Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

SPOTI DOKTA: Sababu za vifo vya wanahabari ni hizi

Spoti Dokta Pic Sababu za vifo vya wanahabari ni hizi

Thu, 15 Dec 2022 Chanzo: Mwanaspoti

Mashindano ya Kombe la Dunia 2022 Qatar yakiwa sasa yanaelekea fainali hapo Jumapili tasnia ya habari imepatwa na simanzi kutokana na vifo vya ghafla vya wanahabari wawili wa michezo.

Wa kwanza alikuwa Grant Wahl (pichani) aliyefariki kwa kupata la shambulio la moyo kitabibu heart attack akiwa kwenye Uwanja wa Lusail akiripoti mchezo wa robo fainali wa Uholanzi dhidi ya Argentina.

Grant aliyekuwa akifanya kazi CBS, alifahamika zaidi nchini Qatar baada ya kuingia katika utata na vyombo vya usalama mara baada ya kuvaa fulana inayounga mkono mapenzi ya jinsia moja.

Mara baada ya kifo hiki zikapita saa 48 mwandishji wa pili ajulikanaye kama Khalid al- Misslam wa kituo cha Al Kass alifariki huku sababu za kifo hazijajulikana.

Matukio haya mawili yote yanajulikana kama vifo vya ghafla. Mara nyingi sababu ya vifo hivi vinahusishwa na matatizo ya moyo kama ilivyokuwa kwa Grant aliyepatwa na shambulizi la moyo.

Mara kwa mara maneno ya cardiac arrest na heart attack utayasikia panapotokea vifo vya ghafla kwani ndio chanzo cha matatizo haya. Leo tutapa ufahamu kuhusu matatizo haya mawili.

Shambulizi la Moyo vs Moyo kusimama

Cardiac Arrest kwa lugha rahisi ni moyo kusimama ghafla kufanya kazi au mshtuko wa moyo, ni tatizo linalotokea katika moyo chanzo kikiwa ni hitilafu ya umeme wa moyo.

Kwa kawaida tatizo likitokea utendaji wa moyo wa kutoa mapigo kusukuma damu huenda mrama na kusimama ghafla.

Mshtuko wa moyo hutokea bila kuwa na dalili au viashiria vya kuonya, mara nyingi huchochewa na matatizo ya mfumo wa umeme wa moyo baada ya kupata hitilafu na kusababisha mapigo yasiyo na mpangilio.

Hii ikijitokeza moyo huweza kusimama na kushindwa kusukuma damu maeneo nyeti ikiwamo ubongo, mapafu na ogani nyingine.

Tatizo hili likitokea muathirika huweza kupoteza fahamu huku unepaji wa mishipa ya damu hupotea na ndani ya dakika chache muathirika anaweza kupoteza maisha.

Wakati heart attack tatizo alilopata Grant ni shambulizi la moyo ikimaanisha ni yale matatizo ya damu yanayohusiana na utawanyaji au upelekeaji wa damu katika moyo kupata kizuizi.

Hivyo utaona kuwa shambulizi la moyo ni hitilafu ya mzunguko wa damu na moyo kusimama ni hitilafu ya umeme wa moyo.

Baadhi ya watu huweza kudhani matatizo haya yako sawa lakini ukweli wa kitabibu ni kuwa yanatofautiana ingawa yote ni matatizo yanayotokea katika moyo na kusababisha vifo vya ghafla.

Heart attack hutokea pale damu inayopitishwa katika mishipa ya damu ya Ateri kuwa na kizuizi hivyo misuli ya moyo kukosa damu yenye oksijeni.

Endapo kizuizi au mkwamo katika mishipa hiyo haitaondolewa mapema kifo cha ghafla huweza kutokea. Taarifa iliyotolewa ni kuwa Grant alikuwa na tatizo la shinikizo la damu kwa muda mrefu.

Uhusiano wa matatizo haya mawili ni kutokana na kusimama au mstuko wa moyo hutokea mara baada ya kutokea kwa shambulizi au wakati wa uuguzi wa shambulizi la moyo.

Vile vile mara nyingi shambulizi la moyo huwa halisababishi kutokea kwa mstuko wa moyo. Mara nyingi mstuko wa moyo ni tatizo ambalo linaweza kutokea na kusahihishwa na kurudi katika hali ya kawaida.

Nchi zilizoendelea ambazo ndizo zenye idadi kubwa ya watu wanaopata mstuko wa moyo hutumia huduma ya usingaji wa kifua na kuongezea hewa ya oksijeni ili kuwaokoa wanaopata tatizo hili.

Dalili za heart attack zinaweza kuibuka ghafla na zikawa kali, ingawa mara kwa mara huanza taratibu na kuwa kali kadiri saa, siku au wiki zinavyosogea kabla ya kutokea.

Ni moja ya matatizo ya kiafya yasiyoambukiza yanayosababisha mara kwa mara vifo vya ghafla kwa watu wazima hasa umri wa miaka 45 na kuendelea. Hapa unapata picha kwa umri huu tayari Grandt Wahl alikuwa ana kihatarishi kwani umri wake ni miaka 49.

Ni kawaida ikatokea sababu ya kifo cha ghafla isijulikane moja kwa moja lakini asilimia kubwa huchangiwa na matatizo ya moyo hasa shambulizi la moyo.

Tumeona kifo cha mwanahabari wa pili aliyefariki ghafla bado sababu ya kifo chake haijajulikana ingawa yapo matatizo mengine ya kiafya yanayohusishwa na kifo cha ghafla ikiwamo vinavyotokea tukiwa usingizini.

Chanzo cha vifo vya ghafla ni hivi

Moyo ndiyo ogani kubwa inayohusika na usukumaji wa damu mwilini, magonjwa au matatizo yake huwa ni ya kimya kimya na ndiyo yanayoongoza kwa kusababisha vifo vya ghafla duniani.

Maradhi ya moyo huwa yanapiga hatua kimya kimya pasipo kujijua kwa anayeugua, mara nyingi watu hugundulika wakiwa na matatizo ya moyo baada ya kufanyiwa uchunguzi wa jumla.

Mara nyingi kuharibika kwa mishipa ya damu katika moyo ni sababu kubwa inayosababisha matatizo mbalimbali ikiwamo mapigo ya moyo kwenda mrama, misuli ya moyo kufa na shambulizi la moyo.

Mishipa ya damu ya moyo ya Ateri ikiharibika husababisha misuli ya moyo kukosa damu kabisa au kupata kiasi kidogo sana. Uharibifu hutokana na mgando wa tando ya mafuta katika kuta za mishipa hii.

Hali hii husababisha misuli kushindwa kufanya kazi ya kusukuma damu kwa ufanisi wa kawaida, hupiga mapigo bila mpangilio na siku yoyote isiyojulikana ghafla moyo husimama.

Matatizo mengine yanayoweza kusababisha vifo vya ghafla ni kama vile misuli ya moyo kututumka, moyo kushindwa kufanya kazi, maumbile yasiyo yakawaida ya mishipa ya damu, hitilafu au uambukizi wa valve za moyo na kuzaliwa na moyo wenye hitilafu na wingi wa lehumu mbaya.

Pia matatizo ya mfumo wa umeme wa moyo na vituo vyake, upungufu wa madini kama vile magnesium, kuzaliwa na moyo mkubwa na hitilafu ya mapigo ya moyo.

Mambo mengine ambayo hayatokani na maradhi ya moyo ni kama vile sumu, mrundikano wa takasumu, matatizo ya mfumo wa hewa, mkwamo katika njia ya hewa, kuvuta hewa chafu na ajali katika ogani.

Vihatarishi ni pamoja na shinikizo la juu la damu kama ilivyokuwa kwa Grant, kiwango kikubwa cha lehemu, unene, kisukari, uvutaji tumbaku na kutofanya mazoezi, umri mkubwa 45+ na historia ya familia.

Dalili zake ni maumivu ya ghafla ya kifua, mapigo ya moyo yasiyo ya kawaida, kuchoka kirahisi, uchovu, pumzi kukatika, kuona giza, kuishiwa nguvu, kuzimia, kichefuchefu, kutokwa jasho na kukosa usingizi.

Kama ilivyokuwa kwa Grant muhimu walio jirani kutoa mwito wa msaada haraka ili kuokoa maisha ya yule aliyepata tatizo hili.

Matatizo mengi yanayosababisha shambulizi la moyo yanaweza kudhibitiwa endapo utafika mapema katika huduma za afya.

Chanzo: Mwanaspoti