Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Ruvu Shooting wazuiwa gesti, kisa deni

Ruvu Deni Ruvu Shooting wazuiwa gesti, kisa deni

Fri, 1 Mar 2024 Chanzo: Mwanaspoti

Wakati wakiwa kwenye hali mbaya katika Ligi ya Championship wakiburuza mkia kwenye msimamo, Ruvu Shooting wameendelea kukumbwa na majanga baada ya wachezaji wa timu hiyo kuzuiwa nyumba ya wageni kutokana na deni ya Sh22 milioni.

Wachezaji wa timu hiyo iliyoshuka Ligi Kuu msimu uliopita na kuuzwa kutoka Mlandizi, Pwani hadi mkoani Iringa, wamekumbana na kadhia hiyo wakati wakijiandaa na safari ya kwenda Mwanza kucheza mechi ya Ligi ya Championship dhidi ya Copco iliyopangwa kupigwa keshokutwa Jumapili, Machi 3, mwaka huu.

Mwanaspoti ilipenyezewa taarifa kwamba timu hiyo imezuiwa katika nyumba ya wageni ya Vanesa Lodge iliyopo Kihesa mjini Iringa kutokana na kushinikizwa kulipa malimbikizo ya deni la kukaa hapo linalozidi Sh22 milioni.

Mwandishi wa Mwanaspoti alitimba eneo la tukio na kuzungumza na mmiliki wa nyumba hiyo, Frank Nyalusi aliyesema deni hilo ni malimbikizo tangu Desemba, mwaka jana na amesema amekuwa akizungushwa kulipwa fedha hizo kila wakati alipokuwa wakiwakumbusha viongozi wa klabu hiyo, uongozi wa Mkoa wa Iringa pamoja na mstahiki meya ambao ndio walezi wa timu hiyo.

Nyalusi amesisitiza kwamba hatawaruhusu wachezaji hao kuondoka hadi alipwe pesa hizo na mstahiki meya wa Manispaa wa Iringa, Ibrahim Ngwada ambaye ndiye anayemtambua kama mtu aliyeinunua Ruvu Shooting kutoka Pwani kuileta Iringa.

Hata hivyo, Meya Ngwada amemuomba mmiliki wa nyumba hiyo kumvumilia na akimaliza vikao yeye na Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Halima Dendego watazungumza naye ili kuweka mambo sawa.

Mwanaspoti itaendelea kuwaletea taarifa zaidi ya sakata hilo linalofanana na lililowahi kuzikuta Ndanda na Majimaji zilizotamba kwenye Ligi Kuu Bara kutokana na madeni ziliyokuwa zikikabiliwa nayo kabla ya viongozi wa mikoa husika na timu hizo kuingilia kati na kuzifutia aibu.

Ruvu imekuwa na matokeo mabaya, licha ya imani kubwa waliyokuwa nayo wana Iringa ambao waliichukua timu hiyo kuziba nafasi ya Lipuli kwani hadi sasa imecheza mechi 22 na kushinda moja tu, ikitoka sare tano na kupoteza 16, ikifunga mabao 11 tu na kufungwa 43 na kukusanya pointi nane tu zinzoiweka kwenye janga la kushuka kwenda First Division kwa msimu ujao.

Chanzo: Mwanaspoti