Leo ni kilele cha Siku ya Mwanamke Duniani, yapo mengi yaliofanywa na baadhi yao kwenye michezo mbalimbali na wamefanyika mfano wa kuigwa na wengine.
Wapo wanamichezo kibao wa kike wanaofanya vizuri kwenye nafasi za uongozi kuanzia Rais wa Gofu Wanawake, Queen Seraki, Dk Devota Marwa wa Chaneta, Neema Msitha wa BMT na wengineo, lakini kuna wanamichezo wanaoliamsha iwe ni kwenye michezo ya soka, ngumi na mingine ambao siku hii haiwezi kupita bila kuwapa kifyagio.
Mwanaspoti linakuchambulia baadhi ya wanawake kutoka kwenye michezo mbalimbali, walioonyesha udhubutu na sasa wanatazamwa kama majasiri kwenye sekta zao, japo kuna wengine wanaokimbiza pia katika fani hizo sambamba na wanaume kuonyesha kwamba dunia ya sasa mambo ni bambam.
JONESIA RUKYAA-MWAMUZI
Mwamuzi Jonesia Rukyaa ni kati ya wanawake wa shoka, umahiri wake wa kazi, ndio unaowapa imani Chama cha Waamuzi Tanzania kumpanga achezeshe mechi ngumu kama za dabi za Kariakoo (Simba na Yanga).
Mwanadada huyo ni kati ya waamuzi bora wa Ligi Kuu, akielezwa anawajulia sana wachezaji vichwa ngumu ambao wanapomuona uwanjani, hutulia na kuiacha miguu yao ifanye kazi badala ya kubisha na naye kwani huwa hataniwi.
PENDO NJAU -NGUMI
Ukitaja wanawake ambao wanaheshima kubwa kwenye ngumi, huwezi kuliacha jina la Pendo Njau, amecheza na sasa ni mwamuzi wa mchezo huo.
Baadhi ya mapambano makubwa aliyochezesha ni la bondia Ibrahim Mgender ‘Ibrah Class’ alilomtandika kwa Knockout (KO) raundi tisa Mmexico Gustavo Pina Melgar ‘Alan Pina’ lenye uzito wa Super Feather.
“Kila kazi inahitaji nidhamu na kujituma, ndipo unapoweza kuona ndoto zikitimia, kwa sasa naona mabinti wengi wameingia kwenye ngumi na wanapambana, tofauti na mwanzo ambapo ulionekana ni mchezo wa kiume zaidi,” anasema Njau.
EDINA LEMA - SOKA
Huyu ni Kocha Msaidizi wa Biashara United inayoshiriki Ligi ya Championship, Edina Lema ni kati ya wanawake wanaofanya vizuri kwenye soka, kabla ya hapo ndiye alikuwa kocha mkuu wa kwanza kwenye Ligi Kuu ya Wanawake (WPL) wa timu ya Yanga Princess.
Kwa sasa Biashara United ipo nafasi ya pili, pointi 49 kwenye mechi 23, ikishinda mechi tano kati ya saba,itakuwa imepanda Ligi Kuu Bara, hivyo Edina anaweza akaingia kwenye rekodi ya kuisaidia timu hiyo kupanda.
Edina anasema; “Natamani kufanya mambo makubwa kwenye soka, yatakayowapa nguvu mabinti kuamini, hakuna kinachoweza kushindikana kama wana nia ya kuzifanya ndoto zao kufika mbali.”
MATTYY MSETI-KOCHA
Aliyekuwa Kocha Msaidizi wa Simba Queens, Sophia Mseti ‘Matty Diola’ kwa sasa anafundisha moja ya academy kubwa nchini Dubai ambayo ina mchanganyiko wa wachezaji kutoka mataifa makubwa ya kisoka duniani.
Anatajwa kama mmoja ya wakocha wa kike wenye misimamo ndio maana haikuwa ajabu alipoamua kuachana na Simba Queens ili kufanya yake nje ya klabu hiyo, baada ya kuona mambo hayapo upande wake lichja ya taaluma ya ukocha aliyonayo iliyompa heshima kubwa kwa mashabiki wanaomfuatilia.
ANGEL EATON-GOFU
Kwa sasa ndiye mchezaji wa kike pekee ambaye ametani kucheza pro, kabla ya kutani alichukua mataji mengi kwenye mashindano ya gofu ya ridhaa.
Utasema nini kuhusu mwanadada huyo kwenye mchezo huo, hata kama kuna wengine wanaokula naye sahani moja kama kina Madina Ally, lakini Angel ni kiboko yao kwenye anga hizo.
REHEMA SELEMAN-TENISI
Rehema Seleman kwa sasa ndiye mchezaji namba moja kwenye mchezo wa tennisi kwa upande wa walemavu na amechukua mataji mbalimbali ndani na nje.
Kwa upande wa wachezaji wa kike ambao siyo walemavu kwa tennisi anayefanya vizuri kwa sasa ni Edna John.
ZULFA MACHO
Huyu ni bondia maarufu wa ngumi akiwani kati ya mabondia wawili wa kike walioitwa kwenye timu ya taifa ya ngumi iliyoenda Accra Ghana kwa ajili ya michuano ya Afrika (All Africa Games) inayoanza Machi 15-23.
Zulfa ni mtoto wa zamani wa nyota wa soka aliyewahi kutamba na timu za Simba, Yanga, Mtibwa Sugar na Taifa Stars, Yusuf Macho ‘Musso’, kabla ya kuitwa kwenye michezo hiyo amewahi kufanya makubwa kwenye mchezo huo akitwaa taji ya UBO na kuwatembezea vitasa mabondia wenzao kuonyesha alivyo mahiri.