Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Ruvu Shooting wamtangaza Makata kumrithi Mkwasa

Mbwana Makata Mbwana Makata

Tue, 6 Dec 2022 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Timu ya Ruvu Shooting imemtangaza Mbwana Makata kuwa kocha mkuu wa kikosi hicho baada ya Charles Boniface Mkwasa kubwaga manyanga.

Matokeo mabaya hasa katika mechi 10 za mwisho za mzunguko wa kwanza yanaelezwa kuwa ndio chanzo cha Mkwasa kuamua kujiuzulu nafasi yake kwani katika mechi hizo Ruvu ilivuna pointi moja tu iliyopata katika sare dhidi ya Prisons na mechi tisa ikipoteza zote.

Makata anaingia kuinoa Ruvu Shooting baada ya kumaliza adhabu yake ya kufungiwa miaka mitano na Shirikisho la soka Tanzania(TFF) kwa kugomea kuingiza timu uwanjani katika mchezo wao dhidi ya Namungo msimu uliopita wakati akiinoa Mbeya Kwanza. Hata hivyo alipunguziwa adhabu na kutakiwa kutumikia kwa miezi sita baada ya kuomba radhi.

Msemaji wa Ruvu Shooting, Masau Bwire amesema wamehuzunishwa na uamuzi aliouchukua Mkwasa kwani waliamini matokeo mabaya waliyokuwa wanapata ni kipindi cha mpito.

"Tulikuwa na kocha wetu Charles Mkwasa na kwa hakika kazi yake tuliifurahia na kuipenda sana na hakuna Mtanzania asiyejua kazi ya yake katika kufundisha mpira.

"Mkwasa ameandika barua kwa uongozi ya kuuomba kuachia ngazi kutokana na mwenendo na matokeo ya timu hasa katika mechi 10 za mwisho za mzunguko wa kwanza ambazo tumeambulia pointi mojatu jambo ambalo halijawahi kutokea," amesema Masau na kuongeza;

"Mwalimu nadhani akaona apumzike kwa hiari yake licha ya kwamba tumepokea kinyonge uamuzi huo kwa sababu bado tulimuamini na tulijua ni changamoto za kawaida ambazo ipo siku hasa mzungukoo wa pili zingeisha na tungeanza kufanya vizuri," 

Masau amesema huwa hawaamini kuwa timu kufanya vibaya kidogo ndio wakimbilie kumlaumu mwalimu.

"Tuliwahi kushuka mwaka 2014 tukiwa na kocha Tom Olaba lakini hatukumuacha tuliendelea nae hadi daraja la kwanza na akaipandisha tena timu, hivyo timu kupata matokeo mabaya huwa hatukimbilii kumfukuza kocha bali tunaangalia wapi kuna tatizo na tunalitatua," amesema.

Masau amesema baada ya Mkwasa kuandika barua ya kujiuzulu, walianza harakati za haraka kutafuta kocha mbadala na kumpata Makata.

"Makocha wetu wapya, Makata na kocha msaidizi Renatus Shija tayari wako kambini kuendelea na mazoezi na timu ili mzunguko wa pili turejee kwa nguvu kubwa," amesema Masau.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live