Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

SIKU YA WANAWAKE: Jeshi linaloibeba nchi kimataifa

Erge SIKU YA WANAWAKE: Jeshi linaloibeba nchi kimataifa

Fri, 8 Mar 2024 Chanzo: Mwanaspoti

Miaka ya nyuma ilizoeleka kushuhudia wachezaji wa kike kutoka Nigeria, Morocco, Afrika Kusini wakicheza karibu kila msimu Ligi ya Mabingwa Ulaya upande wa wanawake ni kama ilikuwa stori tu kwa wachezaji wa Kitanzania ambao msimu huu wa 2023/24, Aisha Masaka ameonyeshwa kuwa inawezekana.

Kwa miaka mingi wenzetu wa Nigeria wamekuwa wakitamba na Asisat Oshoala mmoja kati ya wachezaji bora wa Kiafrika ambaye amecheza soka la kulipwa Ulaya kwa miaka mingi akiwa na Liverpool na Arsenal za England, fundi huyo amebeba ligi ya mabingwa Ulaya kwa wanawake mara mbili akiwa na FC Barcelona.

Masaka ambaye anaichezea BK Hacken FF yenye maskani yake Gothenburg, Sweden amekuwa mchezaji wa kwanza wa kike wa Kitanzania kucheza michuano hiyo hivyo leo, Alhamisi ya siku ya Kimataifa ya Wanawake (IWD)inayoadhimishwa kila mwaka Machi 8 kama kitovu cha harakati za haki za wanawake, mshambuliaji huyo na wengine ambao wanacheza soka la kulipwa nje wanasimama kama mifano ya kuigwa.

Nyota hao wametambuka viunzi licha ya kuwa na changamoto nyingi lakini wanapambania ndoto zao kama ilivyo upande wa kaka zao ambao nao kila kukicha wanapambana kupiga hatua ili kuliweka soka la Tanzania kwenye ramani nzuri kama ilivyo kwa wenzetu wa Kaskazini na Magharibi.

Akiwemo Masaka hawa hapa nyote wengine sita wa Kitanzania ambao wanafanya makubwa nje ya nchi.

AISHA MASAKA (BK HACKEN FF- SWEDEN)

Japo alianza kwa kusumbuliwa na majeraha ambayo yalimfanya msimu uliopita kukaa nje ya uwanja kwa kipindi kirefu, Masaka amekuwa kwenye kiwango bora msimu huu ambao ameingia kwenye vitabu vya kumbukumbu vya Uefa kwa kuwa mchezaji wa kwanza wa kike kutoka Tanzania kucheza michuano hiyo upande wa wanawake.

Mshambuliaji huyo mwenye miaka 20, amefunga mabao matano kwenye ligi ya Sweden ‘Allsvenskan Women’ kwenye michezo 12 upande wa ligi ya Mabingwa kwa wanawake alifunga kwenye hatua za awali kabla ya chama lake kutinga hatua ya makundi ambapo amecheza mechi sita.

Katika moja ya mahojiano ambayo alifanya na gazeti hili, Masaka anaamini kwake Sweden ni njia tu ya kumfanya kucheza ligi kwenye mataifa makubwa zaidi kisoka barani Ulaya kama vile England, Hispania na hata Ufaransa.

“Mkubwa ni Mungu, nimekuwa nikiamini hivyo nguvu zangu huwa nazielekeza kwenye mazoezi huku nikimuomba kuwa anisaidie kwa sababu kwa akili na uwezo wangu ni ngumu, bado ninandoto za kucheza soka kwenye ligi kubwa zaidi,” anasema.

Katika hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa kwa wanawake, Masaka amecheza dhidi ya Chelsea (W) ya England, Rea Madrid (W) ya Hispania na Paris (W) ya Ufaransa hivyo alipata nafasi ya kwenda kwenye mataifa ambayo anatamani kucheza ligi zao.

CLARA LUVANGA (AL NASSR- SAUDIA)

Anatajwa kuwa mmoja kati ya wachezaji wa kike wenye vipaji vikubwa, kuna kipindi alikumbwa na matatizo (ilifichwa kumlinda) ambayo yalimfanya kushindwa kuonekana uwanjani kwa kipindi kirefu lakini wanasaikolojia walimjenga ndipo walipoibukia Hispania ambako alicheza kwa kipindi kifupi na kutua Saudia Arabia.

Agosti 2023, Luvanga alijiunga na timu ya daraja la Pili Hispania ya Dux Logrono.Alicheza mechi yake ya kwanza akiwa na uzi wa DUX Logrono Agosti 30 dhidi ya UDL na kuisaidia kuibuka na ushindi wa mabao 7-0, aliweka kambani mabao mawili na kuendelea kufanya vizuri kwenye michezo sita iliyofuata jambo ambalo liliwafanya matajiri wa Saudia kumwaga minoti ili kupata huduma yake.

Oktoba 2023, Luvanga alijiunga na timu ya Al Nassr ya Ligi Kuu ya Wanawake ya Saudia. Oktoba 13, alichezea Al Nassr katika ushindi wa 6-0 dhidi ya Al-Riyadh. Novemba 3, alifunga bao lake la kwanza, akifunga mabao mawili dhidi ya Eastern Flames.

Mshambuliaji huyo anatuzo ya bao bora kati ya 10 aliyofunga kwenye ligi hiyo na ndiye kinara na hapa anaeleza vile anatamani kuwa mfungaji bora.

“Ligi inaushindani mkubwa na kwangu haikuwa shinda sana kuendana nayo kwa sababu nilitoka Hispania, naamini kuna mengi yanakuja,” anasema.

ENEKIA KASONGA (FLAMES-SAUDIA)

Wamorocco wanamjua vizuri Enekia, akiwa na Ausfaz assa Zag alifunga mabao 49 kwenye michezo 41 kabla ya kwenda Saudia ambako anaichezea Eastern Flames.

Enekia ni miongoni mwa wachezaji ambao wanapigania vikumbo kwenye vita ya ufungaji bora kwenye ligi hiyo huku akikumbana na upinzani mkali kutoka kwa Luvanga.

Mchezaji huyo wa kimataifa wa Tanzania amefunga mabao sita.

JULIETHA SINGANO (JUAVARES - MEXICO)

Mwanasoka huyu alikuwa wa kwanza kuandika historia ya kuwa Mtanzania wa kwanza kucheza soka la kulipwa Mexico kwa upande wa wanawake. Kucheza soka nchini humo kunaifanya Ligi ya Tanzania kujulikana kwani timu hiyo inashiriki Ligi Kuu ya Wanawake ya Mexico, moja ya taifa kubwa kisoka.

Beki huyo kabla ya kujiunga na klabu hiyo aliwahi kuichezea Simba Queens na kuonyesha kiwango cha hali ya juu.

OPAH CLEMENT (BESKITAS - UTURUKI)

Opah mwenye mabao tisa kwenye michezo saba ya Ligi Kuu Uturuki kwa wanawake ni miongoni mwa mabinti wanaoiwakilisha vyema Tanzania.

Alijiunga na Beskitas ya nchi hiyo akitokea Simba Queens na aliondoka akiwa kinara wa wafungaji akiwa na mabao tisa kwenye ligi. Hii ni mara ya pili kwa Opah kucheza soka la kulipwa kwenye nchi hiyo Kayseri Kadin FK kabla ya kurudi nchini mwishoni mwa msimu uliopita na kuiwezesha Simba kutetea ubingwa wa WPL kwa msimu wa tatu mfululizo tangu ilipoipokea JKT ambao ndio mabingwa msimu uliomalizika wa ligi ya Bara na Cecafa.

Timu hiyo msimu huu inasaka ubingwa ili kupata nafasi ya kushiriki Ligi ya Mabingwa Ulaya kwa upande wa wanawake msimu ujao na kama itabeba ubingwa huo basi Opah atakuwa miongoni mwa wachezaji wanaoiwakilisha Tanzania.

DIANA MSEWA (AMED SPOR - UTURUKI)

Mwanadada huyo ambaye kwa sasa anakipiga Uturuki anaongeza idadi ya wanawake Watanzania wanaocheza soka la kulipwa nje ya nchi.

Diana ambaye ni kiungo aliwahi kucheza Ruvuma Queens kabla ya kujiunga na Amed Spor mwaka jana akianza kucheza Ausfaz ya Morocco akiwa na Mtanzania mwenzake, Enekia.

Chanzo: Mwanaspoti