Ruvu Shooting inashuka leo Jumatatu katika Uwanja wa Benjamini Mkapa kucheza dhidi ya Yanga, lakini mwenendo mbovu wa kikosi hicho umemfanya Kocha Mbwana Makatta kuwapa tizi mastaa wake mara mbili kwa siku, asubuhi na jioni.
Akizungumza na Mwanaspoti, jijini Dar es Salaam Makatta alisema nidhamu pekee ndio itakayowapa matokeo chanya katika mchezo huo na akikiri anaenda kukutana na moja ya timu nzuri kwenye Ligi Kuu Bara.
“Naamini maandalizi yamefikia asilimia 90 na kilichobaki ni mambo madogo madogo tu ya kiufundi, ni kweli hatujapata ushindi muda mrefu lakini bado tunaendelea kupambana kuona tunamaliza vipi,” alisema na kuongeza;
“Tunawaheshimu sana Yanga kwa sababu ina wachezaji wazuri na hata matokeo yao yanaonyesha ni timu ya aina gani, tutacheza kitimu zaidi ndiyo maana tulibadilisha programu ya mazoezi tofauti na hapo mwanzo,” alisema.
Kwa upande wa mshambuliaji wa kikosi hicho, Abalkassim Suleiman alisema mchezo huo ni mgumu kwao lakini kitu kikubwa ambacho wamekuwa wakielezana wao kwa wao ni kucheza kwa nidhamu kubwa na kuwaheshimu wapinzani wao.
Ruvu Shooting inakutana na Yanga ikiwa na mwenendo mbovu wa matokeo kwani imecheza michezo 15 mfululizo bila ushindi tangu mara ya mwisho ilipoifunga Coastal Union mabao 2-1 Septemba 29, mwaka jana katika Uwanja wa Uhuru.
Katika mchezo wa mwisho kwa timu hizo kukutana Yanga ilishinda mabao 2-1 Oktoba 3, mwaka jana ukiwa ni wa mzunguko wa kwanza wa ligi, huku mara ya mwisho Ruvu Shooting kuifunga Yanga ilikuwa ushindi wa bao 1-0 Agosti 28 mwaka 2019, lililofungwa na Sadat Mohamed.