake walishinda tuzo ya Fair Play 2021 hii ni kutokana na jitihada za kuokoa maisha ya Christian Eriksen alipoanguka ghafla uwanjani.

Hapa tunapata somo kubwa kuwa hata kama lengo la timu ni kushinda kwa namna yoyote ile lakini linapokuja suala la uhai au afya ya mtu lengo hili huwekwa pembeni.

Tukio jingine maarufu la kiungwana ni lile la mchezaji wa soka wa West Ham enzi hizo, Paolo Di Canio dhidi ya Everton katika mchezo wa Ligi Kuu England.

Kipa wa Everton alivutika pembeni ili kupokonya mpira lakini akaumia wakati akifanya hivyo. Mchezaji wa West Ham aliunasa mpira kirahisi na kutoa pasi ya moja kwa moja.

Di Canio alikuwa katika nafasi nzuri alipokea pasi hiyo akiwa yeye na lango lililowazi lakini badala ya kufunga yeye akautoa mpira nje ili kutoa nafasi kipa wa Everton apate huduma ya kwanza.

Huu ulikuwa ni uungwana wa kiwango cha juu katika soka hivyo kuchangia Di canio kupata tuzo ya FIFA ya Fair Play Award mwaka 2001.

CHUKUA HII

Elimu ya Uungwana wa kimchezo katika soka inapaswa kuendelea kutolewa mara kwa mara katika klabu na shule za kufundishia soka ili kujenga kizazi bora cha soka hatimaye kupunguza majeraha mabaya.

Mchezaji wa soka ashikamane na uungwana wa kimchezo wakati wote anapocheza soka ili kujizuia kucheza faulo zisizo za kiungwana.

Chanzo: Mwanaspoti